Saturday, May 14, 2016

IDD FAIZ MAFONGO MWEKA HAZINA WA SAFARI YA NYERERE UNO 1955

Idd Faiz Mafongo

Wa Kwanza Kushoto ni Idd Faiz Mafongo Mwekahazina wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika
na Mwekahazina wa TANU.
Wanaofuatia ni: Sheikh Mohamed Ramiya wa Bagamoyo, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu
Picha Hii Ilipigwa Dodoma Railway Station Mwaka 1956 Wakati wa Kueneza TANU Katika Majimbo

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Idd Faiz Mafongo alihudhuria mkutano wa uzinduzi wa TANU katika Ukumbi wa Arnautoglu August 1954. Haifahamiki kwa hakika hasa ni lini Idd Faiz alijiunga na TANU kwa sababu kadi yake ya kwanza ya uanachama ilipotea na akapewa kadi nyingine iliyokuwa na namba 915 iliyotolewa tarehe 28 Agosti, 1954. Lakini kwa kukisia tu kutokana na kadi ambayo Idd Faiz mwenyewe aliitoa kwa kaka yake Idd Tosiri ambayo ilikuwa kadi namba 25 na yenye saini yake kama afisa aliyetoa kadi hiyo, inaweza kuchukuliwa kwa uhakika kuwa Idd Faiz alikuwa miongoni mwa wale watu wa mwanzo kabisa kuingia TANU na huenda akawa miongoni mwa wanachama ishirini wa mwanzo. Ukichukua katika fikra ukweli kwamba Ali Mwinyi Tambwe aliyekuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) aliingizwa TANU na Mtemvu katikati ya mwezi Agosti, 1955, huenda Ally Mwinyi kama katibu wa Al Jamiatul Islamiyya na Idd Faiz akiwa mweka hazina wake bila shaka wote wawili waliingia TANU wakati mmoja.
Idd Faiz na nduguye Idd Tosiri, muasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika, walikuwa Wakusu, moja ya makabila ya Kimanyema, kwa upande wa baba yao; na Wabwali kwa upande wa mama yao. Wote wawili walikuwa katika Batetera Union (Congo Association), chama kilichokuwa kikiwaunganisha Wamanyema wa Tanganyika. Mzee bin Sudi alikuwa rais muasisi wa chama hicho na baada ya kifo chake Sheikh Hussein Juma alichaguliwa kushika nafasi hiyo. Huyu Mzee bin Sudi alipata kuwa rais wa African Association katika miaka ya 1930. Batetera Union kilikuwa chama kilichoshikamana na chenye nguvu sana miongoni mwa vyama vya kikabila. Wamanyema ni kabila la Waislam watupu na kwa sababu hii hakukuwa na pingamizi katika kuunga mkono TANU. Batetera Union kilikuwa na nguvu sana kiuchumi kwa kuwa kilikuwa katika wafuasi wake, watu waliomiliki majumba na walihodhi takriban nusu ya nyumba zilizojengwa mjini Dar es Salaam kati ya vita kuu mbili za dunia. Uwezo huu wa kiuchumu pamoja na Uislam wao uliwafanya Wamanyema kuwa wapinzani wagumu wa serikali ya kikoloni na uliwanyanyua hadi kufikia kuwa mbele katika siasa mjini Dar es Salaam na katika miji mingine ya Tanganyika. Umoja wa Wamanyema ndiyo uliojenga msikiti maarufu wa Wamanyema mwaka wa 1912 uliokuwa karibu na makao makuu ya African Association. Wamanyema hawakuweza kufaidika na elimu iliyokuwa ipo mokononi mwa wamishionari. Hata hivyo Wamanyema walipiga hatua kubwa katika elimu ya dini yao na hii ndiyo sababu kuwa hadi leo utamaduni wa Kiislamu umeenea katika kila familia ya Mmanyema iwe nyumbani Kigoma au huko pwani. Mmanyema hayupo mbali sana na utamaduni wa Kiislam. Wamanyema, Warufiji na Wadigo ni katika makabila ambayo ni tabu sana kumpata Mkristo.
Idd Faiz alikuwa Mmanyema. Hadhi yake iliongezeka zaidi kwa kuwa alikuwa mweka hazina wa TANU. Vilevile aliifanyia kampeni TANU, akifuatana na Nyerere katika safari za awali za kukitangaza chama, akihutubia mikutano jukwaa moja na Nyerere.  Ilikuwa ni Idd Faiz na kaka yake Idd Tosiri ndiyo waliompeleka na kumtambulisha Nyerere kwa binamu yao Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo. Ilikuwa ni baada ya utambulisho huu kwa Sheikh Ramia ndipo urafiki ukajengeka kati ya Sheikh Ramia na Nyerere na ndiyo Nyerere akakubalika Bagamoyo. Sheikh Ramia akiwa Khalifa wa Tariqa ya Qadiriya alikuwa na murid wengi waliomfuata kama kiongozi wao. Juu ya hayo alikuwa miongoni mwa wanachuoni walioheshimiwa sana. Hakuna kilichoweza kusimama na kuota mizizi Bagamoyo bila kupata ridhaa ya Sheikh Mohamed Ramia.[1] Akiwa khalifa wa tariqa ya Qadiriya ambayo ilianzishwa na kustawishwa Bagamoya na baba yake, Sheikh Yahya Ramia, mwanzoni mwa karne ya ishirini, nguvu za Sheikh Ramia zilikuwa hazisemeki. Alichosema sheikh ndicho hicho kilichfuatwa. [1]
