KUANZISHA BIASHARA NI KUCHAGUA LA KUFANYA , SI KUKOMALIA PESA
UTANGULIZI
Kabla ya yote, ni lazima tutafute maana ya dhana hii ya ujasiriamali, kwani kuna mitazamo tofauti.
Sasa hebu tuielekee
taasisi maarufu ya kijamii ya HakiElimu, ambayo kwenye chapisho lake
liitwalo “Elimu ya Ujasiriamali: Kuelekea kwenye Maendeleo Endelevu
Tanzania”, lililoandikwa na Chiraka Muhura linasema:
“2.0. Maana ya Ujasiriamali
Dhana
ya ujasiriamali imeelezwa kwa namna tofauti-tofauti. Baadhi ya watu
hufikiri kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara tu. Baadhi wanauangalia
ujasiriamali katika muktadha mpana unaohusisha ujuzi na maarifa ya mtu
katika kutumia fursa zilizopo. Tranchet na Rienstra, (2009), kwa mfano,
wanaelezea dhana ya ujasiriamali kama uwezo binafsi wa mtu wa
kubadilisha mawazo na kuwa vitendo. Ujasiriamali unajumuisha ubunifu,
kutengeneza kitu kipya na kuwa tayari kukabiliana na ugumu; vilevile
kuwa na uwezo wa kupanga na kuendeleza miradi ili kufikia malengo. Dhana
hii humsaidia mtu katika maisha yake ya kila siku akiwa nyumbani na
katika jamii. Huwafanya waajiriwa kuwa na uelewa kuhusu muktadha wa kazi
zao na kuwa katika nafasi nzuri katika kutumia fursa. Pia ujasiriamali
hutoa msingi kwa wajasiriamali kujenga shughuli za kijamii au
kibiashara. Olomi, (2009) anakubalina na dhana kuwa ujasiriamali kwa
ujumla unaweza kuelezewa kama namna ya kufikiri, kutafakari na kutenda
inayosababisha utengenezaji, uimarishaji, utambuzi na ufanyaji mpya wa
vitu kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu na jamii.
Mwandishi George Jobu
anayeandika kwenye Blogu ya “‘ujasiriamali’ dhana chanya katika
maendeleo”, yenye anuani yake http://gjobu.blogspot,com, anatamka
ifuatavyo:
Zifuatazo ni tabia za ujasiriamali.
Kuthubutu
Hii
ni tabia muhimu kwa mjasiriamali, tukizingatia uwezo na utayairi wa
kuamua kuingia katika biashara fulani au mradi fulani, ukiondoa nidhamu
ya woga. Watu wanaogopa hasara, hawajui jinsi ya kuendesha mradi.
Nidhamu
Hii
ni kanuni muhimu kwa mjasiriamali. Mjasiriamali lazima awe na nidhamu
katika biashara yake, nidhamu katika matumizi ya pesa na nidhamu ya
kufanya kakazi, na nidhamu kwa wateja wake wasimkimbie.
Umakini na Werevu
Wale
waliofanikiwa walikuwa tayari kufanya kazi na waliweka umakini mkubwa
katika kazi waliyokuwa wakiifanya. Mjasiriamali anatakiwa kuwa makini
kwa kila jambo.
Kuwa na uwezo wa Kuongoza
Mjasiriamali
anapaswa kuwa na uwezo wa kuongoza na kuamua. Inadaiwa kwamba uongozi
ni karama ombayo mtu anazaliwa nayo au anapewa na Mungu. Mtu anaweza
kuzaliwa na kipaji cha kuongoza, lakini anaweza kujifunza na akawa
kiongozi mzuri.
Kupenda Kufanya Kazi
Ni
lazima mjasiriamali aipende kazi anayoifanya. Kama unaipenda kazi
unayoifanya, haitakuwa mgumu, utafanya kitu ambacho kwako ni “hobby”, na
utaifanya kwa bidii na maarifa.
Uaminifu na Ukweli
Hii
ni tabia muhimu kwa mjasiriamali. Wateja wanapenda mtu mwaminifu na
mkweli. Mjasiriamali uwe mwaminifu na mkweli upate wateja wengi. Uongo
katika biashara ni sumu.
Dhamira
Mtu
yeyote naweza kujiita mjasiriamali lakini mafanikio yanahitaji uelewa,
kufanya kazi huku ukiwa umeweka mbele lengo au dhamira. Dhamira ya
inahitajika kabla hujaingia katika biashara au mradi.
Kwenda na wakati
Mjasiriamali
lazima aende na wakati aweze kutambua mabadirilo yanayotokea katika
masoko. Mjasiriamali hataachwa nyuma kwa kwenda na wakati katika
ushindani wa kibiashara katika soko huria Pia kunatoa fursa kwa
mjasiriamali kujua njia mpya za uzalishaji, ambazo ni pamoja na kusoma
magazeti, kufanya utafiti na kurambaza katika mitandao mbalimbali.
Tabia ambazo
zimeorodheswa hapo juu ni tabia za ujumla ambazo mjasiriamali anatakiwa
kuwa nazo,lakini kama huna baadhi ya tabia hizo usifadhaike kwani
ujasiriamalia ni somo na sio kipaji.
Kwa mujibu wa Benki ya
Azania, katika kipeperushi chake kinachoitwa “Usishindwe Kuanzisha
Biashara kwa Kukosa Maarifa”, “ili ndoto yako itimie” mjasiriamali
anatakiwa kuzingatia yafuatayo:
1. Nyambulisha na uainishe mradi unaotaka kufanya kwa msingi wa wazo linalotekelezeka
2. Fursa ya biashara hutokana na yafuatayo
a. Tathmini ya wazo lako la biashara.
b. Tathmini ya kina ya mahitaji ya soko ambalo biashara yako italenga.
c. Tathmini ya kina ya bidhaa zako na huduma zako.
d. Tathmini ya kina na jinsi bidhaa yako/huduma yako itakavyokidhi mahitaji ya soko ulilolenga
e. Fikiria na ufafanue walengwa/watumiaji wa bidhaa au huduma zako.
f. Tathimini taratibu za kisheria na kiutawala kuhusu biashara unayotaka kuanzisha.
