Idd Faiz Mafongo
Wa Kwanza Kushoto ni Idd Faiz Mafongo Mwekahazina wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika
na Mwekahazina wa TANU.
Wanaofuatia ni: Sheikh Mohamed Ramiya wa Bagamoyo, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu
Picha Hii Ilipigwa Dodoma Railway Station Mwaka 1956 Wakati wa Kueneza TANU Katika Majimbo
Kumbukumbu
zinaonyesha kwamba Idd Faiz Mafongo alihudhuria mkutano wa uzinduzi wa TANU
katika Ukumbi wa Arnautoglu August 1954. Haifahamiki kwa hakika hasa ni lini
Idd Faiz alijiunga na TANU kwa sababu kadi yake ya kwanza ya uanachama ilipotea
na akapewa kadi nyingine iliyokuwa na namba 915 iliyotolewa tarehe 28 Agosti,
1954. Lakini kwa kukisia tu kutokana na kadi ambayo Idd Faiz mwenyewe aliitoa
kwa kaka yake Idd Tosiri ambayo ilikuwa kadi namba 25 na yenye saini yake kama
afisa aliyetoa kadi hiyo, inaweza kuchukuliwa kwa uhakika kuwa Idd Faiz alikuwa
miongoni mwa wale watu wa mwanzo kabisa kuingia TANU na huenda akawa miongoni
mwa wanachama ishirini wa mwanzo. Ukichukua katika fikra ukweli kwamba Ali
Mwinyi Tambwe aliyekuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa
Waislam wa Tanganyika) aliingizwa TANU na Mtemvu katikati ya mwezi Agosti,
1955, huenda Ally Mwinyi kama katibu wa Al Jamiatul Islamiyya na Idd Faiz akiwa
mweka hazina wake bila shaka wote wawili waliingia TANU wakati mmoja.
Idd
Faiz na nduguye Idd Tosiri, muasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika,
walikuwa Wakusu, moja ya makabila ya Kimanyema, kwa upande wa baba yao; na
Wabwali kwa upande wa mama yao. Wote wawili walikuwa katika Batetera Union
(Congo Association), chama kilichokuwa kikiwaunganisha Wamanyema wa Tanganyika.
Mzee bin Sudi alikuwa rais muasisi wa chama hicho na baada ya kifo chake Sheikh
Hussein Juma alichaguliwa kushika nafasi hiyo. Huyu Mzee bin Sudi alipata kuwa
rais wa African Association katika miaka ya 1930. Batetera Union kilikuwa chama
kilichoshikamana na chenye nguvu sana miongoni mwa vyama vya kikabila.
Wamanyema ni kabila la Waislam watupu na kwa sababu hii hakukuwa na pingamizi
katika kuunga mkono TANU. Batetera Union kilikuwa na nguvu sana kiuchumi kwa
kuwa kilikuwa katika wafuasi wake, watu waliomiliki majumba na walihodhi
takriban nusu ya nyumba zilizojengwa mjini Dar es Salaam kati ya vita kuu mbili
za dunia. Uwezo huu wa kiuchumu pamoja na Uislam wao uliwafanya Wamanyema kuwa
wapinzani wagumu wa serikali ya kikoloni na uliwanyanyua hadi kufikia kuwa
mbele katika siasa mjini Dar es Salaam na katika miji mingine ya Tanganyika.
Umoja wa Wamanyema ndiyo uliojenga msikiti maarufu wa Wamanyema mwaka wa 1912
uliokuwa karibu na makao makuu ya African Association. Wamanyema hawakuweza
kufaidika na elimu iliyokuwa ipo mokononi mwa wamishionari. Hata hivyo
Wamanyema walipiga hatua kubwa katika elimu ya dini yao na hii ndiyo sababu
kuwa hadi leo utamaduni wa Kiislamu umeenea katika kila familia ya Mmanyema iwe
nyumbani Kigoma au huko pwani. Mmanyema hayupo mbali sana na utamaduni wa
Kiislam. Wamanyema, Warufiji na Wadigo ni katika makabila ambayo ni tabu sana
kumpata Mkristo.
