Thursday, February 21, 2019

MUDA WA KUANGALIA TELEVISHENI , KUOGA, KULA TUNAO !! LAKINI LINAPOKUJA SUALA LA KAZI, BIASHARA , KUSOMA VITABU VISINGIZIO VINGI.

Kwenye maisha yetu ya kila siku, vitu vyote muhimu huwa hatuvifanyi mara moja na kuachana navyo, bali huwa tunavifanya kila siku. Na hakuna hata siku moja ambayo tunajiambia tumechoka na hivyo hatufanyi.


Fikiria yale tunayofanya kila siku ili maisha yetu yaende, unakula kila siku, unapumua kila siku, unasafisha mwili wako kila siku, na hata nyumba au nguo zako, unasafisha kila mara.


Lakini inapokuja kwenye kazi na biashara, huwa tunajipa kila aina ya sababu kwa nini tusifanye kwa baadhi ya siku. Huwa tunachukulia kazi na biashara zetu kama kitu cha ziada kwenye maisha yetu na siyo maisha yetu.


Kadhalika vitu kama kujifunza, mfano kusoma vitabu. Utasikia watu wakisema kabisa kwamba hawasomi vitabu kwa sababu hawana muda. Lakini hutawasikia watu hao wakisema wana siku mbili hawajala kwa sababu hawajapata muda.


Kwa kila kilicho muhimu kwenye maisha, huwa tunapata muda wa kukifanya, hata kama tumebanwa kiasi gani.


Hivyo ninachotaka uondoke nacho hapa rafiki yangu ni hiki, chagua vitu ambavyo lazima kila siku utavifanya na uvifanye kweli bila ya kusingizia muda au kuchoka. Na ukiacha vile ambavyo tayari unafanya ili uwe hai, kama kula na kadhalika, ongeza vitu kama kujifunza, kufanya majukumu yako na kukuza vipaji au kile unachopenda.


Kama wewe ni mwandishi basi hakikisha kila siku unaandika, usikubali siku ipite hujaandika. Na wengine kwa nafasi zao za kazi au biashara, hakikisha kila siku kuna kitu unakifanya cha kukufanya uwe bora zaidi.

No comments:

Post a Comment