YAKO maeneo mengi
katika maisha ambako lugha ya kawaida inasaidia kuelewa kiini cha
mahusiano muhimu ya maeneo tofauti, bila kuwa na utaalamu wowote kuhusu
jambo hilo, ila kwa kuwaangalia watu tofauti katika shughuli hizo. Uwezo
wa kufanya kazi kwa ufanisi, ambao pia ni chembe ya msingi ya
kufanikisha shughuli ya kibiashara, unaelezeka kwa kanuni ya aina hiyo,
kuwa watu wana uwezo wa kutofautisha nini hasa kinafanya mtu apate
mafanikio, au tuseme amudu shughuli fulani. Kuna chembe ya hisia katika
hali hiyo, ila huwa inaashiria ukweli.
Licha ya kuwa taaluma
za kisasa zinalenga zaidi kufanyika utafiti wakilishi ili kujua
mahusiano kati ya maeneo tofauti ya maisha au shughuli zinazoendana
katika mantiki yake, bado nafasi ya kung'amua tu kwa kutazama haiwezi
kutupwa. Ikiondolewa, sehemu kubwa ya mazungumzo ya kawaida itakwama,
pale ambapo takriban kila kitu kinachozungumzwa inabidi kutanguliwe na
aina fulani ya utafiti au upelelezi kubakikisha kuwa ni hivyo msemaji
anavyodhani, na atakayesikia hilo hawezi kujibu hadi ahakikishe utafiti
wa msemaji kuwa ni sahihi. Ingekuwa taabu.
Moja ya maeneo ambako
uwezo wa kung'amua mahusiano halisi yakoje ni katika kufanikisha
biashara, au kumudu kitu ambacho kwa jumla ni kipya, na ambacho
kinategemea uwezo wa huyo anayekishika, siyo msimamizi wala mwenye mali
mwingine. Ni kwa njia gani ambako kipaji alicho nacho mtu kinatangulia,
au ni juhudi zale licha ya kuwepo kipaji cha juu au cha kati, au labda
ni kujifunza na kuelewa nini cha kufanya kwa muda mfupi kuliko mwingine?
Je maeneo haya matatu ni tofauti kabisa au ni jambo moja ambalo
linajieleza tu kwa sura tofauti?
Njia nyingine ya
kufafanua suala hilo ni kulibadilisha katika mafungu, kama chembe hizo
zinaenda pamoja, kwa mfano kama kila mwenye kipaji ana juhudi, au huenda
hana juhudi ila afaulu kwa kipaji chake. Pia unaweza kuuliza kama kila
mwenye kipaji hujifunza haraka, au labda aliye na kipaji anaelewa kwa
kuangalia tu na hahitaji kujifunza, kwani 'inaandikika' kichwani akiona
tu nini kinatendeka. Ni kwa njia hiyo pia unaweza kuuliza kama mwenye
juhudi anajifunza haraka, au juhudi inajazia pale ambako yako mambo
hayaelewi vyema ila anazingatia kanuni.
Ni wazi katika mpangilio huo
wa kutoa na kujumlisha kuwa kipaji kina uwezo zaidi wa kusimama peke
yake bila juhudi halisi kuwepo, ambayo haina maana kuwa mwenye kipaji
hahitaji kufanya juhudi. Maana yake ni kuwa kipaji ndicho hasa nyenzo ya
msingi ya kila jambo, kinachomfanya mtu awe 'anafaa' katika eneo fulani
kwani silika zake na hisia zake zinaendana na jambo hilo. Ikiwa kuna
upungufu wa wazi wa kipaji, suala la kujazia kwa juhudi linakuwa tatizo,
na pa haiwezekani kuongeza uwezo wa kujifunza kama kipaji kimepungua
sana, ila kuna uwezekano wa kuongezea uwezo wa kipaji pale elimu
inapokuwa imeongezeka.
Cha kushangaza, au
labda cha kujiuliza, ni jinsi gani watu wanaangaliwa katika maeneo ya
kazi, na hapa inakuwa ni tatizo kama chanzo na matokeo ni kitu kile kile
au ni tofauti.. Kwa mfano mtu anayesifiwa katika jambo fulani mara
nyingi zaidi anasifiwa kwa kipaji chake, uwezo mahiri wa kufanya jambo,
na siyo kiasi alichojifunza, au bidii anayoweka katika jambo hilo. Ila
anapolaumiwa au tuseme kukosolewa katika kile anachokifanya, ni nadra
kuona fikra ya anayemtazama iwe imeelekea katika kipaji chake, ila
laweama zitalenga juhudi zake, uvivu, kutosikia.
Hapo ndipo linapokuja
tatizo la uhusiano wa mantiki ya kawaida ya mazungumzo na hali halisi ya
kitu, na kama mantiki ya kawaida inarahisisha tu kuelewana tunavyohisi
kuhusu jambo fulani, kukiwa kuna upana tu wa 'makosa' katika kile
tunachoona kwa kukitazama kwa macho, au tunakaribia ukweli. Unachoweza
kuyanikinisha ni kuwa mantiki ya kawaida inatoa elimu maridhawa kuhusu
jambo fulani, lakini siyo lazima ipatie kwa usahihi halisi wa kimantiki.
Kuna viwango tofauti za 'kuachana' kwa mazungumzo na ukweli, ambavyo
vinafanana na tatizo hili la kipaji, juhudi na kujifunza - kipaji cha
mzungumzaji, ikiwa ni mkweli, n.k.
Suala la kipaji mara
nyingi halianzii tu katika uwezo wa kuelewa cha kufanya kwa haraka ila
pia kuchangamkia jambo hilo, kuwa na mwito nalo, ambao mara nyingi
huendana na kipaji cha jambo hilo. Ndiyo maana biashara mara inatakiwa
iwe ni kitu mtu anafanya kwa kuwa kinamfurahisha kukifanya, na siyo kwa
shurti la njaa au umaskini, kwani katika hali hiyo shughuli ile itakuwa
mzigo kwake. Kipaji cha kwanza ni kukipenda kitu kinachohusika ambacho
kinafungua milango ya juhudi ya kujituma na kuelewa pale anapojifunza
zaidi. Ni wazi asiye na juhudi halisi ana walakini wa msingi wa
kutopenda anachokifanya; asiyeelewa vile vile hakipendi.
CHANZO CHA HABARI: GAZETI LA MAJIRA NA JOHN KIMBUTE ,Jumatatu, Januari ,20,2014.
No comments:
Post a Comment