Idd
Faiz alikuwa Mmanyema. Hadhi yake iliongezeka zaidi kwa kuwa alikuwa mweka
hazina wa TANU. Vilevile aliifanyia kampeni TANU, akifuatana na Nyerere katika
safari za awali za kukitangaza chama, akihutubia mikutano jukwaa moja na
Nyerere. Ilikuwa ni Idd Faiz na kaka
yake Idd Tosiri ndiyo waliompeleka na kumtambulisha Nyerere kwa binamu yao
Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo. Ilikuwa ni baada ya utambulisho huu kwa
Sheikh Ramia ndipo urafiki ukajengeka kati ya Sheikh Ramia na Nyerere na ndiyo
Nyerere akakubalika Bagamoyo. Sheikh Ramia akiwa Khalifa wa Tariqa ya Qadiriya
alikuwa na murid wengi waliomfuata kama kiongozi wao. Juu ya hayo alikuwa
miongoni mwa wanachuoni walioheshimiwa sana. Hakuna kilichoweza kusimama na
kuota mizizi Bagamoyo bila kupata ridhaa ya Sheikh Mohamed Ramia.[1]
Akiwa khalifa wa tariqa ya Qadiriya ambayo ilianzishwa na kustawishwa Bagamoya
na baba yake, Sheikh Yahya Ramia, mwanzoni mwa karne ya ishirini, nguvu za
Sheikh Ramia zilikuwa hazisemeki. Alichosema sheikh ndicho hicho kilichfuatwa. [1]
Safari
ya Nyerere UNO ilikuwa imepangwa hata kabla Nyerere hajafika Dar es Salaam
lakini ilikujakuwa Baraza la Wazee wa TANU ndiyo walikamilisha safari ile.
Baraza la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir liliyachukua
mafanikio ya safari ya Nyerere kuwa
jukumu lao binafsi. Sehemu ya kwanza ya maandalizi ilitakiwa ifanyike
kwa siri sana. Uongozi wa TANU ulikabidhi Idd Faiz kazi ya kuandaa, kukusanya
na kusimamia mfuko wa safari ya rais wa TANU kwenda Umoja wa Mataifa, New York.
Safari ilikuwa ifanyike mwezi wa Februari, 1955. Mwaka wa 1953 Idd Faiz alikuwa na umri wa
miaka 43, mwenye ari na nguvu tele. Alipokuwa katika kamati kuu ya ya TANU mwaka wa 1959 aliteuliwa kuwa mweka
hazina wa taifa wa TANU pamoja na kuwa
mjumbe wa Kamati Kuu. Idd Faiz alikuwa mmoja wa viongozi wa chama walioanzisha
TANU Press iliyokuwa katika njia panda ya Mtaa wa Mchikichi na Livingstone
mjini Dar es Salaam. TANU Press ndiyo ilikuwa ikichapisha na kusambaza
jarida la TANU – ‘’Sauti ya TANU’’ lililohaririwa
na rais wa chama Julius Nyerere. Kulikuwa na gazeti ‘’Mwafrika’’ chini ya
uhariri wa Rashid Heri Baghdelleh na Robert Makange. Gazeti hili liliunga mkono
siasa za TANU. Kampuni iliyokuwa
ikichapa ‘’Mwafrika’’ ilimilikiwa na
Mwananchi Development Corporation iliyomilikiwa na TANU na TANU ilimteua Abdul
Faraj kuiongoza kampuni hiyo.
TANU
ilihitaji takriban shilingi elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri
kwenda Umoja wa Mataifa, New York. Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na
Abbas Sykes ilikuwa imekusanya kiasi cha fedha kutoka majimboni ambacho
kilitumika katika safari ya Ally Sykes na
Denis Phombeah kwenda kuhudhuria Pan African Congress mjini Lusaka mwaka 1953.
