Saturday, April 23, 2016

MIEZI MITATU KABLA SIMU BANDIA KUZIMWA , WATEJA WAHAHA KUZIBADILI




DESEMBA 18, mwaka jana Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza kuzifunga simu zote zitakazobainika kuwa bandia baada ya miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu, yaani Januari Hadi Juni.
Kwa maana hiyo imebaki takribani miezi mitatu kutoka hivi sasa ili kuifikia Juni ambapo Mamlaka hiyo itazizima simu zote bandia na wamiliki wake hawataweza kupata mawasiliano.
Ukweli ni kwamba dunia ya sasa ni ya mawasiliano na kila mmoja  anapenda kuwa ‘hewani’ akiwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki zake kila wakati.
Ndio maana matumizi ya simu za mkononi yamekua kwa kasi katika miaka ya karibuni duniani.
Mussa Mwaikyusa, mkazi wa Dar es Salaam, anasema alilazimika kununua simu ya mkononi  ili imsaidie kurahisisha mipango yake ya kibiashara.
“Mimi naishi hapa Dar es Salaam lakini natokea mkoani Mbeya huku nimekuja kwa lengo la kufanya biashara na familia yangu ipo mkoani Mbeya, huwa nachukua mizigo kule na kuja kuiuza huku hasa ndizi na viazi.
“Mara nyingi huwa natumia simu yangu ya mkononi kuwasiliana na familia yangu pamoja na kuwajulisha waniandalie mzigo mwingine pale ninapokaribia kumaliza ule nilionao,” anasema.
Mwaikyusa anasema alinunua simu yake hiyo aina ya Samsung katika duka moja hapa jijini Dar es Salaam kwa Sh 80,000.
“Ina mawasiliano vizuri lakini nimesikia habari kwamba TCRA itazizima itakapofika Juni na nimejaribu kuuliza kama walivyosema kujua kama ni halisi au bandia nikagundua kwamba ni bandia,” anasema kwa masikitiko Mwaikyusa.
Mwaikyusa hivi sasa yupo katika harakati za kununua simu nyingine mpya na anasisitiza kwamba kabla hata hajaondoka katika duka atakalonunulia ataingiza namba zilizotolewa na TCRA ili ajue kama na yenyewe ni halisi au la.
Mary Kazaula anasema aliwahi kununua simu kwa Sh 20,000 katika duka moja huko Kariakoo ambapo alipatiwa muda wa kuichunguza wa wiki mbili.
“Miaka mitatu iliyopita niliinunua na kwenda zangu nyumbani kabla hata wiki mbili hazijaisha nilishangaa imezima ghafla ikabidi niirudishe lakini hawakukubali kuipokea, nilisikitika kwamba nimepoteza Sh 20,000 yangu nikalazimika kwenda kununua nyingine ambayo nimedumu nayo hadi sasa na nimeingiza hizo namba za TCRA imeniambia kuwa ni halisi,” anasema.
Ukweli ni kwamba soko la Kariakoo ndilo eneo maarufu ambako wafanyabiashara wengi wanauza simu za kila aina kwa bei mbalimbali.
Na kwa miaka mingi wafanyabiashara hao wamekuwa wakiuza simu hizo ambazo  zinafanana na simu halisi na za aina tofauti bila kujali suala la ubora wa vifaa hivyo.
Kutokana na bidhaa feki kuwa zinakwepa kodi Tanzania imekuwa inapoteza kiasi kikubwa cha mapato kutoka kwenye mauzo na hata kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na halikadhalika ushuru mwingine pamoja na tozo nyingine za serikali.
Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, simu  feki zilizojaa kwenye soko lisilo rasmi zinaunda takribani asilimia kumi ya mauzo duniani kote na kiwango hicho kinaweza kuongezeka. Simu feki zina madhara kwa watumiaji  na hata wapendwa wao.
Halikadhalika madhara mengine ni pamoja na uharibifu wa mtandao pamoja na kumiliki bidhaa zilizo duni.

