Sunday, December 1, 2019

ACHA KUKIMBIZANA NA KILA AINA YA FURSA

Kuna fursa mpya imekuja, umeshawishiwa kwamba ni nzuri na ukafanya maamuzi ya kuingia kwenye fursa hiyo. (fuga kware)
 
Umeamua kuingia, wakati unaanza kufanya unakutana na ugumu fulani, kabla hujaanza kutatua ugumu uliokutana nao, unasikia kuna fursa nyingine bora zaidi ya hiyo ya kwanza. Hii ya sasa ni ya uhakika zaidi inalipa zaidi na haisumbui. (fuga sungura, ndiyo habari ya mjini).
 
Unaingia kwenye fursa ya pili nayo unaianza, ukiwa na matumaini makubwa, lakini pia unakutana na baadhi ya changamoto kwenye fursa hiyo, ambazo awali hukuambiwa. Wakati unaanza kufanyia kazi changamoto hizo, unasikia kuna fursa nyingine kabambe, hiyo siyo ya kukosa, ni nzuri, na haikuhitaji wewe ufanye kazi kabisa, ni kukaa kwenye mtandao tu kwa dakika chache na kuingiza fedha. Oh, tena huhitaji kufanya, wewe unaweka tu hela na wataalamu wanakusaidia kufanya unasubiri kupokea tu faida (fanya forex au cryptocurrency).
 
Kama mpaka sasa hujaelewa kinachoendelea hapo, una tatizo, na nipo hapa kutatua tatizo hilo.
 
Iko hivi rafiki, kila fursa ni nzuri na ina changamoto zake, kila fursa ina ugumu ambao lazima ukutane nao, uuvuke na ndiyo uweze kufanikiwa.
 
Sasa unapokutana na ugumu kwenye fursa moja, usikimbilie kwenye fursa nyingine, badala yake tatua ugumu huo na kuendelea na fursa hiyo mpaka ufanikiwe.
 
Ninachokuambia leo ni hiki; ACHA kukimbizana na kila aina ya fursa mpya inayokuja. Hutafanikiwa kwa kujaribu kila fikra, bali utafanikiwa kwa kuchagua fursa moja na kuifanyia kazi kweli mpaka kufanikiwa, na hapo utakutana na magumu na changamoto nyingi, katika kuyavuka magumu hayo ndiyo utafanikiwa.
 
Bilionea Richard Branson amewahi kusema fursa ni kama daladala, ukikosa moja jua kuna nyingine inakuja. Hivyo ACHA kabisa kukimbizana na kila aina ya fursa, chagua kitu kimoja na kifanye, weka kazi, weka muda na kuwa na subira na ung’ang’anizi mpaka upate kile unachotaka.
 
Na kwa kumalizia, ukiona unakaribishwa kwenye fursa ambayo unaahidiwa kupata fedha bila ya kufanya kazi yoyote ile, yaani wewe unaweka tu fedha halafu kwa namna fulani zinazaliana na unavuna faida kubwa na kwa haraka, basi jua hili; WEWE NDIYO FURSA YENYEWE.
 
ACHA kukimbizana na kila aina ya fursa, chagua kitu kimoja au vichache utakavyofanya mpaka ufanikiwe.

1 comment:

  1. Usomaji wa vitabu ni njia bora ya wewe kuweza kufikiri kwa usahihi na kuepuka kugeuzwa kuwa fursa kwa wengine

    ReplyDelete