MKOA wa Dar es Salaam
umebainika kuwa na watumishi hewa 209 ambapo, hali hiyo imefanya wakuu
wote wa idara mkoani humo kula viapo vya kuchukuliwa hatua kama
watabainika wengine kutoka katika idara wanazoziongoza.
Mkuu wa mkoa huo, Paul
Makonda aliyasema hayo jana katika kikao kilichoshirikisha wakuu wote wa
wilaya, idara kutokana na taarifa za uongo kuwa mkoa huo una watumishi
hewa 71 tu.
Makonda alisema
inashangaza kuona mkoa huo kuwa na watumishi hewa 71 hivyo aliamua
kufanya uchunguzi na kubaini watumishi hewa wengine 209 ambao
wameisababishia serikali hasara zaidi ya sh. bilioni 2.9 kutokana na
fedha walizolipwa.
"Ndio maana kila Mkuu
wa Idara amekula kiapo cha kuandika na kusema ili tukiunda tume ya
uchunguzi na kubaini watumishi hewa wengine wao wahusike moja kwa moja.
Tulifanya uhakiki wa kwanza Temeke, walituambia watumishi hewa wapo 13
na mara ya pili wakasema wapo 51, mbaya zaidi tulipofanya uhakiki mara
ya tatu tukabaini wapo 64," alisema.
Aliongeza kuwa,
ongezeko la wafanyakazi hewa katika wilaya hiyo linamfanya ajiulize
maswali mengi yasiyo na majibu hivyo, hayupo tayari kuona jambo hilo
likifanywa kwa kimzaha.
Alisema kila Mkuu wa
Idara aliomba kazi kwa hiari yake, wengine walitumia rushwa ili waweze
kuipata; lakini kazi wanazofanya lazima wasimamiwe au kuandikiwa memo
ndipo wawajibike wakati majukumu yao wanayajua.
"Mkataba utaanza
kutumika Jumatatu ijayo, kuanzia leo hadi wiki ijayo kila Mkuu wa Idara
ahakikishe katika idara yake hakuna watumishi hewa, baada ya hapo
ikiundwa Tume ya uchunguzi na kubaini watumishi hewa hawa wakuu watakuwa
wanahusika," alisema.
Makonda aliongeza kuwa,
haiwezekani Rais Dkt. John Magufuli kila siku azungumzie uchafu na
watumishi hewa kwa kuitaja Dar es Salaam wakati wahusika wapo jambo
ambalo haliwezi kukubalika kwani kila mmoja anapaswa kuwahudumia
wananchi katika nafasi yake.
Katibu Tawala wa Mkoa
huo, Theresia Mmbando alisema mkoa una watumishi 26,324 ambao kati ya
hao, 166 ni wa Sektetarieti ya Mkoa, 26,158 Mamlaka ya Serikali za
Mitaa, jiji lina wafanyakazi 254 na Manispaa ya Kinondoni 9,009, Ilala
8,710, Temeke 8,185.
"Awali Kinondoni
waligundulika watumishi hewa 34, tulipofanya uhakiki mara ya pili
tuliwapata 55, hadi sasa wamefika 89, Ilala tuliwapata 21 lakini mara ya
pili wamekuwa 35.
"Baadhi ya watumishi
inadaiwa wapo masomoni bila ruhusa, likizo bila malipo, walioazimwa,
waliofariki hivyo jumla ni 209," alisema.
Hata hivyo, baadhi ya
wakuu wa idara walilamikia kitendo cha kusainishwa mikabata na kusema ni
sawa na kuwatoa kafara kwani wengine wanasainiwa na wakubwa bila wao
kujua chochote.
CHANZO CHA HABARI: GAZETI LA MAJIRA,03, MEI , 2016
No comments:
Post a Comment