Wednesday, February 10, 2021

HUWEZI KUZUIA WATU WASIKUONGEE KUHUSU WEWE , NI SUALA LILILO NJE YA UWEZO WAKO.

Watu wengi wamekwama kuanzisha vitu au kuanza maisha wanayotamani wangeishi kwa maoni ya watu watanionaje. Si hilo tu wapo ambao wameacha kufanya vitu vizuri ambavyo walikuwa wanaendelea navyo kwa maoni tu watu waloyasikia au kuambiwa moja kwa moja. Kweli unawapa watu nafasi ya juu kuharibu msimamo wako kuamini katika unachokifanya ?. kwanini mtu uue ndoto zako kwa maoni ya watu. Ni nani ambaye hawezi kufanya kitu hata kiwe kizuri bila kupata maoni mbalimbali toka kwa watu wengine.

Ni kawaida kwa sisi binadamu kusukumwa kufanya kitu kwa kusikia kwanza maoni. Hatuanzi kufanya vitu mpaka tusikie baba au mama anasemaje, au mwajiri wangu anasemaje au mwalimu anasemaje au jamii inasemaje. Tusipopata maoni hayo watu wengi hawaanzi kuchukua hatua wakifikiri kuwa bila maoni hawawezi kwenda mbele. Ni watu wangapi wameacha kufanya vitu vyao ambavyo huenda vingekuwa na faida kwa wengi kwa kukosa tu maoni. Hata hivyo tunapotarajia maoni ya watu yakitoka ndo hutuharibu kabisa endapo maoni hayo yakiwa yakutuchoma hisia zetu.

Unajisikiaje kuwa umeamini kabisa ulichokifanya ni kizuri ila ulipowashirikisha watu watoe maoni yao. Unakutana na maoni hasi kuhusu ulichokiamini ni kizuri. Huenda umehangaika usiku na mchana kuandaa bidhaa, maarifa fulani au huduma ila watu wanakwambia “bidhaa yako haivutii”, “kazi yako mbaya” au “hiki kitu umelazimisha si saizi yako” au “ungeachia wengine tu wafanye. Hizi kauli zimeua hamasa ya watu wengi kufanya vile ambavyo wangeweza kuendelea kujiboresha na kufanya kwa ukubwa. Kwa kuwa jamii zetu zina watu laini kuumizwa hisia wanapoambiwa ukweli au wengine wanapo wakejeli basi huacha kufanya hivyo vitu.

Maoni ya watu yameua mwelekeo wa maisha ya watu wengi. Si watu wote hufurahia mafanikio au mabadiliko unayotaka kufanya maishani. Wengi huogopa wakikupa maoni fulani mazuri utafanikiwa zaidi kuliko wao hivyo wanatumia njia ya kukuvunja moyo katika kile unachotaka kufanya ili usikifanye na uendelee kuwa kama wao. Utakutana na kundi dogo la watu ambao maoni yao huenda yakupa nguvu na hatua kusonga mbele. Ikiwa utategemea sana maoni ya watu una hatari ya kuumizwa hisia zako na ukashindwa kuvuka hilo eneo.

Pima maoni ya watu wote wanayotoa kupitia kile unachokifanya. Usiruhusu maoni yao yakaharibu utulivu wako wa ndani bali fikiri. Mtu amekwambia bidhaa yako haivutii, kazi yako mbaya. Jitahidi kujifunza na kuingia ndani yake na kujua ni nini msukumo wake wa kusema hivyo. Ukishajua msukumo wake wa kusema hivyo kisha rejea katika maoni unayojipa mwenyewe na kisha kama kuna jambo la kujiboresha boresha zaidi na kama kuna jambo la kuachana nalo achana nalo. Haitatokea utakachokifanya watu wasisukumwe kukitolea maoni. Utoaji wao maoni ni suala usiloweza kulizuia ni nje ya uwezo wako.

Utakapofanya jambo zuri kuna watu wataibuka na kuona unachokifanya ni kitu kibaya. Wakati huo huo wengine walikiona kibaya wapo ambao wanafurahia ulichokifanya kuwa kinawasaidia na wasingependa uishie njiani. Ukiwa mtu wa kufuata maoni kila saa unapotaka kufanya vitu utajichelewesha sana katika maisha. Kupata maoni hufananishwa na kuitwa na sauti nyingi wakati mmoja na hili litakuchanganya ufuate lipi na uache lipi.

Amini maoni yako pia kuwa hata wewe unaweza kuwa sahihi katika unachokifanya na si lazima watu ndo wakupe kipimo kuwa unachokifanya ni kitu kizuri. Maadamu unachokifanya hakiondoi uhai wa mtu, utu wa mtu na hakiharibu mwili wako, akili au mazingira basi endelea kukifanya huku ukijiboresha usiku na mchana. Watu watatoa maoni kila siku hadi siku unayokufa hivyo hili lisikusumbue kuendelea mbele.

KOCHA  MWL.  JAPHET    MASATU

Whats App +255 716  924  136  )  /  +  255  755  400  128  /  + 255 688 361 539


 

1 comment:

  1. Huwa Nashangazwa Namna Kila Mtu Husema Hujipenda Mwenyewe Kuliko Wengine Ila Bado Hujiwekea Thamani Ndogo Kuheshimu Maoni Yake Ila Kuheshimu Maoni ya Watu Wengine.

    ReplyDelete