Kilichosalia hakikutosha kumpeleka Rais wa TANU, Nyerere Amerika. Ilibidi fedha
za ziada zitafutwe kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere kufanya safari
hiyo. John Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha zilizotakikana.
Wanachama wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU katika siku zile
ikiwa bado changa ilikuwa masikini, kiasi hicho kilikuwa bado kiko nje ya uwezo
wake. Ikitambua ule upungufu wa fedha za
safari ya Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya kutoa
fedha katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya na kuzitia katika hazina ya TANU
kukiwezesha chama kumpeleka Nyerere New York. Hata pamoja na fedha zile kutoka
Al Jamiatul Islamiyya hizo fedha hazikuweza kukidhi haja.
Al
Jamiatul Islamiyya haikuwa na jingine isipokuwa kumuomba Idd Faiz asafiri
kwenda Tanga kupata fedha zaidi kutoka huko. Mwalimu Kihere alikuwa tayari
amekusanya fedha hizo na alikuwa anasubiri tu zije zichukuliwe na kupelekwa Makao
Makuu ya TANU, New Street. TANU ilipata
habari kwamba yeyote ambaye angeenda Tanga kuchukua fedha hizo kwa ajili ya
safari ya Nyerere angekamatwa. Kabla ya kuondoka, Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa
TANU, na John Rupia, Makamu wa Rais wa TANU, walikwenda kuonana na Idd Faiz
nyumbani kwake Ilala kumuaga, kumtakia safari njema na kumpa maelezo kwa ufupi.
Safari
ya kwenda Tanga haikuwa na tatizo lolote, lakini katika wakati wa kurudi basi
ambalo Idd Faiz alikuwamo lilisimamishwa njiani Turiani na makachero wa
Speicial Branch. Idd Faiz alikamatwa, akavuliwa nguo na kupekuliwa, lakini
hakukutwa na fedha. Hili lilimshangaza na kumchanganya yule afisa aliyemkamata
kwa sababu walikuwa na taarifa kwamba Idd Faiz alikuwa amechukua fedha kutoka
kwa Mwalimu Kihere kule Tanga. Idd Faiz aliwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa
Dar es Salaam kwa usaili zaidi wakati wote akiwa analindwa na askari wenye
silaha. Baadaye Idd Faiz aliachiliwa huru. Zile fedha za TANU zilifika makao
makuu ya TANU Dar es Salaam, salama salimini. Zilizokuwa zimepewa kubeba
msichana mdogo aliykuwa abiria ndani ya basi lile alimokuwa Idd Faiz. [1]
Iddi Faizi Mafongo Aliyevaa Kanzu Koti na Tarabush Uwanja wa Ndege Dar es Salaam Akimsindikiza Nyerere Kwenda New York, UNO 1955 |
Mnamo
tarehe 17 Februari, 1955 Nyerere aliondoka kwenda New York kuhutubia Baraza la
Udhamini la Umoja wa Mataifa. Nyerere aliiweka wazi nia ya TANU kuwa alikuwa
ametumwa na wananchi wa Tangayika kuwasilisha ujumbe ufuatao:
‘’…kuona kanuni ya uchaguzi ikianzishwa na
Waafrika kujiwakilisha katika taasisi zote za umma... Hii tunaamini, ni kwa
mujibu wa masharti ya Makubaliano ya Udhamini na Ibara ya 76 ya Mkataba wa
Umoja wa Mataifa.’’
Leo ukiingia ofisi ndogo
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Lumumba hutokuta kumbukumbu yoyote
ya shujaa huyu Idd Faiz Mafongo na ukienda Tanga hakuna hata mtaa mmoja
uliopewa jina la Mwalimu Kihere. Hii ni bahati mbaya au imekusudiwa ili
kufifilisha michango ya mashujaa hawa? Ikiwa ni bahati mbaya huu ndiyo
wakati wa kusahihisha. La ikiwa imekusudiwa swali la kujiuliza ni kipi
kinachoogopwa?
Mwalimu Kihere |
CHANZO CHA HABARI : MOHAMED SAID WEBSITE.
No comments:
Post a Comment