Friday, May 24, 2019

SHAUKU NI NGUVU ITAKAYOKUWEZESHA KUPATA CHOCHOTE KATIKA MAISHA YAKO.


Shauku ndiyo nguvu ya kwanza ya kukuwezesha kupata kile ambacho unataka kwenye maisha yako. Shauku ni ule msukumo wa ndani wa kukutaka upate kile unachotaka. Msukumo ambao hauondoki wala kupungua. Shauku ina nguvu kubwa ya kukusukuma kufanya mambo ambayo wengine wanaogopa, lakini kwako yanaonekana kawaida.

Watu wengi wamekuwa wanategemea hamasa iwafikishe kwenye mafanikio makubwa, lakini tatizo la hamasa ni huwa haidumu, mara kwa mara inabidi uchochee upya hamasa yako. Lakini shauku huwa haipungui wala kuhitaji kuchochewa, shauku unakuwa nayo muda wote na hii ndiyo inakusukuma wewe kupiga hatua zaidi.
 
Shauku inatokana na ile sababu kubwa inayokusukuma kupata unachotaka, ile KWA NINI inayokufanya wewe upambane kupata unachotaka. Kwa nini zinatofautiana kwa watu, wapo ambao wanafanya kwa sababu wamejitoa kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi, wapo ambao wanafanya ili kuwaonesha wengine wanaweza na kadhalika.
 
Hakikisha una msukumo mkubwa ndani yako wa kukupeleka kwenye kile unachotaka, kwa sababu bila ya msukumo huu, hakuna nguvu nyingine itakayoweza kukusaidia kupata unachotaka.

No comments:

Post a Comment