UJASIRIAMALI : NI UJASIRI , AU NI KUBAHATISHA ?
KATIKA miaka
iliyofuatia Azimio la Arusha, kulikuwa na hekaheka nyingi za kukuza
Kiswahili, na mojawapo ilikuwa ni kutayarisha msamiati wa masomo ya
sayansi, na kwa upande fulani biashara. Lengo lilikuwa ni kutumika kwa
msamiati huo katika kufundisha masomo ambayo yana vitabu vya
kufundishia au vya kitaaluma vya Kiingereza, ikidhaniwa kuwa
vikiandikwa kwa Kiswahili masomo hayo yataelewka zaidi. Hivyo ilianza
shughuli ya kujenga misamiati katika maeneo mengi na mengi kati ya
maneno yanayotumika sasa yalianza kubuniwa wakati huo.
Hali hiyo haikuondoa
hali ya awali kuwa uanzishaji wa maneno mara nyingi unatokana na kudra
tu katika mazungumzo na hasa katika uandishi wa riwaya au mashairi,
ikatokea kuwa mtu aingize neno jpya. Kwa mfano Mwalimu alileta neno
kung'atuka akisema kuwa ni neno la Kizanaki ambalo alilitumia kana
kwamba ni Kiswahili, na likabaki hapo. Kuna uwezekano kuwa watungaji wa
maneno katika mabaraza rasmi kama BAKITA au TUKI pale Mlimani, au
wazungumzaji wengine wenye hadhi hii au ile, watakuwa wameingiza neno
ujasiriamali katika msamiati.
Kinachoonekana katika
neno hilo ni dhana ya ujasiri, ambayo inaanza kwa kuleta mashaka,
kutafuta hasa ujasiri wenyewe uko wapi, kwani maana ya kawaida ya neno
ujasiri ni kuthubutu kuingia au kufanya shughuli hatarishi, kutokana na
malengo fulani ambayo ni muhimu. Neno ujasiri vile vile linahitaji
shughuli hiyo iwe njema kijamii, hivyo ikiwa hatari yoyote itatokea au
kutumia, mtu kama hiyo anaitwa shujaa, kwa mfano askari anapokufa
vitani. Pale ambapo mtu anafanya shughuli hatarishi isiyo na manufaa kwa
jamii, kwa mfano ujambazi, haitwi jasiri.
Kwa maana hiyo
aliyetunga neno hilo alikuwa na maana ya kujipongeza kama alikuwa
akijizungumzia, au kuwapongeza watu fulani kama alikuwa anawataja kwa
maana ya kuthubutu, kudiriki, kujitoa (na siyo kujitoa mhanga, hasha).
Kuna undani wa ujasiri unaozungumziwa na pia mpaka wa wazi, kuwa licha
ya kuwa anayezungumza anatambua ujasiri huo, asingependa kutia chumvi.
Ukivusha dhana hiyo ya ujasiri ikawa ya kina sana, inaanza kupoteza
maana, iwe kichekesho.
Hivyo mjasiriamali ni jasiri kidogo tu, hawezi
kuitwa shujaa kwani hatazamiwi kufa katika kutafuta mali kwani hakuna
anakufa akiuza vitu, labda kama kuna uhalifu, ambao si ujasiri kijamii.
Lakini ukifika katika magereza au kuwasikia watu ambao ndugu zao au
majirani zao wana mtu aliyewahi kufungwa akatoka jela akaelezea
wanayoongea huko, ni wazi mantiki yao ni tofauti na jamii, kwani kwao
ujambazi ni "kutafuta maisha,' yaani ujasiriamali. Ni sawa na rushwa
miongoni mwa polisi au 'ufisadi' serikalini, ubadhirifu ni 'kutafuta
maisha,' tuite ujasiriamali.
Hata hivyo kinachosemwa
ambacho kwa bahati mbaya kinauganisha jambazi na mchuuzi au mwanzishaji
wa shughuli yoyote ile, ni udiriki wa jambo fulani, yaani kuacha kile
unachofanya kila siku, chenye uhakika, uthubutu kuanza kitu kingine.
Ujasiri uko katika ufahamu kuwa hakuna biashara inayoanzishwa na uhakika
wa mia kwa mia ya kufaulu, na hivyo kuna majonzi tarajiwa au
yanayowezekana pale mtu anapoanza shughuli ya biashara. Dhana ya
ujasiriamali inasaidia kumpa mtu motisha ya kujituma, kumpa daraja ya
wadiriki, na si wabahatishaji, wabangaizaji.
Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ambao miaka kuanzia ya tisini wanaendesha shughuli za pamoja kwa
Kiswahili badala ya ile jadi ya Kiingereza walianza kutumia neno
'wabangaizaji' kuzungumzia tabaka la 'wavuja jasho' badala ya neno la
Mchungaji Christopher Mtikila, 'walala hoi.' Wakati siyo kila 'mvuja
jasho' ni mbangaizaji, kwani anaweza kuwa na kipato cha uhakika wakati
mbangaizaji hana uhakika wa kipato - kwani anangoja atumwe, aitwe,
ahitajiwe, au achuuze kwa bahati, ujasiriamali ni tofauti. Hauelekezi
hisia katika jasho, na unakwepa na hata kupinga 'ubangaizaji' ambao una
maana mtu hajui anachokifanya, hubahatisha tu.
Ujasiriamali una kiini
cha ujasiri wake na ubunifu wake katika kugundua mahitaji ya soko, kuwa
kina kitu kinachotakiwa, siyo kwa vile hakipo ila kinahitajiwa kwa wingi
zaidi au kwa namna tofauti. Ndiyo maana ujasiriamali unajiumiza kwa
kiini kile kile kinachouwezesha kuwa na umuhimu, yaani kutokuweza kuona
tofauti kati ya kudiriki kushiriki katika shughuli fulani, na kujazana
tu katika shughuli hiyo. Watu wanapojazana siyo lazima baadhi wakose
riziki, lakini ushindani unakuwa mgumu na baadhi itabidi wapangue
waondoke. Mtu anapofaulu kukaa katika eneo alilochagua na kujihakikishia
riziki anakuwa mjasiriamali aliyefaulu; akishindwa anakuwa mbangaizaji
(hata ingekuwa biashara ya mamilioni) hadi afaulu. Siri ya ujasiriamali
ni kuwezesha biashara kuwa endelevu; ujasiri unapatikana kama kofia au
pete pale mtu anapokuwa amefaulu, ndipo atambuliwe. Kabla ya hapo huwa
anajitambua peke yake au aonekane akijaribu, hata akidhaniwa ni
mbangaizaji tu.
CHANZO CHA HABARI: GAZETI LA MAJIRA NA JOHN KIMBUTE ,Jumatatu, Januari , 20 2014,
No comments:
Post a Comment