Saturday, December 22, 2018

TUMIA VIGEZO HIVI VITANO ( 5 ) KUYAFIKIA MALENGO YAKO.

(1).LENGO LINAPASWA KUWA MAALUMU (SPECIFIC).
Kigezo cha kwanza muhimu kwenye kuweka malengo ambayo utayafikia ni umaalumu wa lengo husika. Unapaswa kuweka lengo ambalo linaeleweka ni nini hasa unachotaka.
Unapaswa kujua ni nini kwa hakika unachotaka kwenye lengo hilo, unakipata wapi, utashirikiana na nani, kwa nini unakitaka na hatua zipi unapaswa kuchukua.
Tukienda kwenye mfano wetu wa fedha, usiweke lengo kwamba nataka fedha zaidi, au nataka kuwa bilionea. Unapaswa kuweka kiasi cha fedha unachotaka na kujua utakipataje kwa hatua zipi unazopaswa kuchukua.
Utaona tofauti kubwa kati ya hali hizo mbili, unaposema unataka fedha zaidi, ukipata elfu kumi ambayo hukuwa nayo ni fedha zaidi. Lakini unaposema unataka milioni 50 au bilioni moja, hapo sasa unakuwa na uhakika nini unataka.
Usiweke malengo yanayoelea hewani, jua kabisa nini unataka na nenda mbali zaidi kujua unakipataje na kwa kufanya nini. Pia unapaswa kuwa na kwa nini inayokusukuma kufikia lengo hilo.

(2). LENGO LIPIMIKE (MEASURABLE).
Kigezo cha pili kwenye kuweka malengo utakayoweza kuyafikia ni kila lengo linapaswa kuwa linapimika. Hapa unapaswa kuona kabisa ni jinsi gani kupata kile unachotaka kutabadili maisha yako.
Pia unapaswa kuligawa lengo lako kubwa kwenye hatua ndogo ndogo ambazo unaweza kuzitumia kupima maendeleo yako kwenye lengo hilo.
Kwa mfano kama lengo lako ni kupata milioni 50 kwa mwaka, unaweza kuligawa kwa miezi 12 na ukapata kama milioni 4 kwa mwezi, hii inakuwa rahisi kwako kujipima kila mwezi kuona unaelekeaje kwenye lango lako.
Kuweza kuligawa lengo lako kubwa kwenye hatua ndogo ndogo zinazopimika kutakuondolea kukata tamaa pale lengo linapoonekana ni kubwa sana.
Hakikisha kila lengo unaloweka unaweza kupata taswira ya ukiwa umelikamilisha kisha ligawe kwenye hatua ndogo ndogo ambazo ni rahisi kwako kupima.

(3). LENGO LIWE NINAFIKIKA (ATTAINABLE).
Kigezo cha tatu ni lengo liwe linafikika. Tumekuwa tunayaelewa sana mafunzo ya maendeleo binafsi ambayo yanatufundisha kwamba ndani yetu tuna uwezo mkubwa na tunaweza kufanya chochote tunachotaka kufanya. Hili ni kweli kabisa kwamba tuna uwezo mkubwa na kuweza kufanya chochote tunachotaka.
Lakini inahitaji muda, nguvu na hata vipaji kufikia lengo lolote tunalojiwekea. Hivyo unapoweka lengo, lazima ujiulize je kwa muda, nguvu, rasilimali na hata vipaji ulivyonavyo utaweza kufikia lengo hilo? Kama siyo unajidanganya.
Kwa mfano kama mwaka huu kipato chako ni shilingi milioni moja kwa mwezi, kujiambia kwamba mwaka kesho unataka upate bilioni moja ni kujidanganya na kujiandaa kushindwa. Ni kweli lengo la bilioni moja linafikika, lakini linachukua muda, na linahitaji jitihada zaidi.
Kwenye kila lengo unalojiwekea, angalia rasilimali ulizonazo kisha weka lengo kubwa ambalo litakusukuma, lakini lisikukatishe tamaa.

(4). LENGO LIWE NA UHUSIANO NA KUSUDI LA MAISHA YAKO (RELEVANT).
Kigezo cha nne kwenye kuweka malengo utakayoyafikia ni lengo liwe na uhusiano na kusudi la maisha yako. Mara nyingi wengi wamekuwa wanaweka malengo ambayo siyo yao. Kwa sababu wamesikia wengine wakiweka malengo hayo basi na wao wanaona inabidi wayaweke la sivyo wataachwa nyuma.
Watu wengi wamekuwa wanafuata mkumbo kwenye uwekaji wa malengo, wanaweka malengo ambao hayahusiani kabisa na lile kusudi walilonalo kwenye maisha. Wanapokuja kugundua hili wanashindwa kuendelea na malengo yao.
Kwenye kila lengo unalojiwekea, hakikisha linaendana na kusudi kubwa la maisha yako. Hata kama ni lengo kubwa kiasi gani, kama halitokani na kusudi lako kubwa, utaishia kushindwa.
Usijiambie unataka kupata mabilioni ya fedha kupitia biashara fulani ambayo inaonekana kuwa yenye faida kubwa, wakati wewe unapenda kufanya kitu kingine tofauti kabisa. Lengo unaloweka liendane na kile unachopenda na kujali kufanya.

(5).LENGO LIWE NA UKOMO WA MUDA (TIMELY).
Kigezo cha tano katika kuweka malengo ambayo utayafikia ni kuwa na ukomo wa muda. Wote tunajua jinsi ambavyo ukomo wa muda unavyotusukuma kuchukua hatua. Watu wanaweza kupewa nafasi ya kufanya kitu kwa muda mrefu lakini wasifanye, inapofikia tarehe ya ukomo ndiyo kila mtu anafanya.
Tumia nguvu hii ya ukomo wa muda kwenye malengo unayoweka, kila lengo liwe na ukomo wake wa muda na ujikumbushe ukomo huo ili uweze kujisukuma kufanya zaidi na kufikia lengo hilo. Kwenye kila lengo ulilogawa kwenye hatua ndogo, jiwekee ukomo kwenye kila hatua na ufuate ukomo huo.
Kama umejiambia unataka kupata bilioni moja ndani ya miaka kumi, basi gawa kiasi cha kupata kila mwaka, kila mwezi, kila wiki na hata kila siku, kisha weka muda wa kufuatilia kila kiwango unachotaka kupata ili kuona maendeleo yako yakoje.
Rafiki, hivyo ndivyo vigezo vitano muhimu unavyopaswa kuvitumia kuweka malengo ambayo kwa hakika utayafikia. Tumia vigezo hivi katika kila lengo unaloweka na utaona jinsi utakavyolielewa lengo lako vizuri, kuona kila hatua unayopaswa kuchukua na kuwa na msukumo wa kuchukua hatua kabla muda uliojiwekea haujaisha.

No comments:

Post a Comment