Sunday, March 14, 2021

MAAMUZI MAGUMU YANA GHARAMA , NDIO NJIA YENYE MATOKEO BORA KATIKA MAISHA.

Ukiangalia maisha yako utajishukuru kuwa katika maamuzi magumu ulowahi kuyafanya ndio yalokujengea uimara au kukupa mabadiliko makubwa maishani mwako. Ukiangalia unaona namna bila kuamua maamuzi magumu pengine usingekuwepo ulipo sasa. Maamuzi magumu hayaanza kufanyika sasa ila toka zama zilizopita miaka 2000 huko Ugiriki ambapo tunakutana na habari za Mgiriki aitwaye Demosthenes.

Demosthenes alizaliwa mwaka 384 kabla ya Kristu huko Ugiriki ya Zamani. Utoto wake alizaliwa mtu ambaye alikuwa si imara katika mwili wake, alikuwa na tatizo la kutamka au kigugumizi na tatu alipoteza wazazi wake ambapo walezi walipora mali za urithi zote alizoachiwa na baba yake ambazo zilkuwa dola milioni 11 za Kimarekani sawa na shilingi bilioni 25 na milioni 454 kwa sasa. Walezi walichomwachia ni nyumba ndogo tu na pesa wakaondoka nazo. Hali hii alopitia Demosthenes hata leo inajitokeza ambapo watoto wanaachiwa mali na wazazi wao ila ndugu au walezi wanatumia nafasi kudhulumu haki zao.

Maisha ya Demosthenes yangetosha kukata tamaa na pengine kutoona mwelekeo wa siku zijazo. Akiwa katika huo huo umri mdogo kabla ya miaka 20 alifanya maamuzi magumu ambayo yamebakia historia katika maandiko ya Kigiriki na hata leo tunamsoma kujifunza kwake. Maamuzi makubwa matatu aloyafanya ambayo yalimwinua kuwa moja ya wazungumzaji nguli kuwahi kutokea huko Ugiriki huwezi msahau Demosthenes na pia inasemekana ni moja ya waanzilishi wa sanaa ya uzungumzaji Duniani.

Demosthenes alipenda sana uzungumzaji licha kuwa na kigugumizi ila hilo halikuzuia kuamua kujifungia chini ya handaki na kunyoa nusu ya nywele katika kichwa ili asitoke nje. Ndani ya handaki alikuwa akisoma kwa kina vitabu kuhusiana na siasa, tamaduni za kigiriki na maarifa mengi.

Pili aliamua kujifunza kuzungumza huku akiwa na vijipande vidogo vidogo vya mawe mdomoni huku akikimbia. Zoezi hili halikuwa jepesi kwake kuwa unarudia rudia sentensi za kuzungumza huku na vijimawe na unakimbia katika upepo mkali. Maamuzi haya yalichangia kuzalisha mzungumzaji bora kuwahi kutokea Ugiriki. Zoezi lingine alikuwa akizungumza na huku anajitazama katika kioo mara kwa mara.

Maamuzi magumu aloyafanya Demosthenes ni mwaliko wa maisha tunayoishi sasa kuwa ili tuvuke hatua fulani kubwa katika maisha lazima tuwe tayari kulipa gharama ya kufanya maamuzi magumu ambayo yanaweza kutugharimu kwa muda ila yakazalisha matokeo makubwa siku zijazo. Unaweza kuwa unatamani kuwa na maisha bora ila unaogopa kufanya maamuzi magumu kuhusu maisha yako kwa kuanzisha mfumo wa maisha wenye kuhitaji ujitoe, ujitose, ujikaze na usijihurumie ili kuzalisha matokeo bora.

Maamuzi magumu yatakutisha na kukuogopesha sasa ila utakapoweza kuvuka njia ya maamuzi magumu hutabakia mtu wa kawaida. Fanya maamuzi magumu kwa chochote kile ukijua kwa kufanya maamuzi magumu hayo kuna mchakato utapitia utakaokuwa na maumivu ya muda ila wenye matokeo mazuri baadaye. Changamoto ni njia kwa watu wanaishi falsafa na changamoto hazikimbiwi.

KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

WhatsApp + 255 716 924136 /  + 255 755  400 128

 

No comments:

Post a Comment