3. Angalia ushindani uliopo sokoni (husisha yafuatayo)
a. Angalia na uorodheshe biashara nyingine zinazotoa huduma/bidhaa kama unazotaka kutoa wewe.
b. Angalia na ujiulize kama wapo washindani wengine wapya wanaotaka kuingia kwenye biashara hiyo hiyo unayokusudia.
c.
Jiulize changamoto zilizopo na vikwazo vilivyopo (kisheria, kimtaji,
au vinginevyo) vinavyoweza kuzuia biashara nyingine zinazofanana na
biashara yako kuanzishwa.
d. Jiulize na uorodheshe upekee wa
bidhaa/huduma zako (jiulize sababu za kumfanya mtu ahitaji bidhaa/huduma
yako badala ya bidhaa/huduma nyingine zilizopo sokoni)
4. Angalia uwezekano wa biashara yako kuendelea na kukua (ujibu yafuatayo)
a. Utawafikiaje walengwa wa biashara yako (Ni kwa vipi walengwa wako watajua kuhusu bidhaa na huduma zako)?
b.
Utasambazaje/fikishaje bidhaa/huduma zako (Bidhaa zako zitafikaje kwa
wauzaji wa rejareja au huduma zako zitafikaje kwenye maeneo uliyokusudia
na maeneo hayo ni yapi)?
c. Nini makadirio yako ya wafanyakazi
unaohitaji kwa miaka miwili ya kazi (wafanyakazi wangapi utahitaji mwaka
wa kwanza, na wangapi utahitaji mwaka wa pili)?
d. Unahitaji ufanye nini ili biashara yako ipate faida na itachukua muda gani kuwa na faida?
e.
Nini matarajio yako ya mapato na matumizi kwa miaka 4 ya kazi (ni
mapato na matumizi kiasi gani katika mwaka wa kwanza, mwaka wa pili, wa
tatu na wa nne)?
f. Unahitaji mtaji wa kiasi gani (kiasi gani cha
fedha unachohitaji kuwekeza) katika mwaka wa kwanza,wa pili, wa tatu na
wa nne ili kuendesha biashara yako?
g. Utawezaje kupata kiasi
hicho cha mtaji? Je ni kwa kuanza kuweka akiba katika benki au kuomba
mkopo na kwa gharama gani?. Je mchango wako katika mtaji ni kiasi gani?
h. Je mradi wako unaweza ukabeba gharama zinazotakiwa kiundeshaji na bado ukazalisha faida?
5. Uzoefu wako katika ujasiriamali na uwajibikaji.
a.
Tathmini kiwango chako cha elimu na uzoefu wako unaohusiana na wazo
lako la biashara na mahusiano uliyo nayo na wadau muhimu kisekta wewe
kama mjasiriamali.
b. Tathmini kuhusu wataalam wa fani mbalimbali
ambao utahitaji kuwatumia katika maeneo ambayo wewe si mtaalam wala
mzoefu ili kufanikisha uanzishaji na uendeshaji wa biashara yako.
c.
Kwa ufupi tathmini nia/malengo yako ya kutimiliza kuanza na kukua kwa
biashara ukizingatia muda utakaotumia kupanga, muda unaokusudia kutumia
katika mradi, kiwango cha fedha za kwako mwenyewe unachoridhia kuweka
katika mradi n.k.”
Huo ni mtazamo wa kibenki, kwa mujibu wa Benki ya Azania.
HITIMISHO
Msomaji
wa makala haya, hiyo ni mitazamo kutoka vyanzo 4 tofauti. Je, mwandishi
wa makala haya ana mtazamo gani? Maoni ya mwandishi kuhusu ujasiriamali
ni kama ifuatavyo:
Kasumba ya kuamini
kwamba kila kitokacho nje ya nchi – Ulaya, Marekani au Asia – ni bora
kuliko kitengenezwacho hapa nchini ifutwe. Hii ni dhana potofu sana.
Wapo wataalam lukuki, wabunifu wa “kujaza”, hapa nchini; wanadharauliwa
kutokana na kasumba hii. Sasa tuwathamini, tuwatumie ipasavyo, tutaona
neema itakayokuja. Mdharau kwao ni mtumwa!
Mwisho, lazima
utambue – wewe mjasiriamali – kwamba wapo Watanzania wengi wenye KUOGOPA
MAFANIKIO. Wao hawajiamini, wanaogopa mafanikio, kwa hiyo, kila
wamjuaye mwenye dhamira ya kujituma na kuwa mjasiriamali, wanajaribu
kila mbinu kumkatisha tamaa, kwani wanaona kwamba kwa kuwa wao hawawezi
kufanikiwa, basi, hakuna mwingine atakayefanikiwa. Achana kabisa na watu
hawa. Usiwasikilize. Usiwaendekeze. Ujasiriamali unahitaji uwe “mbishi”
katika maamuzi yako. Mtu akikuambia “huwezi”, wewe mwambie “Asante kwa
kunipa moyo! Sasa naamini nitaweza!” Songa mbele, usirudi nyuma!
[Makala haya yamehaririwa na mwandishi kwa kurekebisha makosa ya lugha na kuyafupisha.]
Asanteni kwa kunisoma. Ni mimi mjasiriamali wenu, Paul Francis Mongi,Gazeti la Majira, Jumatatu ,January,20,2014.
No comments:
Post a Comment