Monday, March 22, 2021

TUMEUMBIWA MASIKIO MAWILI NA MDOMO MMOJA. KUWA MSIKILIZAJI SANA KULIKO KUONGEA.

Tumeumbiwa masikio mawili na mdomo mmoja ambapo masikio mawili tusikilize zaidi na mdomo mmoja kuongea kidogo. Wale wanaosikiliza zaidi hupata mengi kupitia wale wanaongea. Kuongea sana ni kujipa nafasi ya kurudiwa na kile unachoongea na kujikuta unachoongea kisiwe halisia na kile unachokifanya. Tafiti fulani zilifanyika na kuonesha kuwa kadri unavyoongea juu ya mipango yako au kitu chochote ndivyo ilivyo nafasi ndogo ya kukifanya au kukitenda. Hili ndo limezalisha na kuwa ukiona mtu ni muongeaji sana basi ni mtendaji kidogo. Watendaji wengi si waongeaji ukilichunguza hili utaona.

Akiba ya maneno ni ya muhimu mno katika zama tuishizo sasa kuliko zile zilizowahi kuwepo. Tunaishi katika mifumo ya kumbukumbu kupitia mitandao ya simu kiasi kwamba yale ambayo tunayaandika au kuyaongea watu huyahifadhi na baadaye huyatumia kama fimbo au hukumu unapokuwa umeyasaliti maneno yako. Watu huwa hawafikirii namna neno huishi zaidi ndani ya wale wanaosikiliza.

Kuongea ni kujiandalia mtego hasa hasa pale unapotaka kuchangia mazungumzo fulani ya mambo. Kuongea sana kunapelekea mtu aanze kuongea vitu visivyo kweli ili wale wanaomsikiliza waendelee kumsikiliza. Watu wengi wamefungwa kwa maneno yao ambayo walishindwa kujizuia kuongea. Kusikiliza kunaepusha migorogoro mingi sana katika maisha ya watu na ndiko kunakozalisha watu kuwa na hekima.

Inaleta maswali mengi kuwa tupo katika zama ambazo kila mtu anasukumwa kuongea, kutoa maoni na tunakosa watu ambao huwa kimya na wasikivu kipindi ambacho kila mmoja anasukumwa kuongea ongea. Utaona namna katika majukwaa mbalimbali ya mtandaoni watu wasivyo na subira katika kuyazungumza mambo au kuyaongea. Kila mmoja anaona atapitwa kuongea juu ya jambo fulani au tukio fulani. Katika kufanya hili watu wengi wamepoteza utulivu wa maisha na kujikuta wanahangaishwa na kile walichokiongea kinapoenda tofauti na namna wanavyoishi sasa.

Huwa ninafaidika sana katika mazungumzo ninapokuwa msikilizaji. Ninapokuwa nasikiliza iwe ni mazungumzo ya watu, mijadala au watu watoa maoni napata mengi mno nilokuwa sijajui kupitia kusikiliza watu wanaozungumza au kuongea. Kusikiliza kunatengeneza yule anayeongea aone anathaminiwa tofauti na mtu mmoja anaongea na mwingine analeta mazungumzo kati kati.

Kama wanafalsafa tujiepushe na kuongea kama watu wengine ambao wanakosa udhibiti wa kujizuia kuongea kwa kila wanachokiona. Pili ni kuongeza nafasi ya kuwa wasikilizaji maana hata katika kusikiliza ndipo kunakozaliwa ufahamu wa mambo. Mtu anayesikiliza vizuri huweza hata kufafanua alichokisikia. Si lazima uongee kwa kila kinachotokea hususani zama hizi tuishizo za usumbufu, kelele na mihemko kila kona.

NA   KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.
 ( WhatsApp + 255 716 924136  )  /  + 255 755 400 128
EMAIL :  japhetmasatu@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment