Wednesday, April 27, 2016

CHANJO KWA KINGA


Jitihada zimekuwa zikifanywa na binadamu kote duniani tangu zamani ili kumwepusha na kuathiriwa na vinavyoweza kuzorotesha afya yake. Katika utaalamu wa kileo, chanjo za dawa hutumiwa kwa kuzidunga mwilini (vaccination) ili kuamsha chembe za kinga za kimaumbile zizaliane kwa wingi kuuhami mwili dhidi ya viini vya magonjwa, sumu na kadhalika, kwa mwenendo wa kimaumbile (natural) au kutokana na jitihada za mwili wenyewe. 
 Mbali na kinga (immunization) dhidi ya ndui (small pox), kidonda cha kooni (diphtheria) na homa ya vipele vyekundu (scarlet fever), tunaweza kuwa na kinga (immune) ya pepopunda (lockjaw), homa ya matumbo (typhoid fever), tauni ya mitoki (bubonic plague), homa ya manjano (yellow fever), aina fulanifulani za mafua (influenza) na kichaa cha mbwa (rabies). 
Chanjo kwa dawa za kinga kwa magonjwa mengi hufanywa kwa kuingizwa mwilini viini vya ugonjwa  unaonuiwa kukingwa. “Kuvifungia katika vichupa maalum kwenye maabara na kuvitakasa virusi kwa chanjo za kinga, ni jambo la lazima kabla havijadungwa mwilini” – Boyce Rens-berger. Kampeni ya kimataifa ya kusambaza chanjo za kinga (vaccinations) iliyoanzishwa mwaka 1974 ili watoto kote duniani wawe wanapatiwa huduma hiyo, iliwezesha, kufikia miaka ya mwanzoni ya1980, kuwapo watoto 8,000,000 walioweza kuokolewa na vifo kutokana na magonjwa ya utotoni – Shirika la Afya Duniani (WHO). 
Dawa nyingi za kinga hizi huingizwa mwilini kwa chanjo moja tu ili kutoa kinga ya maisha. Lakini nyingine huhitajika zirudiwe kwa dozi nyingine (booster dose) baada ya muda fulani maalumu ili kuziimarisha. Kampeni hiyo ya ‘Afya kwa Wote Ifikapo Mwaka 2000’ ilianzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF). Magonjwa yaliyohusishwa yalikuwa yakiua watotot 3,500,000 kila mwaka hadi kufikia miaka ya mwisho ya 1960, ni pamoja na pepopunda (tetanus), kidonda cha kooni (diphtheria), surua (measles) na kifua kikuu (tuberculosis).
Kutoka na utafiti uliofikiwa kuhusu chanjo za kinga kwa magonjwa tofauti, hivi sasa wazazi wana uwezo mkubwa wa kuwaepusha watoto wao na magonjwa ya kuambukiza, ambayo hapo zamani yalikuwa ya kawaida.
Baada ya kupatikana kwa mafanikio makubwa ya kuutokomeza ugonjwa wa ndui (small pox) hapo mwaka 1977, kutokana na kampeni ya WHO, wataalamu wanaamini magonjwa mengine ya kuambukiza yanaweza pia, si tu kupunguzwa, bali hata kutokomezwa kabisa. Hatua mojawapo ya msingi baada ya kuutokomeza ni ya kutoa chanjo za kinga dhidi ya maambukizo kwa watoto wote.   Wakati ulipoanzishwa mpango huo wa kuokoa maisha ya mamilioni ya vizazi vijavyo, ilitarajiwa kugharimu dola milioni 500 za Kimarekani zilizohitaji mchango wa jumuiya ya kimataifa. Takwimu zinaonesha kwamba mbali na mafanikio yaliyofikiwa katika kusambaza huduma za afya mijini na vijijini Tanzania, lakini watoto kama 240,000 walio na umri wa chini ya miaka sita walikuwa wakifa kutokana na magonjwa hayo kila mwaka mnamo miaka ya mwanzoni ya 1980 – kama watoto 135 kati ya kila watoto 1,000 waliokuwa wakizaliwa. Hii inamaanisha kwamba kila mwaka watoto 145,000 wa umri wa chini ya miaka mwaka mmoja, na watoto 95,000 wa chini ya miaka sita walikuwa wakifa kila mwaka kutokana na magonjwa yaliyohitaji chanjo. Hiki ndicho kilichoifanya UNICEF ianzishe kampeni hiyo kwa nchi zote wanachama wa WHO mwaka 1974.
Mpango wa chanjo ulianzishwa Tanzania mwaka 1974 kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA), WHO, UNICEF na Wizara ya Afya. Hata hivyo, ni asilimia 35 tu ya watoto waliostahili kupewa chanjo hizo ndiyo waliokuwa wanapatiwa huduma hizo Tanzania mwaka 1988.  Tatizo mojawapo la kutekelezwa kwa mpango huu ni ubovu au uchakavu wa vifaa vya huduma hiyo, kwani dawa za chanjo zinalazimika kuwekwa katika majokofu ili zidumu na hali ya ubaridi wao uleule ziliotoka nao viwandani. Kuharibika kwa majokofu hayo katika zahanati hasa za vijijini, huku vipuri vyake vikiwa ghali na si rahisi kuvipata, kumerudisha nyuma jitihada zilizowekwa.

CHANZO   CHA   HABARI :  GAZETI  LA  JAMHURI,, February , 10, 2016

No comments:

Post a Comment