Tuesday, April 26, 2016

MIPAKA YA HITAJI LA MAFUNZO KATIKA BIASHARA


MOJA ya maeneo magumu kimaudhui kuhusu biashara ni kile kinachoitwa mbinu za biashara, kama ni sawa na yale yanayofundishwa darasani au huweza kuwa sehemu ya mafunzo ya biashara, au ni ujanja ambao kila mtu anabuni kivyake. Kujaribu kupekua vitabu kuangalia wataalamu wanasema nini haisaidii sana, kwani kimsingi vitabu vinaeleza jinsi biashara ilivyo, yaani inavyofanya bila kujali kama anayefanya biashara anajua hivyo au la. Ni kama suala la kawaida la kutafuta mchumba, kuwa ni haba kusikia mtu anapelekwa shule au darasani kufundishwa.
 

Kwa kawaida mtu anaanza biashara kwa vile ameona mtu fulani akifanya hivyo, na anahisi kuwa huduma au bidhaa hiyo inahitajiwa katika eneo fulani, naye anamudu kwa kiwango fulani kuingia katika biashara hivyo. Kwa maana hiyo biashara hasa ni kujua bidhaa au huduma inayohitajiwa eneo hilo, na kuwa tayari kutumika kwa jambo hilo, na mengineyo ni mazingira binafsi ya kuweza kufanya hivyo, kwa mfano kupata mtaji, na katika mazingira kadhaa ya jamii, hata kuruhusiwa kufanya hivyo. Hiyo inagusa biashara za kina mama; akiolewa, siyo rahisi kujishughulisha.

 

Kuna tayari daraja la kisaikolojia ambalo linavukwa kabla ya suala lenyewe la kuanzisha biashara kuanza, nayo ni ule utayari wa kuingia katika hali hiyo, yaani kutumika. Pale kwa mfano mwanamke anapokuwa mama wa nyumbani mwenye mwenza anayehakikisha kila kitu kipo, staha kwa upande wake itakuwa ni kuweka nyumba katika mazingira mazuri yanayopendeza kwa wageni wakifika, ili mwenza ajisikie kuwa yuko mahali panapofaa. Mara nyingi suala la biashara linaendana na hitaji halisi kimaisha, au kwa wale walioenda shule, kwa vile hawawezi tu kukaa.

 

Tayari hapo kuna tofauti ya mtazamo, kuwa mtu anayehitaji kufanya biashara kutokana na hitaji halisi la maisha, kwa mfano hata fedha ya kulipa pango kila wakati, atakuwa katika hali tofauti ya kisaikolojia na yule anayehitaji tu kuongeza kipato. Suala la mafunzo katika biashara hasa linakuja kwa hawa ambao nia yao ni kuongeza vipato, kwa maana kuwa watahitaji biashara zenye mazingira bora zaidi kuliko ya 'wabangaizaji.' Hapo ni rahisi zaidi kuharibu mtaji ambao ni mkubwa.'

Mafunzo, kama ilivyo elimu ya darasani kwa jumla, si kitu ambacho kinatumika kwa upana wake, kuwa hili amefundishwa analifahamu, na kadhalika, ila kwa ufinyu wake, kuwa liko jambo ambalo anayefundishwa atakumbuka, hasa kama atakutana na suala kama hilo baada ya masomo. Kwa maana hiyo lengo halisi la kuwepo mafunzo ya biashara ni kutoa dokezo la maeneo mengi, na hata kujua 'visa' vilivyowahi kutokea kuhusu chembe moja au nyingine ya uendeshaji wa biashara. Kwa mtu mpya katika eneo hilo anajifunza mengi; mzoefu anathibitisha tu kile ambacho anakijua, au ashangae kuna suala alikuwa halifahamu, alaitambue. 

Mfikiriaji wa Ujerumani wa karne ya 19, Karl Marx ni kama alitatua suala hilo kwa msemo uliovuma katika nyanja za fikra ya sayansi, licha ya kuwa labda hakuwa wa kwanza kugundua hilo lakini akalivumisha. Alisema "hitaji moja katika viwanda linatoa msukumo mkubwa zaidi kwa sayansi kuliko vyuo vikuu kumi," yaani, ambavyo vinafanya tu utafiti, wa kubuni na hata kutunga matatizo. Pale mtu anapojaribu kutatua tatizo halisi katika biashara, akafaulu, siyo tu kuwa anawezesha biashara yake kuendelea, lakini anatoa mchango hata katika fikra ya kuendesha biashara kama hiyo, kwa mfano pale akitokea mtu afuatilie alichofanya. 

Hiyo ina maana kuwa yapo maendeleo yanayopatikana kila siku katika uendeshaji wa biashara bila kuwepo darasa lolote kwa wale wanaofanya shughuli hizo, yaani kutatua matatizo halisi ya uendeshaji wa biashara kwa kukutana nayo, si kusoma kuhusu matatizo hayo. Kuna msemo unaotumiwa na mwanzilishi wa kampuni ya habari na vitabu ya Global Publishers ambao unafupishwa kama Street University - chuo kikuu cha barabarani. Kujifunza mbinu za biashara wakati wa kuifanya, kwa kutatua matatizo, ni moja ya vielelezo vya Street University, kufaulu mtihani wa maisha kwani biashara ni maisha. Inaweza kuharibu utulivu wa mtu anapokwama.

CHANZO  CHA  HABARI :GAZETI  LA  MAJIRA  NA  JOHN  KIMBUTE, Jumatatu,Januari ,20, 2014.

No comments:

Post a Comment