Saturday, February 20, 2021

JIANDAE KWA CHANGAMOTO / MATATIZO / MAGUMU UKIWA BADO UNZAO NGUVU SASA.

Aliyekuambia kuwa njia ya maisha itakuwa nyepesi huenda alikuficha ukweli kuhusu maisha yalivyo. Maisha ni njia yenye kukabiliana na magumu siku hadi siku. Kadri unavyoendelea kuishi na kuelekea uzee ndivyo magumu kuhusu maisha yanaweza kuonekana wazi wazi kabisa ikiwa maandalizi hayakuwepo. Uzee una changamoto zake na ni wakati ambao kinga za mwili zinakuwa dhaifu, mwili umechoka na ufanisi wa vitu vingi vinakuwa viko chhini. Uimara katika maisha ni muhimu sana ili kuhimilia yajapo magumu.

Maandalizi katika maisha yanahitajika tena zaidi wakati ambao mambo hayajawa mabaya au kuwa magumu. Maandalizi wakati mambo tayari ni mabaya au magumu si wakati ufao wa mapambano na watu wengi hushindwa na kukata tamaa nyakati kama hizi. Ijapo kuwa wengi wanajua umuhimu wa maandalizi ulivyo ila si wote wanachukua hatua za kujiandaa mambo yanapokuwa mazuri au rahisi. Kujiandaa kihisia, kiuchumi, kifikara na kiroho huwa na matokeo mazuri wakati mambo yapo shwari.

Kifalsafa tunajiandaa na magumu wakati ambao upo na nguvu zako za mwili, akili na hisia. Unajiandaa kwa magumu kwa kujaribu kuishi kama magumu yameshajitokeza. Hili unalifanya kwa kuthubutu kufanya vitu ambavyo utaweza kuhimili ukiwa nyakati ngumu. Hapa unafanya zoezi la kuruhusu kitu ulichokuwa unakihofia kwa kuanza kukifanyia mazoezi sasa. Zoezi muhimu ni kuishi ukiwa kama umepoteza kila kitu ulichonacho sasa au kuishi katika mazoezi ya kujinyima ingawa una kila kitu.

Jifunze kujinyima unapoweza kwa kuacha vitu ulivyokuwa unaweza kuvifanya. Una utajiri ila jifunze namna ukiishiwa inakuaje. Una watu wanaokuzunguka ila jifunze kuishi kama watu wote waliokuzunguka wameyapoteza maisha yao. Jifunze kujitegemea wewe mwenyewe. Jinyime na punguza kiasi unachokula licha una utajiri wa chakula. Fanya mazoezi haya angalau mara moja katika mwezi au miezi mitatu. Jinyime wakati mwingine kwa kujipumzisha kuwa katika mitandao ya kijamii na ishi kama haupo katika dunia ya kidijitali. Kujifunza haya endapo magumu yakijitokeza hayo maeneo hutashangazwa kabisa na hilo.

Jifunze kuishi nje na matarajio na fanya chochote kile bila matarajio yoyote yale. Fanya kazi na usitegemee pongezi, saidia mtu na usitegemee kusaidiwa, wainue wengine na usitegemee wengine wakuinue. Kujifunza namna hii ni kujiandaa endapo matarajio yako yakienda tofauti hutaumizwa hisia zako au maisha yako. Jiondoshe na matarajio kwa chochote kile na wakati mwingine tegemea mambo yanaweza kwenda vibaya. Kujiandaa huku ni kujiepusha na maumivu ya hisia pale kinyume na matarajio kunapojitokeza.

Unafanya haya mazoezi kujenga ujasiri na uimara zaidi ili yanapojitokeza magumu yoyote unakuwa tayari ulishafanya mazoezi hayo ya kutosha. Ikitokea mitandao ya kijamii inazimwa hutapata shida maana ulishajifunza kuishi pasipo mtandao, ikitokea chakula hakipo au ukame basi mwili ulishajifunza kuishi katika wakati mgumu wa kukosekana kwa chakula. Jifunze haya kila siku ili usishangazwe na chochote kile maishani. Usipokuwa imara magumu yakijitokeza yatakuumiza na kukuharibu.

NA   KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU

WhatsApp  + 255 716924136   /  +   (  + 255 755 400128  )


 

No comments:

Post a Comment