Sunday, August 2, 2020

UFUKARA UNAONDOA FURAHA.

Kwenye moja ya tafiti ambazo Daniel ametumia kwenye kitabu chake, inaonesha kwamba wale ambao wako kwenye umasikini mkubwa, ambao wanaishi chini ya kiwango cha kawaida cha maisha, wanakuwa na wakati mwingi wa kukosa furaha kuliko ambao hawapo kwenye ufukara.
Mfano kitendo tu cha kuumwa na kichwa, kinawapelekea walio kwenye ufukara kupatwa na wasiwasi zaidi kuliko ambao hawapo kwenye ufukara.
Katika changamoto za kawaida za maisha, kama kuumwa, kufukuzwa kazi, biashara kufa, kutengana na mwenza, zinawaumiza zaidi walio kwenye umasikini kuliko wale ambao hawapo kwenye umasikini.
Na kikubwa zaidi ambacho Daniel ametushirikisha kwenye hili ni kwamba kwa walio masikini, maamuzi yoyote anayofanya ni ya kupoteza.
Iko hivi, sisi binadamu huwa tunaepuka hali ya kupoteza na kupenda hali ya kupata. Hivyo hatua yoyote ya kupoteza tunayochukua, huwa tunajisikia vibaya na hilo linachangia kukosa furaha.
Kwa kuwa masikini ana uhaba wa fedha, kila fedha aliyonayo haimtoshi, hivyo akitumia fedha hiyo kupata kitu fulani, anakuwa amechagua kukosa kitu kingine. Una elfu 5 mfukoni, unataka kwenda kujiburudisha mahali, ungependa kununua chakula na kinywaji, lakini fedha hiyo haitoshi, hivyo utaishia kupata chakula tu, au kinywaji tu.
Haijalishi chakula utakachopata au kinywaji utakachokunywa kitakuwa kizuri kiasi gani, akili yako haitaangalia kile ulichopata, bali itafikiria kile ulichokosa. Hilo ndiyo linachangia hali ya kukosa furaha kwa walio masikini.
Maumivu ya kukosa ni makubwa kuliko raha ya kupata. Ukipoteza elfu 10, utaumia kuliko raha utakayoipata kwa kuokota kiasi hicho hicho cha fedha.

No comments:

Post a Comment