Kama
kuna kitu kimoja ambacho kila mtu anapaswa kuambiwa na kukielewa ni
kwamba matatizo yetu mengi ya kiafya yanatokana na ulaji wa sukari. Kwa
kifupi sukari ni sumu kubwa sana kwenye miili yetu. Japo tunaiona tamu
na tunaipenda sana, lakini hakuna kinachotuua kama sukari.
Sukari
ya kawaida tunayotumia inaitwa sucrose, ndani yake ina sukari rahisi za
aina mbili, glucose na fructose. Glucose ndiyo sikari inayotumika kwa
urahisi na mwili na hata ubongo katika kuzalisha nguvu. Fructose huwa
haitumiki sana kuzalisha nishati, badala yake inageuzwa kuwa mafuta na
kuhifadhiwa kwenye mwili. Na aina hii ya sukari rahisi ndiyo inachangia
sana kwenye magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kama kukomaa na kujaa
mafuta kwenye mishipa hiyo kitu kinacholeta shinikizo la juu la damu
(presha).
Ubaya
zaidi wa sukari uko hapa, unapokula chakula cha sukari au wanga, sukari
ni rahisi kumeng’enywa, hivyo muda mfupi baada ya kutumia sukari,
kiwango cha sukari kwenye damu yako kinakuwa juu sana. Hali hii
inachochea mwili kuzalisha homoni inayoitwa Insulin, ambayo kazi yake ni
kuondoa sukari kwenye damu na kuihifadhi kwenye seli za mwili na
nyingine kugeuzwa kuwa mafuta kwenye ini. Sasa kwa kuwa sukari imepanda
kwa wingi kwenye damu, insulini inayozalishwa inakuwa nyingi pia, kitu
ambacho kinapelekea sukari kwenye damu kushuka haraka. Hii inaleta hali
ya mtu kujisikia uchovu na kutamani kula kitu cha sukari muda mfupi
baada ya kula sukari.
Kama
umekuwa unakunywa chai yenye sukari asubuhi, utakuwa unaliona hili mara
kwa mara, saa moja baada ya kutumia sukari unajisikia kuchoka choka na
unatamani kitu chochote chenye sukari. Hapa ndipo wengi wanakunywa soda
au hata kula pipi, ili mradi tu kutuliza lile hitaji la mwili la kutaka
sukari ya haraka.
Ndugu yangu,
kama kuna hatua moja ambayo unapasa kuichukua, hata kama utashindwa
kuchukua hatua nyingine zozote kwenye ulaji wako, basi ni kuachana
kabisa na sukari. Yaani acha kabisa kutumia sukari, na utaupumzisha
mwili wako na hali hii ya kutengeneza sumu ambazo zinakuchosha,
kukuletea magonjwa na hata kukuzeesha haraka.
Vyakula
vya sukari vya kuepuka ni kama ifuatavyo, sukari yoyote unayoongeza
kwenye chai au chakula, asali, miwa na juisi yake, matunda yoyote yenye
utamu wa sukari, soda, juisi za matunda hata kama ni asili, bia, mvinyo,
bidhaa zozote za kiwandani ambazo zimetengenezwa kwa kuongezwa sukari,
kama mikate, maandazi na chochote ambacho kimeongezwa sukari.
Nyongeza;
usidanganyike na vitu vitamu ambavyo unaambiwa havina sukari, mfano
soda za dayati, hizi zina kemikali ambazo ni sumu kwenye mwili wako kama
ilivyo sukari. Tofauti yake na soda nyingine ni kwamba hazipandishi
sukari kwenye damu, lakini bado ni sumu.
Najua
hili litakuwa limekustua sana, kwa sababu vyakula vingi hapo ndiyo
unatumia kila siku. Lakini kutumia kila siku au kuzoea haifanyi kuwa
sahihi. Tafiti za kisayansi na za lishe zinaonesha wazi kwamba mazoea
yetu kwenye ulaji ndiyo kikwazo kwetu kuwa na afya bora. Hivyo tunapaswa
kujifunza na kuchukua hatua sahihi ili tuwe na afya bora na maisha bora
pia.
No comments:
Post a Comment