Friday, February 5, 2021

MAKUNDI MATATU ( 03 ) YA WATU KATIKA KUSTAHIMILI MAGUMU NA VIKWAZO MAISHANI.

Tunaishi katika zama ambazo watu wengi wanapokutana na magumu hukimbia, hurudi nyuma, hukata tamaa na wakati mwingine wapo ambao huchukua maamuzi ya kukatisha maisha yao. Magumu hayaepukiki katika maisha na yule ambaye anaweza kushinda na kuvuka ndiye mtu aliye shujaa na hodari na wakati mwingine mtu huyo huwa kivutio, mfano wa kuigwa na kioo cha kujitazamia.

Leo tunaenda kuangalia makundi makubwa matatu ya watu walivyo wanapokutana na magumu na uwezo wao wa kustahimili kushinda au kuvuka vikwazo hivyo. Jiangalie katika kila kundi namna gani maisha yako umekuwa ukiyaendesha kila siku. Utakapojiona basi fuata njia ambayo itakupa kuwa na uwezo na nguvu ya ustahimilivu wa kushinda magumu na kuvuka vikwazo.

Kundi la kwanza ni watu laini “soft people” ndani na nje. Matukio au taarifa mbalimbali zinapojitokeza ni rahisi kutetereka kwa watu hawa, ni rahisi kuumizwa, hawawezi kustahimili. Huenda wakawa ni sawa na yai. Yai nje haliwezi himili mitikisiko kwa kani au nguvu ndogo tu toka nje wanavurugika haraka. Watu hawa wanaumizwa haraka na mambo yanapobadilika, hisia zao ziko nje nje kuvurugwa na maisha. Kundi hili lina watu wengi katika jamii ambapo mtu nje na ndani hawezi stahimili magumu au vikwazo. Huwa ni wepesi kuacha kitu walichokianzisha, wepesi wa kukata tamaa na hawawezi kujaribu wakiwa na hofu kubwa vipi endapo nitakutana na magumu itakuwaje ?

Kundi la pili ni watu walio na uimara kidogo nje na ndani wanaweza kustahimili kwa muda tu ila kadri mambo yanavyokuwa magumu ndivyo wanavyorudi kuwa kundi la watu wa kwanza. Wanavurugika mapema endapo magumu wanayoyapitia hayaoneshi dalili ya kupata majibu. Wanapoteza tumaini haraka kadri mambo yanavyozidi kuonekana mbele kiza kinene. Kundi hili wapo watu wengi pia ambapo huonekana ni imara kwa nje ila mambo yanapokuwa magumu basi unaona namna wasivyo na ustahimilivu, wanachoka haraka mambo yanapokuwa hayatokei majibu. Uimara wao hulainishwa kadri mambo yanavyozidi kujaa vikwazo na masumbufu mengi.

Kundi la tatu ni watu waitwao miamba “rocks”. Watu hawa ni miamba maana si nje wala ndani ni watu imara, hakuna kitu kigumu ambacho kinawazuia kusonga mbele, kadri magumu yanavyozidi kuwa mengi ndivyo wanavyozidi nao kuimarika na kuwa miamba zaidi. Watu hawa ni watu ambao hugeuza vikwazo, magumu na masumbufu wanayoyapitia kuwa njia ya kupita kuelekea ukuu na mafanikio. Kundi hili lina watu wachache ambao tunawapa majina ni mashujaa, hodari, miamba na mifano ya kuigwa. Njia yao huenda isiwezwe na makundi mawili ya juu ila hawa watu ndio wanaofanya mabadiliko makubwa katika maisha iwe ni eneo la biashara, uongozi, taaluma, sanaa na maisha kwa ujumla. Falsafa ya Ustoa inakuandaa uwe katika kundi hili kuwa hakuna kitu kitachokukwamisha katika maisha yako. Kuwa katika magumu si wakati wa kukimbia ila ni wakati wa kukabiliana na vikwazo na kuvishinda.

Marcus anasema "The impediment to action advances action. What stands in the way becomes the way". Akiwa na maana “kuwa kila kikwazo mbele yako ni njia”. Magumu yote ambayo utapitia yanakuandaa kuwa hodari, kuwa na subira, kujijenga kihekima na kiuzoefu. Mwaka huu utakutana na matukio mengi na matukio yote yatakayojitokeza yafanye njia na kuwa mtu mwamba kuvuka hilo eneo. Haitakuwa rahisi ila utaweza kadri usivyoruhusu kukimbia utakapokuwa unapitia changamoto au magumu.

KOCHA  MWL.  JAPHET    MASATU

 (  WhatsApp  + 266 716924136  ) /  + 255 755 400128  /  + 255 688 361539


 

No comments:

Post a Comment