Tuesday, April 26, 2016

MTAWANYIKO WA NGUVU KAZI KAMA MSINGI WA KUANZISHA BIASHARA


MOJA ya vielelezo vya kawaida vya biashara ndogondogo mitaani ni hali ya kulazimisha kufanya shughuli fulani na kutazamia kuwa itafanikisha jitihada za kuingiza kipato. Kwa maana hiyo, si kila biashara ambayo inaonekana barabarani inaweza kuitwa kuwa ingefaa kuwa hapo au kuwepo kabisa, lakini utitiri huo wa biashara ni msingi mmojawapo muhimu wa jinsi biasbara zinavyoanza na kukua. Mara nyingi kuna chembe ya kubahatisha, ingawa yapo maeneo ambako ni wazi hapakuwa na wazo thabiti la biashara kuanzia mwanzo, hivyo haisimami kabisa.

Hali hiyo ni mojawapo kati ya vielelezo vya tofauti ya mtu anayefanya biashara na anayejaribu kukwepa ajira, labda kwa sababu itakuwa ya sulubu au imeshindikana kupata ajira kama hiyo. Moja ya vianzio vya ajira ni kuaminiana, hivyo mtu asiye na mdhamini wa aina moja au nyingine pale anapotafuta kukubalika katika aina moja au nyingine ya shughuli, inabidi 'ajiajiri mwenyewe' kwa kuanzisha shughuli yake. Ndiyo hapo linakuja tatizo, kama mtu hiyo ana moyo wa biashara au ni wa kutumwa, na ikiwa katika biashara hiyo atakuwa na moyo wa kutumwa, itakwama.

`Ipo tofauti kati ya moyo wa biashara na moyo wa kutumwa, kuwa katika biashara mtumishi wa kwanza ni yule mwenye biashara, kuwa anatakiwa ajali kila kitu na kuangalia kila kitu kiwe salama, wakati moyo wa kutumwa ni kinyume chake. Mtu anayetumwa hufanya yale yanayomgusa, anayowajibika nayo au kuulizwa, na hayo mengine yahamhusu, yakae vyema au vinginevyo suala hilo halimhusu. Hisia ya namna hiyo inafikia tamati ya kutokuwa na moyo wowote kuhusu shughuli nzima inayoendelea, nje ya kisehemu kidogo ambacho mtu anakabidhiwa, ndicho anajali.

Kwa maana hiyo mtu ambaye amezoea kuajiriwa na ana hulka ya mwajiriwa katika eneo la kazi, hajishughulishi na chochote kile ambacho hakimgusi moja kwa moja, hawezi kuanzisha biashara ikasimama. Mtu kama huyo anazoea lawama badala ya kuchangia, anakwepa majukumu badala ya kusaidia kuboresha, na si ajabu hata akawa na furaha pale mtu mwingine akikosea jambo fulani, kwani kwa hali hiyo aonekane bora zaidi kuliko huyo mwingine. Akiinua biashara, atabadili roho yake?
Hulka ambazo mtu anakuwa nazo kwa vipindi virefu vya maisha baada ya kuingia ujana na hasa kuanza kupata fedha haziwezi kubadilika ghafla kutokana na 'mahitaji' kubadilika. Hivyo uzoefu au historia ya biashara ni kupanda na kushuka au kuanguka kwa biashara hasa kutokana na hulka za watu wanaozianzisha, pale hisia zao na mwenendo wao unapokuwa kikwazo katika biashara yenyewe. Ni tatizo ambalo kwa kiasi fulani lipo hata katika biashara zilizofaulu, kuwa kuna wakati anatokea mtu aajiriwe kama meneja halafu mambo yaende vizuri, baadaye aje mwingine, iporomoke. Katika biashara ndogo, ni biashara yenyewe inayokufa.

Ndiyo maana idadi kubwa ya biashara zinaandikishwa na hata kuanza, lakini nyingi zinadidimia baada ya muda si mrefu, kwani walioanzisha hawalingani kisaikolojia na shughuli wanayoianzisha. Ni hali inayoonekana katika nyanja zote za jamii, na mara nyingine utasikia mtu akieleza jinsi alivyohangaika hadi kipindi fulani akaanza biashara inayoendana na hisia zake, inayomfaa, au kupata kazi ambayo anaendana nayo. Akiondolewa katika nafasi hiyo, hasa kama bado ni kijana anayeangalia zaidi haiba yake (nafasi yake kijamii), anaweza kuporomoka.

Ndiyo maana ukiona biashara imesimama mahali fulani, usikimbilie kudhania kuwa mradi imesheheni basi imefaulu, ila kutambua kuwa kuna 'moyo unadunda,' au kwa lugha ya kitaaluma ni 'half life,' kuwa kitu kinachipuka, kichanue halafu kififie, labda kama kitaota mizizi, kiwe endelevu. Ukitafakari ni biashara ngapi unazoona ambazo zimechanua tu na hazina mizizi, na badala ya kuwa endelevu huenda ziko mbioni kunyauka, utashangaa, na siyo rahisi kusema kuwa huyu alikosea hiki au kile. Masuala mengine ni ya kimazingira, kwa mfano ni wapi mtu aweke biashara yake, achuuze bidhaa gani au atengeneze nini, kila kitu hutegemea kingine; biashara inakuwa ni kama wazo linachipuka, liinuke au ligonge mwamba.

CHANZO  CHA  HABARI:GAZETI  LA  MAJIRA,NA  JOHN  KIMBUTE, Jumatatu , Januari  20 , 2014.

No comments:

Post a Comment