Moja ya masomo ya
msingi kabisa wanayofundishwa wajasiriamali, hasa pale wanapojiandaa
kupata mikopo ya kuendeleza au kuanzisha shughuli fulani, ni utunzaji wa
vitabu. 'Vitabu' katika biashara inamaanisha kufahamu mtiririko halisi
wa fedha, kwani kila bidhaa na kila huduma inayotolewa kibiashara
inahitaji kulipiwa, na malipo hayo yaonekane au yafahamike ili
kumbukumbu hiyo iweze kutumika kupima mwendo wa biashara husika.
Imekuwa ni kianzio cha mafunzo takriban yote ya biashara; ina maana kuwa
kila mmoja anahitaji kufanya hivyo.
Ukiangalia kwa karibu
biashara inayofanyika unakuta kuwa maelezo hayo siyo sahihi, kwani kuna
biashara nyingi ambazo hazina vitabu kabisa, au kimsingi havihitajiki,
Kitabu cha kwanza cha mfanyabiashara ni akili timamu na kutokuwa mlevi
au amechoka hajapata usingizi wa kutosha, hivyo aanze kujisahau katika
kurudisha fedha kwa mteja, n.k. Unapoondoa udhaifu wa wazi kama huo
katika shughuli zake kulingana na biashara anayofanya, kinachobaki ni
'kuweka kichwani' nini kimetangulia na nini kinafuata, na siyo kuandika
katika kitabu ili akumbuke.
Mtu anapoizoea
biashara, cha kufanya kinaonekana katika mazingira yake wakati ule ule,
na hakitokani na matumizi ya rejea ya aina moja au nyingine. Mara
nyingine kanuni zinatokana na watu wanavyoishi eneo fulani, na hata
ngazi ya biashara yenyewe. Kwa mfano utaingia katika mgahawa unaona kuna
tangazo 'lipa kwanza,' lakini kila mtu anaagiza chakula na baadaye
analipa, ambayo ina maana kuwa wafanyakazi wameona kuwa kufuatilia
tangazo hilo inakuwa usumbufu kwa wateja. Pale wanapoenda kwingine
hakuna kanuni hiyo ya 'lipa kwanza' kwa jazba.
Ipo kwa mfano kanuni ya
kukopa ambayo pia inapigiwa kelele katika maeneo mengi, ambako
ushindani wa kanuni unajitokeza, na si rahisi kusema ni ipi inatumika
wakati gani, kwani haipo inayotumika wakati wote. Wako wanaodhani
kukopesha ni kufukuza wateja kwani deni likiwa kubwa atakimbia, lakini
wako wengi wanaofahamu kuwa mteja anayefanyiwa fadhila ya kukopeshwa
anaweza kubaki mteja wa duka hilo kwa muda mrefu au kwa mahitaji yake
yote ya aina hiyo. Ni suala pia la kuangalia mteja mwenyewe, unavyoweza
kumwamini, au la.
Suala la umuhimu wa kutunza vitabu katika kila aina
au takriban aina zote za biashara linatatuliwa kwa kurejea msemo mmoja
wa Waingereza, unaosema "chukua tahadhari kuhusu mapeni, noti
zitajilinda zenyewe." Ina maana kuwa unapotoa chenji sahihi kwa malipo
sahihi ya bidhaa fulani, suala la kuweka orodha ya nini umeuza nini
umepata linakuwa dogo, kwani kufanya hesabu ya bidhaa zote kila siku, au
hata kila wiki, ni usumbufu, wakati kuhesabu fedha iliyoingia kwa siku
hiyo ni kazi rahisi. Suala gumu siyo kuweka vitabu, ila kuuza bidhaa
husika.
Yako maeneo ambako
inahitajiwa kumbukumbu, lakini inategemea biashara yenyewe, kwani mtu
mwenye duka kwa mfano la aina 200 za dawa anahitaji kitabu kujua ni
ngapi huenda zikahitajiwa kununuliwa wiki inayofuata, na zipi bado zipo.
Hahitaji kitabu kujua dawa ipi inatoka zaidi, lakini anaweza kuandika
mahali fulani aina za dawa ambazo kwa wakati wowote wakati anauza,
ataona kuwa sasa inahitaji kufuatiliwa 'shehena' nyingine. Siyo suala la
kuanza kutazama siku ya kwenda 'wholesale' ila picha inayojengeka
taratibu, kwa mfano kwa wiki moja.
Tatizo la kuwepo vitabu
kuyakinisha nini kimeuzwa na fedha kiasi gani iliingia linatokana zaidi
na suala la uwakala, kuwa anayeuza siyo mwenye duka, mgahawa au baa, na
katika hali hiyo 'kucheza rafu' inakuwa ni kawaida. Hata hivyo suala
hilo kwa jumla halitatuliwi na kuweka vitabu, kwani bado ni usumbufu
kuangalia kama kila kitu kiko katika kitabu. Nyenzo muhimu zaidi ni ile
ya matazamio ya mwenendo wa biashara, kuwa mtu anaposema 'leo nimeuza
bidhaa za shilingi laki moja' mwenye duka ajue haraka sababu zake - ni
uzembe, au siku mbaya katika wiki, ubora wa bidhaa fulani, au sababu
yoyote ile. Ikiwa yeye mwenyewe haijui biashara ni wazi atakuwa 'pakacha
likivuja nafuu ya mchukuzi' kwa muuzaji wake.
Ndiyo maana katika
suala la uwakala, yaani nani umweke katika duka, mgahawa au kwingineko
kwa ajili ya mauzo jambo la msingi kabisa siyo kupata kijana au
mfanyakazi unayedhani atakuwa mwaminifu. Waingereza wanasema 'looks is
deceiving,' sura zinadangnya, hivyo hakuna sura ya upole, umakini wa
kusikiliza, n.k. ambao unahakikisha kuwa kijana hiyo au mtu hiyo atakuwa
mwaminifu. Suala ni kuwa watu wanatofautiana kwa udiriki wao, kwani
uhalifu pia ni udiriki, na zipo kanuni za kumwajiri mtu - kwa mfano kuwe
na mtu wa kumtolea ushuhuda wa awali, aliye muhimu kwake, asiyetaka
kumwaibisha. Lakini mwenye duka au mgahawa lazima awe makini; mfanyakazi
akiona unakubali chochote kila 'ataanza.'
CHANZO CHA HABARI : GAZETI LA MAJIRA NA JOHN KIMBUTE ,Jumatatu, Januari , 20 ,2016.
No comments:
Post a Comment