Safari ya Nyerere UNO ilikuwa imepangwa hata kabla Nyerere hajafika Dar es Salaam lakini ilikujakuwa Baraza la Wazee wa TANU ndiyo walikamilisha safari ile. Baraza la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir liliyachukua mafanikio ya safari ya Nyerere kuwa  jukumu lao binafsi. Sehemu ya kwanza ya maandalizi ilitakiwa ifanyike kwa siri sana. Uongozi wa TANU ulikabidhi Idd Faiz kazi ya kuandaa, kukusanya na kusimamia mfuko wa safari ya rais wa TANU kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Safari ilikuwa ifanyike mwezi wa Februari, 1955.  Mwaka wa 1953 Idd Faiz alikuwa na umri wa miaka 43, mwenye ari na nguvu tele. Alipokuwa katika kamati kuu ya  ya TANU mwaka wa 1959 aliteuliwa kuwa mweka hazina  wa taifa wa TANU pamoja na kuwa mjumbe wa Kamati Kuu. Idd Faiz alikuwa mmoja wa viongozi wa chama walioanzisha TANU Press iliyokuwa katika njia panda ya Mtaa wa Mchikichi na Livingstone mjini Dar es Salaam. TANU Press ndiyo ilikuwa ikichapisha na kusambaza jarida  la TANU – ‘’Sauti ya TANU’’ lililohaririwa na rais wa chama Julius Nyerere. Kulikuwa na gazeti ‘’Mwafrika’’ chini ya uhariri wa Rashid Heri Baghdelleh na Robert Makange. Gazeti hili liliunga mkono siasa za TANU. Kampuni  iliyokuwa ikichapa ‘’Mwafrika’’  ilimilikiwa na Mwananchi Development Corporation iliyomilikiwa na TANU na TANU ilimteua Abdul Faraj kuiongoza kampuni hiyo.
TANU ilihitaji takriban shilingi elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes ilikuwa imekusanya kiasi cha fedha kutoka majimboni ambacho kilitumika katika  safari ya Ally Sykes na Denis Phombeah kwenda kuhudhuria Pan African Congress mjini Lusaka mwaka 1953. Kilichosalia hakikutosha kumpeleka Rais wa TANU, Nyerere Amerika. Ilibidi fedha za ziada zitafutwe kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere kufanya safari hiyo. John Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha zilizotakikana. Wanachama wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU katika siku zile ikiwa bado changa ilikuwa masikini, kiasi hicho kilikuwa bado kiko nje ya uwezo wake.  Ikitambua ule upungufu wa fedha za safari ya Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya kutoa fedha katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika hazina ya TANU kukiwezesha chama kumpeleka Nyerere New York. Hata pamoja na fedha zile kutoka Al Jamiatul Islamiyya hizo fedha hazikuweza kukidhi haja.
Al Jamiatul Islamiyya haikuwa na jingine isipokuwa kumuomba Idd Faiz asafiri kwenda Tanga kupata fedha zaidi kutoka huko. Mwalimu Kihere alikuwa tayari amekusanya fedha hizo na alikuwa anasubiri tu zije zichukuliwe na kupelekwa Makao Makuu ya TANU, New Street.  TANU ilipata habari kwamba yeyote ambaye angeenda Tanga kuchukua fedha hizo kwa ajili ya safari ya Nyerere angekamatwa. Kabla ya kuondoka, Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa TANU, na John Rupia, Makamu wa Rais wa TANU, walikwenda kuonana na Idd Faiz nyumbani kwake Ilala kumuaga, kumtakia safari njema na kumpa maelezo kwa ufupi.
Safari ya kwenda Tanga haikuwa na tatizo lolote, lakini katika wakati wa kurudi basi ambalo Idd Faiz alikuwamo lilisimamishwa njiani Turiani na makachero wa Speicial Branch. Idd Faiz alikamatwa, akavuliwa nguo na kupekuliwa, lakini hakukutwa na fedha. Hili lilimshangaza na kumchanganya yule afisa aliyemkamata kwa sababu walikuwa na taarifa kwamba Idd Faiz alikuwa amechukua fedha kutoka kwa Mwalimu Kihere kule Tanga. Idd Faiz aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa Dar es Salaam kwa usaili zaidi wakati wote akiwa analindwa na askari wenye silaha. Baadaye Idd Faiz aliachiliwa huru. Zile fedha za TANU zilifika makao makuu ya TANU Dar es Salaam, salama salimini. Zilizokuwa zimepewa kubeba msichana mdogo aliykuwa abiria ndani ya basi lile alimokuwa Idd Faiz. [1]
Iddi Faizi Mafongo Aliyevaa Kanzu Koti na Tarabush Uwanja wa Ndege
Dar es Salaam Akimsindikiza Nyerere Kwenda New York, UNO 1955