 Tigo yapewa jukumu la kuhamasisha
Ili kuhakikisha kwamba elimu hiyo inafika vyema kwa jamii  TCRA  imeamua kuipa jukumu hilo kampuni ya simu za mkononi ya mtandao wa maisha ya kidigitali Tigo.
Akizungumzia hatua ya Tigo kutoa tahadhari kwa wateja wake Mkuu wa Idara ya Vifaa vya simu  wa kampuni hiyo, David Zakaria anawatahadharisha wateja kuhusu muundo na alama za biashara za bidhaa halisi zinazotumika  kulaghai wateja kabla ya kununua.
“Ili mteja aweze kuelewa iwapo simu zao ni feki  au ni halisi anatakiwa kupiga namba *#06# ambapo  atapokea  namba ya Utambulisho wa Kimataifa wa Vifaa vya Simu  (IMEI) ambapo pia inaweza kupelekwa kama ujumbe mfupi wa maneno (meseji) kwa namba 15090 ilikupata jibu kama  simu hiyo ya mkononi ni halisi au nifeki,” anasema Zakaria.
Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa Umma wa TCRA, Innocent Mungy kuchukuliwa kwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano na Posta  ambayo inaiwezesha Mamlaka kusimamia mawasiliano ya simu nchini na shughuli zinazohusiana ili kudhibiti uhalifu wakupangwa ambapo simu za mkononi zimekuwa zinaibwa na kuingizwa nchini.
“Kwa miaka minne sisi wenyewe tumekuwa tunajipanga pamoja na kampuni za simu zilizopo nchini ili kutekeleza jambo hili. Hitaji la kuzifunga simu feki linakwenda mbali zaidi ya  hitaji la nchi la kuondokana na bidhaa feki na kutokomeza  uhalifu wa kupangwa. Badala yake  unalenga kwenye afya na ubora na kutapakaa kwa bidhaa hizo,” anasema.
Anasema utambulisho IMEI una maanisha kuwa kila simu ya mkononi ina namba ya kipeke ya kuitambulisha hivyo kwamba endapo simu inaelezwa kuwa ni feki au imeibwa, namba hiyo IMEI itapelekwa kwenye Rajisi Kuu ya Utambulisho wa Vifaa (CEIR) ambayo ina wajibika kuifanya kifaa husika kisitumike kwenye  mtandao wowote duniani.
“Baadhi ya simu hizi za mkononi ambazo ni bandia hazijakidhi viwango vya mionzi vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Halikadhalika kuwepo kwa namba ya kipekee ya IMEI kuna mwezesha mteja  kuizuia simu yake iliyopotea kitendo ambacho kinazuia matumizi yake sehemu yoyote duniani,” anasema.
Anasema TCRA imefunga CIER ambayo itahakikisha, mbali na  kudhibiti  kupenyezwa kwa simu bandia, simu zilizoibwa zinaweza kufungwa na hazitaweza kutumiwa  tena.
Mungy anafafanua CEIR ni Rajisi Kuu ya Utambulisho wa vifaa ambayo  huhifadhiwa kwa ajili ya Utambulisho wa Kimataifa wa Vifaa vya simu (IMEI) na namba za simu zote zilizofungiwa ndani ya nchi.
“Pindi simu  ya mkononi inapoelezwa kuwa ni bandia au imeibwa namba ya rajisi yaani IMEI inaenda moja kwa moja CEIR na mara moja  simu hufungwa au kifaa hicho kuzuiwa kutumika tena duniani kote. Hivyo basi kifaa  kinapotambulika kama ni bandia au kimeibwa namba inayotambuliwa kimataifa hukizima,” anasema Mungy.
Anasema mwaka  2012 takribani wananchi wa Kenya  milioni 1.5 waliathirika kutokana na zoezi la  kuzifungia simu bandia  lililoendeshwa na Tume ya Mawasiliano ya Kenya (CCK) katika kuzitokomeza.
“Kwa maana hiyo Watanzania wanatakiwa kuchukua hatua za haraka ili kuachana na simu zao feki kabla ya siku hiyo haijafika,” anatoa wito.

CHANZO  CHA  HABARI :  GAZETI   LA   MTANZANIA.Na  VERONICA  ROMWALD , DAR   ES  SALAAM.  Jumanne , machi  15 ,2016.

No comments:

Post a Comment