Sunday, February 7, 2021

ISHI KAMA MKONDO WA MAJI , SIRI YA KUISHI KWA AMANI NA FURAHA.

Tunacheleweshwa katika maisha kuyaona kama zawadi kwa mambo mengi ambayo bado tumekuwa wazito kuyaacha yapite na turuhusu kuona thamani ya wakati tulio nao sasa. Ugumu mwingine ambao watu wanajitengenezea ni huu wa kuendelea kushikilia vitu au mambo yalokwisha kupita. Walio huru na kufurahia maisha ni wale wote ambao muda ukipita basi wanaruhusu nayo mambo yapite.

Naamini katika maisha yako umewahi pita eneo la mto au hata kuona mfereji wa maji unaopita katika mkondo wake. Ukitulia na kuangalia kwa macho yako mawili utaona namna maji yapitavyo na ikiwa utaweka kitu juu au kurusha ndani ya maji hayo hubebwa na kusafirishwa. Hili si ajabu kuona namna mikondo ya maji hukusanya vitu toka eneo lingine na kwenda kupeleka eneo lingine. Hili ni somo pana na kubwa la kifalsafa linalofundishwa na asili namna ya kuachilia vitu na tuviruhusu kupita.

Wangapi umekutana nao wakiwa na kauli za mambo yalopita au bado kufikiri kwa habari zilizopita. Wangapi ambao hadi sasa wameshindwa kuchukua hatua kwa sababu ya kuweka lawama kuwa asingekuwa fulani nisingekuwa maskini au kuwa hapa leo. Kauli za kujikatisha tamaa na kuendelea kuzitumia ziendelee kuwa na nguvu hata muda uwapo umepita kimekuwa kikwazo kwa watu wengi kuona wanahitaji kubadilika na kuanza maisha mapya na kuruhusu kufurahia wakati wa sasa. Utafungwa na nyakati zilizopita hadi lini kwa kushindwa tu kuachilia ili uruhusu upya ndani ya maisha yako ?

Nimekuja kugundua namna nilivyokuwa nikiachilia mambo yapite ndivyo nilivyokuwa naachia nafasi ya kufurahia maisha, kuwaza kutofauti na kuishi kwa utulivu mkubwa wa ndani. Si mimi pekee huwa naliona hili hata kujifunza kwa watu wengine wenye maisha imara, utulivu na furaha ni watu ambao huachilia mambo wanayokutana nayo. Kuachilia kwao kwa mambo na matukio wanayokumbana nayo maishani kumewazawadia utulivu na maisha ya furaha wakati wote.

Ukiishi namna mto unavyobeba vitu na kuvipitisha hutosumbuliwa na chochote kile. Wakati watu wanaendelea kufikiri yalopita wewe utakuwa ukitumia sasa yako vizuri na kuifurahia. Utakapokuwa unaruhusu kuachilia vitu vipite utakuwa ukitengeneza akili tulivu na kuepusha msongo wa mawazo ambayo ni hali inayowasumbua maelfu ya watu kwa kushindwa tu kukubali na kuachilia mambo.

Mstoa Marcus namnukuu “A person can stand by a mountain stream and insult it all day long—the stream remains pure. Even if they throw dirt into it, the dirt is quickly dispersed and carried away. Let your soul be like that stream—flowing freely, simply, and contentedly”, Hii ikiwa na maana “Mtu anaweza kukaa katika mkondo wa maji mlimani na akatukana siku nzima juu ya mkondo wa mto nao usiseme kitu. Hata ikiwa mtu atatupa uchafu ndani yake, si muda uchafu utasombwa na kuchukuliwa. Hebu chukulia nafsi yako iwe kama mkondo, mkondo ulio huru”. Maneno haya ni mazito na kuyatafakari kwa kina namna umuhimu wa kuachilia nyakati zipite na mambo yapite.

Chochote kile utakachokutana nacho maishani jua kuwa kitapita endapo utaruhusu kipite kama ulivyo mkondo wa maji upitishavyo vitu. Hili litakusaidia kukufanya uwe imara, mwenye furaha na kushiriki katika zawadi ya maisha kikamilifu.

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU

WhatsApp +255 716924136 /  +  255 755400128   /  + 255 688 361 539


 

No comments:

Post a Comment