Saturday, September 5, 2020

JINSI YA KUKUZA BIASHARA KUTOKA WATU 10 MPAKA WATU 10,000 KATIKA KAMPUNI.

Jukumu La Mtendaji Mkuu (CEO)

Kwenye vitabu vingi vya biashara, majukumu ya CEO yamekuwa yanaainishwa kuwa;

1. Kuweka mwelekeo na mkakati wa kampuni na kuuwasilisha kwa wafanyakazi, wateja na wawekezaji.

2. Kuajiri, kufundisha na kutengeneza utamaduni sahihi kwenye kampuni.

3. Kukusanya mtaji na kuugawa kwa usahihi kwenye shughuli za kampuni.

4. Kuwa mwanasaikolojia mkuu wa kampuni, kwa kuwapa wengine moyo pale mambo yanapokuwa magumu.

Kutafuta, Kuajiri Na Kusimamia Vipaji.

Ukuaji na mafanikio ya kampuni unategemea sana watu unaowaajiri kwenye kampuni yako. Ni muhimu uajiri watu sahihi, wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao na hamasa ya kufanya hivyo.

Kujenga Timu Ya Watendaji.

Wakurugenzi wa vitengo mbalimbali vya biashara yako ndiyo watendaji kwenye kampuni. Hawa wanahusika kusimamia vitengo vyao ili viweze kuisaidia kampuni kufikia maono yake. Kama mkurugenzi mkuu, utaweza kukuza kampuni yako unapokuwa na timu nzuri ya watendaji.

Kujenga timu bora ya watendaji ni zoezi gumu kwa waanzilishi wachanga, kwa sababu mwanzoni walikuwa wanafanya kila kitu peke yao. Lakini sasa kampuni inakua kwa kasi, hawawezi tena kufanya hivyo. Na hapo bado wengi wanakuwa hawajawa tayari kugatua majukumu yao.

Lakini inafika hatua ambapo kama mwanzilishi huwezi tena kusimamia kila kitu peke yako, kwa sababu majukumu yanayotaka muda wako ni mengi kuliko muda ulionao. Hivyo unakuwa huna budi kujenga timu ya watendaji.

Changamoto kubwa kwenye kuajiri watendaji ni kwamba unapaswa kutafuta watu wenye uzoefu zaidi yako, kitu ambacho siyo rahisi. Lakini unapofanikiwa kuajiri mtendaji wa kwanza vizuri, wanaofuata haitakuwa changamoto kwenye kuwaajiri.

Unapokuwa na watendaji wazuri, mambo mengi kwenye kampuni yanaenda bila ya wewe mwenyewe kuhusika moja kwa moja. Unaona kama ni miujiza maana mambo yaliyokuwa yanakusumbua awali hayakusumbui tena kwa sababu wapo wanaoyafanyia kazi.

Lakini pia kuna wakati makosa yanafanyika kwenye uajiri na mtendaji anayeajiriwa anakuwa siyo sahihi. Hapo msongo unakuwa mara mbili, kwa majukumu yanayokutegemea na mtendaji asiyefaa. Mtendaji wa aina hiyo huwa chanzo cha wafanyakazi wazuri kuikimbia kampuni yako.

Muundo Wa Kampuni Na Ukuaji Wa Kasi.

Muundo wa kampuni kwenye kipindi cha ukuaji wa kasi ni jambo lenye changamoto kwa waanzilishi wasio na uzoefu. Hii ni kwa sababu inakuwa vigumu kuwa na muundo mmoja, kadiri kampuni inavyokua, ndiyo mabadiliko yanayohitajika kwenye muundo.

Masoko Na Mahusiano Ya Umma.

Masoko na mahusiano ya umma (marketing and PR) ni eneo muhimu kwenye ukuaji wa kampuni yoyote ile. Ila kwa kampuni zilizo kwenye hatua ya ukuaji wa kasi, eneo hilo ni muhimu na linapaswa kufanya kwa usahihi.

Mchango wa masoko na mahusiano ya umma ni kujenga jina la kampuni (brand), kutengeneza taswira nzuri kwa umma, kupata kutunza wateja wa kampuni.

Kwenye uchambuzi kamili utajifunza njia bora za kufanya masoko na mahusiano kwa umma ili kampuni iweze kunufaika.

Usimamizi Wa Bidhaa.

Usimamizi wa bidhaa ni eneo muhimu wakati wa ukuaji wa kasi wa kampuni. Hii ni kwa sababu uhitaji unakuwa mkubwa na hivyo kusipokuwa na usimamizi mzuri, bidhaa inaweza isiwe bora au mahitaji ya wateja yasifikiwe.

Usimamizi mzuri wa bidhaa unaiwezesha kampuni kuweka maono makubwa ya bidhaa, mipango ya kufikia maono hayo, mikakati ya kufanyia kazi na hatua za kuchukua.

Usimamizi mbaya wa bidhaa unakuwa fujo kwa kampuni nzima kwani hakuna maono, na mambo hayafanyiki kwa wakati.

Ili kuwa na usimamizi mzuri wa bidhaa, unapaswa kuwa na kitengo mahususi kwa ajili ya bidhaa, kinachosimamiwa na meneja wa bidhaa ambaye anakuwa na ujuzi wa juu kwenye bidhaa husika. Pia unapaswa kutengeneza mchakato sahihi unaofuatwa kwenye kuandaa bidhaa husika.

Fedha Na Uthaminishaji.

Fedha na uthaminishaji ni eneo muhimu kwenye ukuaji wa kasi wa kampuni. Katika kipindi cha ukuaji wa kasi, japo kampuni inaweza kuwa na wateja wengi, lakini inaweza isiwe inazalisha faida. Hivyo kama CEO utahitaji kupata fedha za kuendelea kuendesha kampuni. Huu ndiyo wakati utakaohitajika kuithaminisha kampuni na kisha kukaribisha wawekezaji kuwekeza mitaji yao. Pia unaweza kuiuza kampuni au kuipeleka kwa umma.

Kuungana Na Kununua.

Njia nyingine ya kukuza zaidi kampuni yako ni kuungana na kampuni nyingine ambayo ni kubwa zaidi au kununua kampuni ambayo ni ndogo.

Kuungana na kununua (Mergers & acquisitions) kunaiwezesha kampuni kupata bidhaa, teknolojia, timu na hata kuondoa ushindani kwenye soko.

 

3 comments:

  1. USHAURI wowote unaopokea ni ushauri tu, lazima wewe unayeupokea utafakari kwa kuangalia kile unachopitia na kisha kuona hatua sahihi za kuchukua.

    ReplyDelete
  2. Kipindi cha ukuaji wa kasi wa biashara, baada ya kuwa imepata mtaji, imekamata soko na inaajiri kwa kasi, kutoka wafanyakazi 10 mpaka kufika maelfu ya wafanyakazi ndiyo kipindi chenye changamoto kubwa. Kwa kuwa ni kampuni chache kati ya zinazoanzishwa ndiyo zinafikia hatua ya ukuaji wa kasi, maarifa kwenye eneo hilo hayapo.

    ReplyDelete
  3. kuwa na maarifa sahihi kutoka kwenye uzoefu wa wengine, inakupa moyo na kukupa nguvu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye safari hiyo

    ReplyDelete