Monday, August 31, 2020

NGUVU YAKO YA UBUNIFU ILIYOKO NDANI YAKO NDIYO HAZINA YAKO YA PESA ULIYONAYO,

Pesa ni kitu gani mpaka karibu kila mtu anaitafuta? Kama pesa inatafutwa na kila mtu, lazima kujiuliza wapi hasa inapatikana. Je? Ni kweli wote tunafahamu sehemu au mahali inapopatikana? Kama mahali pesa ilipo hapajulikani tutawezaje kuipata? Maswali yote haya yanahitaji majibu kwanza kutoka kwa kila mmoja wetu ambaye anazitaka pesa kwa dhati.

Maswali yote haya pia ndiyo yanatoatafsiri halisi ya kwanini kila mmoja anakwambia kuwa anahangaika kutafuta pesa, wengine wanakwambia siku hizi kuwa wanapambana. Yote haya yanaonyesha dhahiri kuwa kuna vita ndani kwa ndani katika fikra, akili na nafsi zetu juu ya wapi pesa itapatikana. 

Uzoefu unaonyesha kwamba mahali pesa ilipo bado hapajulikani kwa waliowengi. Kutokana na hali hii, wengi suala la kutafuta pesa linabaki kuwa suala la kubahatisha na kubangaiza. Kutafuta pesa kwa kubangaiza kumekuwa ndiyo hali ya maisha ya kila siku kwa waliowengi. 

Wakati ukiendelea kutafuta majibu ya maswali hapo juu, ni vizuri kutambua mambo makuu muhimu juu ya pesa; Moja ni kwamba, pesa halisi inapatikana ndani yetu; Pili, pesa yote unayoiona ni ISHARA tu ya kitu fulani kilichofanyika. 

Pesa inakuwaje ISHARA na kupatikana ndani yako? 

Nguvu ya hisia ikichanganyika na matamanio ndani ya akili, inaachia nguvu ya ubunifu wa vitu na huduma mbalimbali. 

Baada ya hapo akili yako inakusukuma ili ukamilishe kazi ya kubadilisha huo ubunifu uliopo katika hali ya wazo kuwa vitu halisi ambavyo mwisho wake hukuletea pesa. 

Ndiyo maana tunasema PESA ni ishara ya nguvu ya ubunifu ulionao katika hali ya kuonekana kwa macho. Kwahiyo, pesa tunatembea nazo mawazoni mwetu, tunalala nazo usingizini, tunakuwa nazo kila mahali tunapokua. 

Kazi tunayo moja tu nayo ni kuzitoa huko ndani yetu. Ili tuweze kuzitoa pesa ndani yetu tunahitaji kuendelea kujifunza namna bora ya kuzitoa nje, maana zikikaa tutakufanazo. 

Binadamu ukishapata kile unachohitaji na ukawa na uhuru wa kuchagua upate nini na uache nini ndiyo unapata kuishi maisha ya furaha na kuridhika pia. 

Unachotakiwa kufahamu ni kwamba wewe umejaliwa nguvu ya ubunifu ndani yako na hiyo ndiyo hazina ya pesa uliyonayo. Kwahiyo, unatakiwa kuwa mtu mwenye matumaini na kuhakikisha hofu na mashaka havina nafasi kwako. 

Habari njema ni kwamba leo hii kuna idadi ya watu wengi sana ambao tunakaribia kuwa watu bilioni tisa hivi. 

Watu wote hawa wako tayari kulipa pesa ili kukidhi mahitaji yao. Unachotakiwa kufanya kama wewe ni kukidhi mahitaji ya asilimia ndogo sana ya watu wote walioko hapa duniani. 

Kwahiyo, ukiona umepata pesa ujue kuwa hiyo ni ishara inayoonyesha nguvu ya ubunifu ndani yako. 

Wengi wanaofikiri hawana pesa siyo kwamba hawana nguvu ya ubunifu tunayosema BALI ni kwamba hawajachukua muda wao kutambua kuwa nguvu hiyo ipo lakini pia hawajachukua hatua ya kuibadilisha nguvu hiyo kuwa vitu halisi vyenye thamani na ambavyo vinaweza kuuzika kwa watu wengine tukapata pesa. 

Kila wakati tuzame zaidi katika kutafiti na kufuatilia hitaji hasa la jamii tunayoweza kuifikia na katika hitaji lao hilo tuone pesa kwa macho yetu ya rohoni. 

Tukishaona kwa macho ya ndani tuanze kufanyakazi ya kuitoa ndani kwa maana ya kufanyakazi kwa vitendo ili kukidhi hitaji lililopo kwenye jamii husika. 

Kazi ya nguvu ya ubunifu ikishakamilika, watu wenye uhitaji wataleta pesa kwako na utaanza kuikusanya kwenye kapu, hapo ndio itaanza kuonekana kwa watu wengine. 

Baadae, utaanza kusikia watu mtaani wakisema fulani amezipata pesa, sijui amezitoa wapi wakati wao ndio wamezileta kwako….hivyo ndivyo maisha yanavyokwenda. 

Mpendwa msomaji wa makala hii litafakari sana suala hili la kuitoa nje pesa iliyoko ndani kwani ni rahisi kuutokomeza umaskini moja kwa moja. 

Najua unapenda kufuata njia za mkato lakini ukweli ni kwamba ukae ukijua kuwa pesa inayopatikana kwa njia za mkato inadumu kwako muda mfupi sana na wakati mwingine njia inayotumika siyo rahisi kuitumia wakati mwingine. 

Kwahiyo, wakati ukiendelea na njia zako za mkato anza taratibu kufuata kidogo kidogo njia hii ya nguvu ya ubunifu ili kutengeneza mfereji wa pesa zitiririkazo kuja kwako bila kikomo.

 

No comments:

Post a Comment