HII ni Wiki ya Nenda Kwa Usalama
inayoadhimishwa kitaifa mkoani Iringa. Nimepata kuandika haya huko nyuma,
lakini nayarudia hapa kutokana na umuhimu wake kwa vile hii ni wiki maalumu ya
Nenda Kwa Usalama.
Ajali, na hususan ajali za
barabarani, limekuwa ni janga kwa nchi yetu. Kwa mujibu wa ripoti ya miaka
michache iliyopita, mtafiti wa usalama barabarani (public transport and safety)
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam T. Rwebangira , asilimia 76 ya ajali nyingi
zinazohusisha mabasi ya abiria zinatokana na mambo ya kibinadamu, asilimia 17
zinatokana na magari yenyewe na asilimia 7 ni sababu nyingine zisizoweza
kuzuilika. Hizo asilimia 17 zinabainisha kuwa vyombo vingi vya usafiri ikiwamo
mabasi mengi tunayotumia hapa Tanzania ni bomu na usalama wake si thabiti kwa
lengo la kusafirisha abiria.
Tuangalie basi hizi asilimia 76 ya
sababu za kibiniadamu zinazosababisha ajali nyingi hapa Tanzania. Mtafiti huyo
alibaini kwamba kila mwaka Tanzania inapoteza zaidi ya shilingi bilioni 20
kutokana na ajali mbalimbali za barabarani. Vyanzo na tafiti mbalimbali
vinaainisha kwamba asilimia zaidi ya 78 ya waathirika wa ajali za barabarani ni
abiria na watembea kwa miguu.
Kiundani takwimu za kuanzia miaka ya
2000 zinaonyesha asilimia zaidi ya 40 ya wanaokufa kwenye ajali za barabarani
ni abiria na zaidi ya asilimia 38 ni watembea kwa miguu. Takwimu hizo hizo
kutoka vyanzo mbalimbali zinaonyesha viini vya ajali za barabarani kuwa ni
uendeshaji wa hatari/uzembe zaidi ya asilimia 54; ubovu wa magari zaidi ya
asilimia 16; uzembe wa watembea kwa miguu zaidi ya asilimia 6.8; mwendo kasi
zaidi ya asilimia 3; uzembe wa wapanda pikipiki zaidi ya asilimia 3; uzembe wa
wapanda baisikeli zaidi ya asilimia 6; ulevi zaidi ya asilimia 1.2 na mengineyo
kama vile utelezi na ukungu husababisha zaidi ya asilimia 6 za ajali
barabarani.
Hivyo basi, zaidi ya asilimia 94 ya
ajali za barabrani zinaweza kuzuilika na jamii yenyewe. Tukiangalia sababu za
ajali nyingi za barabarani nchini utakuta nyingi zinahusiana sana na uzembe na
kutokuwa makini. Sababu kubwa ya kwanza ni ulevi wa aina zote wa madereva na
abiria. Wakati fulani nikiwa nasafiri, moja ya sifa alizokuwa anapewa dereva wa
basi nililopanda na lililokuwa likienda kwa kasi ni kuendesha akiwa na mzinga
wa Konyagi nyuma ya kiti chake. Akifika mwisho wa safari chupa hiyo ya konyagi
huwa haina kilichobaki. Eti hii pia ni sifa! Jamii nzima inapaswa kupiga vita
tabia za kilevi za madereva wetu.
Sababu nyingine ni mwendo kasi
unaoendana na kutojali sheria na alama za barabarani. Tunajua, kwamba madereva
wetu wengine wanaendesha wamelewa. Tunawaacha wakimbize basi wanavyotaka.
Tujiulize, je, dereva huyu aliyekunywa pombe kabla ya kuanza kuendesha gari
anaweza kuwa na maarifa yake ya kawaida na uwezo wake wa kawaida kumudu kasi ya
mwendo wa gari? Je, atakuwa makini na kutumia akili yake yote kwenye chombo
anachokiendesha?
Siku hizi utakuta dereva anakwenda spidi
ya kilomita 150 kwa saa halafu anazungumza na simu. Kuzungumza kwenye simu za
mikononi hakufai kabisa kwa dereva wa gari la abiria aendeshapo gari. Hii ni
hatari kwa abiria na watu wengine watembeao kwa miguu. Tunalitia hasara kubwa
taifa na familia zetu kwa mambo tunayonaweza kuyazuia bila gharama yoyote.
Mabasi mengine utakuta yamepakia
abiria na mizigo kupita kiasi. Hatari iliyopo ni basi kushindwa kupita kwenye
baadhi ya madaraja na kusababisha ajali mbaya. Tuangalie sheria Namba 30 ya
Mwaka1973 na marekebisho yake ya mwaka 1996 inayohusu ni jinsi gani magari
yanatakiwa yawe yakiwa barabarani. Tatizo letu si dereva wala abiria kama
wanasoma sheria za barabarani. Suala la ubovu wa magari nao ni sababu mojawapo
ya ajali nyingi za barabarani.
Kuna rafiki yangu aliyenusurika kufa
katika milima ya Kitonga kwa sababu basi alilopanda lenye abiria zaidi ya 65
lilikuwa halina breki. Tujiulize, je, inawezakanaje gari bovu liruhusiwe kuwa
barabarani? Kwa kutumia gari bovu hatulidanganyi Jeshi la Polisi bali tunajidanganya
wenyewe.
Kumekuwa na sababu nyingine nyingi
kama vile watu wanaondesha magari kwa sababu wana magari lakini si madereva,
kuacha nafasi ndogo kati ya gari na gari, uzoefu mdogo wa barabara na zaidi ya
yote ni dereva na hasa dereva wa mabasi anapaswa kupumzika vya kutosha. Tafiti
zinaonyesha, kwamba dereva anapaswa kupumzika kila baada ya saa mbili za
kuendesha kwa mfululizo. Na tafiti nyingine zinaonyesha dereva anapaswa
kuendesha gari kati ya saa tatu hadi nne.
Lakini kwa vyovyote vile, dereva
hapaswi kuendesha gari zaidi ya saa nne bila kupumzika. Dereva hapaswi
kulazimishwa safari, dereva anapaswa kula chakula kizuri kinachofaa, anapaswa
kulala sehemu nzuri na yenye ubora, na apewe maslahi bora. Haiwezekani hujui
dereva amelala wapi ukaruhusu aendeshe gari la abiria. Unajuaje kama alikwenda
kulala saa 9 usiku au hakulala kabisa. Tukumbuke, kwamba ajali hizi zinachukua
nguvu kazi kubwa ya nchi yetu. Na mbaya zaidi baadhi ya watu wanachukuliwa na
ajali za barabarani ni viongozi bora kabisa.
Kwa pamoja, twapaswa kuchukua hatua
katika hili na kupunguza gharama na mzigo kwa Serikali na familia zetu. Mzigo
usiokuwa na lazima kutokana na ajali za barabarani zinazoweza kuzuilika.
Na Maggid Mjengwa, 19 , Sept , 2012, GAZETI LA RAIA MWEMA
No comments:
Post a Comment