Mnamo tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka kwenda New York kuhutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa. Nyerere aliiweka wazi nia ya TANU kuwa alikuwa ametumwa na wananchi wa Tangayika kuwasilisha ujumbe ufuatao:
‘’…kuona kanuni ya uchaguzi ikianzishwa na Waafrika kujiwakilisha katika taasisi zote za umma... Hii tunaamini, ni kwa mujibu wa masharti ya Makubaliano ya Udhamini na Ibara ya 76 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.’’


Mwalimu Kihere
Leo ukiingia ofisi ndogo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Lumumba hutokuta kumbukumbu yoyote ya shujaa huyu Idd Faiz Mafongo na ukienda Tanga hakuna hata mtaa mmoja uliopewa jina la Mwalimu Kihere. Hii ni bahati  mbaya au imekusudiwa ili kufifilisha michango ya mashujaa hawa? Ikiwa ni bahati mbaya huu ndiyo wakati wa kusahihisha. La ikiwa imekusudiwa swali la kujiuliza ni kipi kinachoogopwa?
CHANZO   CHA   HABARI :  MOHAMED  SAID  WEBSITE.

KARIAKOO MARKET 1949 MOJA YA KITUO CHA HARAKATI ZA SIASA DAR ES SALAAM

Wanamajlis,

Mara nyingi nimekuwa kila nikieleza historia ya TANU na harakati za kudai uhuru nimekuwa nikimtaja Abdulwahid Sykes na Kariakoo Market ambako alikuwa akifanya kazi kama Market Master. 

Soko lenyewe ndilo hilo hapo juu kama lilivyokuwa katika miaka 1950 hadi miaka ya 1970 lilipovunjwa na kujengwa soko hili tulionalo sasa. 

Bahati mbaya huwezi kuona ofisi ya Abdul Sykes lakini mkono wa kulia wa picha hiyo ni Mtaa wa Swahili ukikatizwa na Mtaa wa Tandamti (Mtaa wa Mshume Kiyate). 


Ukiufuata mtaa huo moja kwa moja utakutana na Mtaa wa Mkunguni na ndiyo mwisho wa soko. 



Kushoto ni Mtaa wa Nyamwezi.

Ofisi ya Abdul Sykes ilikuwa katikakati ya Mtaa wa Swahili na Tandamti na Swahili na Mkunguni. 

Hapo ndipo Mwalimu Nyerere alipopelekwa na Abdul na akawa Nyerere akija pale ofisini kwa Abdul kila alipokuja mjini kutoka Pugu. 

Hapo sokoni ndipo Mwalimu Nyerere alipojuana na Shariff Abdallah Attas mmoja wa watu maarufu wa Dar es Salaam enzi zile na mtu aliyekuwa anajua mengi katika historia ya TANU.



Abdul aliuza kadi za kwanza za TANU ndani ya ofisi ile kiasi kwamba iko siku alizozana na Town Clerk Mzungu aliyetaka kujua kwa nini kadi za TANU zinauzwa pale. 

Katika miaka ile ya 1950 mwanzoni hapo palikuwa moja ya vituo vya harakati na kituo kingine kilikuwa Ilala Welfare Centre ofisini kwa Hamza Mwapachu.


Hizi ndizo zilikuwa baadhi ya sehemu za harakati wakati wa mchana. 

Baada ya kazi walikuwa wakikutana Tanga Club New Street na Mkunguni kujiburudisha na kuzungumza siasa.

CHANZO  CHA   TAARIFA :  MOHAMED  SAID  WEBSITE.

MASHUJAA WA TANU WANAOSUBIRI KUTAMBULIWA WAKIWA MAKABURINI


Wazee wa Dar es Salaam katika Baraza la Wazee wa TANU na Mwalimu Julius Nyerere katika Uchaguzi Mkuu wa 1962. Masikitiko ni kuwa mashujaa hawa hadi leo nchi haijawatambua isipokuwa Nyerere peke yake. Kushoto ni Mwinjuma Mwinyikambi, Max Mbwana, Julius Nyerere na Mshume Kiyate picha ilipigwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 1962.
 
CHANZO  CHA TAARIFA :   Mohamed   Said  Website.

Wednesday, May 4, 2016

DKT. ASHA ROSE MIGIRO ATEULIWA KUWA BALOZI WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA , MAY O4 ,2016


Taarifa kutoka Ikulu May 04 2016 imeeleza kuhusu uteuzi alioufanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli, Rais Magufuli amemteua Asha-Rose Migiro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Asha-Rose Migiro anakwenda kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Peter Kalaghe ambaye amerudishwa nyumbani. Asha-Rose Migiro ataapishwa kesho Alhamisi tarehe 05 Mei, 2016 katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.