Monday, April 25, 2016

UJASIRIAMALI--- KUANZA SHUGHULI NA KURASIMISHA BIASHARA .


Aina mbili za biashara kwa kawaida zinaonekana mitaani, hata zingekuwa ni zile kubwa kubwa, aina ya kwanza ikiwa ni biashara zenye mmiliki halisi, na kama kuna uhusiano basi upo katika ngazi ya familia, na zile zinazoanzishwa na watu wawili tofauti. Pale ambapo kuna uhusiano wa kifamilia au kinyumba uhusiano huo sio ushirika kisheria, kwani, kwa haraka, mshirika wa biashara ni mtu ambaye anaweza kusimama mahakamani kutoa ushahidi dhidi yako, hivyo hawezi kuwa mwenza kinyumba au mwana, mjomba, n.k. Ushirika ni wa watu tofauti kijamii.

Kuna aina mbili sa sababu ambazo zinaweza kutajwa kuhusu kutafuta au kukubali kuwa na mshirika katika biashara; zote mbili kimsingi zinakuwa ni kutegemeana. Moja ya sababu ni kuwa wale wanaoanzisha biashara wanakusanya raslimali zao kwa pamoja, kwa mfano kama watu wawili wanakopa SACCOS kupata mtaji wa kutosha kuanzisha biashara, hivyo wanakuwa washirika kwa misingi ya kiwango cha hisa walichonacho kila mmoja katika kampuni. Kwa jumla kuhitajiana kupata msingi wa kutosha ndiyo msingi wa ushirika kwani mahusiano ya kitaaluma au kuweza kufanya kazi kama timu ina chembe ya ajira ndani yake, usipokuwepo mchango wa mtaji - hivyo bila mhusika wa pili kuchangia, biashara isingekuwepo.

Jinsi kila mtu alivyochangia kuinua biashara fulani kwa kawaida inatoa milingano yao ki-hisa, na kama ni kampuni kubwa, mahusiano ya kupiga kura yanapohitajika maamuzi kuhusu uendeshaji wake, nje ya mgao wa faida au viwango vyua gawio. Hata hivyo huko ni mbali an swali la awali la uhitaji, au ulazima wa mtu kuwa na mshirika kibiashara, ambako tatizo la msingi ni kama hilo ni jambo jema. Hivi mtu anatakiwa atafute mtaji wa kwake mwenyewe ajitahidi kusimama wima, au atafute mshirika kujazia viwango vya mtaji vitosheleze, na kusaidiana kiutawala?

Hata pale ambako suala siyo hasa la kuanzisha biashara au kampuni ila kujaribu kuzuia isianguke, masuala hayo huwa yanajirudia, kama mtu atafute mshirika kusaidia kampuni isianguke, au atafute majawabu  yake mwenyewe. Hakuna majawabu ya moja kwa moja yanayoweza kutolewa 'darasani,' kwani suala zima la kupata mshirika liko nje ya vitu vinavyotawaliwa kihesabu. Ni suala la utashi, ari.
Moja ya sababu ambazo watu wanaunda ushirika ni kuwa wanakuwa ni marafiki wakubwa, na hawatazamii kuwa mmojawapo anaweza 'kumsaliti' mwingine siku moja, kwa hujuma ya aina moja au nyingine. Hisia hiyo ni chanzo cha masikikitiko mengi , kuwa "sikudhani angeweza kunifanyia hivi,' baada ya undani wa mtu kuanza kuonekana pale kampuni inapokuwa na nguvu, mtu akajisikia ana sauti, hadhi.  Ndivyo inavyotokea pia katika mahusiano ya kinyumba, kuwa yanaanza kunyauka; ikishapita mpaka fulani unaotofautiana kati ya wanandoa, akili huruka.

Ni kwa kiasi gani ushirika katika biashara unatawaliwa na huzuni kama hizo siyo rahisi kusema, kwani watu wengi huwa wanaficha huzuni zao na hasa kama mahusiano au ushirikiano huo bado unaendelea. Hata hivyo, biashara ambayo inetawaliwa na huzuni, kama ulivyo unyumba, haiwezi kuendelea, kwani ni hulka ya msingi ya binadamu kutafuta uhuru pale anapohisi anakandamizwa, ana anakosa pumzi. Biashara nyingi ambazo hazikusimamishwa na kuendeshwa kwa misingi ya ufanisi katika soko zina mazingira kama hayo ya huzuni, vijicho, visa, watu wakipigania maslahi ndani ya shirika; mara nyingi hujitokteza kama rushwa.

Hivyo hakuna majawabu rahisi kuhusu kuhitaji mshirika ili kuanzisha biashara. kwani viwango vya mtaji ambavyo mtu anahitaji ili biashara ianze inatoa mwanya wa kupangilia ndani ya viwango vya ngazi kadhaa tofauti.  Ambacho ni kigumu zaidi ni kubainisha ni mtu wa aina gani anaweza kuwa mshirika mzuri, na kwa hili inabidi kukumbushia tu alichosema mwalimu wa jadi wa fikra ya soko huria, Adam Smith, kuwa upo 'mkono wa neema usioonekana' ambao unaongoza juhudi kama hiyo.  Huwezi kuondoka nyumbani uanze kukagua unakopita kama kuna mtu anayefaa kuanza naye biashara, au kuwa mwenza kinyumba. Ni kukutana tu.

CHANZO  CHA  HABARI: GAZETI  LA  MAJIRA  NA  JOHN  KIMBUTE.  Jumatatu , Januari  20, 2014.

No comments:

Post a Comment