Tuesday, February 9, 2021

UNAPOJIANDAA KUUMIZA WENGINE , JIANDAE KUJIUMIZA WEWE MWENYEWE.

Tupo katika jamii ambayo watu huoneana wivu, hujenga chuki, wasopenda upendo na hata kupanga njama za kuharibiana maisha. Ila katika yote haya yanayofanyika watu wanasahau kuwa kwa kila jaribio baya dhidi ya mtu mwingine ni kuandaa mazingira ya kuumia wenyewe. Hujaona namna unapokuwa na kinyongo dhidi ya mtu fulani jinsi kinyongo hicho na wewe kinavyokuumiza hata kabla ya kuwafanyia wengine. Wengi huwa hatujui kuwa kwa lolote tunalopanga kuwaumiza wengine tunaanza kuumia kwanza sisi kabla ya hao watu hawajaumizwa.

Falsafa inatufundisha namna umuhimu wa kuishi kwa mashirikiano na watu wote. Inagusa namna maisha yetu ni mategemeano yaliyo sawa kabisa na viungo vya mwili katika mwili. Uwepo wa watu wanaotuzunguka hatuna namna ya kukataa uwepo wao mbali na kujifunza namna ya kuishi nao, kuwaelewa na kusaidiana. Uwepo wa hasira, chuki, visirani na vinyongo ni kutojua maisha yetu yamekuwepo kwa ajili ya uwepo wa watu wengine wanaotuzunguka.

Jamii nyingi zinazoingia katika migogoro huwa zimekosa kujua namna maamuzi mabaya au ya kiuonevu yalivyopanda mbegu ya chuki na hasira inayokuja kujirudia na kuwadhuru na wao pia. Ni kitu kigumu kuishi kwa Amani endapo umefanya jambo liloharibu Amani kwa watu au kuwaumiza wengine. Ndani ya mtu anayefanya ubaya hawezi kusema ana uhuru ndani yake bali ni kuwa katika vifungo na kuanza kuona matokeo au athari ya ubaya wake dhidi ya watu wengine.

Kama ilivyo katika suala la upendo linavyozalisha upendo ndivyo chuki inavyozalisha chuki. Kanuni ya asili inayosema kisababishi na matokeo “law of cause and effect” hufanya kazi katika maisha yetu kwa nguvu kubwa. Kuwa chochote utakachokifanya kitazalisha matokeo. Ukijenga chuki basi utatengeneza nafasi na fursa nyingi chuki ijengeke na kukurudia kukudhuru na wewe.

Kuumiza wengine inaweza kuwa kuwanyima nafasi ambazo wangepewa hizo nafasi au maarifa huenda wangekusaidia na wewe pia. Ila kwa kuwa hatujui chochote tunachokifanya kwa wengine tunajifanyia sisi wenyewe hilo tunapuuza. Unapokosa kufundisha wengine kuishi vizuri, kuwajengea misingi mizuri ndivyo unavyojitengenezea mzigo mkubwa hapo baadaye utakaokurudia. Hili utaliona katika maeneo ya kazi, elimu na uongozi ambapo walotangulia si wepesi kuwafundisha wengine njia angali bado wana nguvu. Ila kwa baadaye hutokea hawana watu chini yao ambao wangekuwa msaada au daraja baada ya wao kuchoka au kuumwa.

Marcus Aurelius anasema “When others try to hurt you, they hurt themselves”. Hii ikiwa na tafsiri kuwa “Tunapokuwa tunawaumiza wengine, basi tunajiumiza sisi wenyewe”. Unaposhindwa kusamehe mtu ndivyo unavyojikuta wewe usiyesamehe ukiumia zaidi kuliko hata aliyekukosea au huenda aliyekukosea hata hajui kama unaumia. Unaposhindwa kusahau yalopita si kuwa unaukomoa muda ila unajiumiza wewe mwenyewe ndani kwa kuendelea kuumizwa na kumbukumbu. Chochote kile unachokifanya unakifanya kikurudie wewe mwenyewe. Ukitenda baya utavuna baya na ukitenda jema utavuna jema. Dunia haidanganywi kwa lolote kukupa kile unachokifanya kwa wengine.

KOCHA   MWL.JAPHET   MASATU

WhatsApp +255 716924136 )  /   * 255 755400128

 

No comments:

Post a Comment