Saturday, May 14, 2016

DC KINONDONI ANUSA JIPU MSD


AlihapydcNA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Ally Hapi, ameituhumu Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwamba imechangia kudhoofisha huduma za afya katika hospitali zilizopo wilayani kwake.
Mbali na hilo, mkuu huyo wa wilaya alisema MSD wanafanya udalali kwa kuchukua fedha za hospitali za Serikali na kwenda kununua dawa katika maduka ya jumla ya watu binafsi na kuwauzia kwa bei kubwa.
“Mganga Mkuu wa Wilaya amesema baadhi ya maduka hayo yanauza dawa ya Panadol kwa Sh 7,000 kwa kopo, moja, lakini MSD wanakwenda kununua huko na kuwauzia wateja wake (hospitali) kwa Sh 14,000,  haiwezekani taasisi ya Serikali kufanya udalali halafu tuangalie tu,” alisema Hapi.
Akizungumza na watoa huduma za afya katika manispaa hiyo, Hapi alisema utafiti alioufanya katika baadhi ya hospitali za manispaa hiyo, amegundua MSD imekuwa ikikwamisha huduma kwa kuchelewesha dawa.
Alisema sambamba na hilo, pia MSD hawatoi taarifa kwa hospitali husika kama dawa walizoagizwa zipo ama la, matokeo yake hospitali zinakaa muda mrefu bila kuwa na dawa na kusababisha malalamiko kwa wananchi.
“Mfano Hospitali ya Palestina (Sinza) nimekuta wameagiza dawa za Sh milioni 18, lakini MSD wamekaa kimya kwa wiki tatu na baadaye walileta dawa za Sh milioni 2 tu,” alisema Hapi.
“Licha ya kutoa dawa kidogo, MSD hawarudishi fedha walizopewa na kubaki nazo hivyo kuzifanya hospitali zishindwe kuagiza dawa kutoka vyanzo vingine.
“Namwomba Katibu Tawala wa Wilaya amwandikie Mkuu wa Mkoa kuhusu hili ili amjulishe Rais ikibidi atumbue jipu la MSD,” alisema.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alizungumzia uhaba mkubwa wa vyandarua na mashuka katika hospitali za Palestina na Mwananyamala.
“Wanawake wanakwenda kujifungua na kukosa vyandarua hospitalini ina maana mna mpango wa kuwaambukiza malaria wakiwa hospitali?” alihoji.
Hapi alishangazwa pia na idadi kubwa ya  watumishi wa Hospitali ya Mwananyamala kwenda kusoma na kusababisha upungufu mkubwa katika hospitali hiyo.
“Hospitali ya Mwananyamala watumishi 50 wapo masomoni, ninataka kujua ni nani anayetoa ruhusa hii bila kuzingatia mahitaji yaliyopo,” alisema.
Hapi pia alitaka kila mwezi kupata taarifa ya mapato na matumizi kwa Mkurugenzi wa Manispaa.
“Nasikia kuna watu wanalipana posho na fedha zinaisha…lazima tuwe wawazi katika hili,” alisema.
Aidha Hapi alimtaka Ofisa Biashara wa Manispaa ya Kinondoni kuangalia upya vibali vilivyotolewa kwa vilabu vya pombe vilivyozunguka baadhi ya hospitali na kupiga muziki kwa sauti kubwa hadi usiku wa manane.

CHANZO   CHA  HABARI :   GAZETI  LA  MTANZANIA, JUMATANO , 11 ,MAY ,2016.

No comments:

Post a Comment