Tuesday, February 9, 2021

WEWE NI SEHEMU YA JAMII INAYOKUZUNGUKA , TENDA YATAKAYONUFAISHA JAMII .

Siku ambayo tutakufa jambo moja litakalokumbukwa kuyahusu maisha yetu ni namna tulivyoweza kugusa maisha ya wale walotuzunguka. Mali, umaarufu na mambo mengine yote huenda yakasahauliwa isipokuwa yale ambayo uligusa maisha ya watu wataendelea kuyakumbuka zaidi. Hili ndilo kusudi mama la maisha kuwa tupo Duniani kuwa sehemu ya jamii na katika si­ku za kuishi kwetu tuwe na mchango chanya kwa wale wanaotuzunguka.

Tuliona katika barua zilizopita namna maisha yetu ni duara la mahusiano. Mahusiano ya awali ni juu yetu wenyewe, wale wanaotuzunguka na mwisho ni ulimwengu mzima. Mahusiano yetu sisi wenyewe yanapokuwa mazuri ikiwa na maana kujipenda, kujielimisha na kupenda utulivu ndiko kunakozalisha kuwapenda wengine na kusambaza upendo toka mtu mmoja hadi mwingine na hatimaye ulimwengu mzima. U sehemu wetu wa jamii unatupa kujifunza kuhusu sisi wenyewe, kujifahamu na kuelewa kuwa tu familia moja ya chanzo kimoja. Kama ni mti basi wenye majani mengi yanayotokea katika utegemezi wa mizizi inayofanana.

Si watu wengi ambao huona umuhimu wa kuyatoa maisha yao kwa ajili ya kutengeneza njia kwa ajili ya wengine. Huenda kutengeneza njia ni kazi ya jasho, ngumu, isopongezwa na wakati mwingine isopewa thamani na wale wanaotendewa. Hili linafanya wengi wasiwe sehemu ya kuchangia mabadiliko chanya ya jamii zinazowazunguka. Licha hayo yote kuwa wengi hawajitoi kwa ajili ya kuongoza njia kwa jamii ipo nafasi nzuri, alama idumuyo na heshima kwa wale wote ambao wanaona maisha yao ni daraja kwa watu wengine na wana wajibu wa kuhudumia jamii katika siku za maisha yao. Unajisikiaje umepata nafasi ya maisha na ikafika ukomo hujafanya la kukumbukwa na jamii yako ?

Ishukuriwe teknolojia kwa kuwa inatupa nafasi muhimu ya kugusa maisha ya watu wengine wengi. Tunagusa maisha ya watu wengine katika yale ambayo tunayafanya kila siku. Iwe unaandika, kazi, una ujuzi fulani, una uzoefu fulani, una kitabu, una watoto au familia ndivyo unavyogusa mamia ya watu wengi. Unaweza kuanza ulipo kwa kugusa watu waliokata tamaa kwa kuwatia moyo, wale walokosa muongozo wa maisha kwa kuwasaidia kuwapa miongozo na wale walopoteza hamasa katika maisha kwa kuwahamasisha. Katika haya matendo madogo unayoyafanya unaacha alama zitakazodumu na kueleza maisha yako pindi utakapokuwa huna nafasi ya kuishi tena.

Marcus Aurelius namnukuu “As you are part of a community, act in ways that benefit your community. To act selfishly, against society, is mutiny”. Ikiwa na maana “Ukiwa Kama Sehemu ya Jamii, Tenda Katika Namna ya Kuifaidisha Jamii Yako. Kutenda kwa Kujiangalia Wewe Pekee “Uchoyo” dhidi ya Jamii ni Uasi”. Unapokosa kuihudumia jamii yako kwa vile ulivyonavyo ni sawa na mtu aliye muasi. Kwanini ufe na hazina ya hekima, uzoefu, maarifa kwa uchoyo wa kutowashirikisha wengine ?

KOCHA  MWL.JAPHET  MASATU

WhatsApp +255 716 924136 }  /   + 255  755400128

 

No comments:

Post a Comment