Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala ya ushauri wa changamoto, ambapo tunashauriana hatua sahihi za kuchukua katika kukabiliana na changamoto ambazo ni kikwazo kwetu kufanikiwa kimaisha.
Moja ya changamoto ambayo wengi wanapitia ni kukwama kuanza kwa sababu ya kuamini bado hawajapata maarifa ya kutosha au hakuna wa kuwasaidia au hawana MTAJI. Hilo linawapelekea kujikuta wanaendelea kujifunza na kusubiri na wasianze kabisa.
Kwenye ushauri wa leo tunakwenda kuona jinsi unavyojizuia kuanza kwa kufikiri hujawa na elimu ya kutosha au hatuna watu wa kutusaidia. Na rafiki yetu JUMA ametuandikia kuomba ushauri kwenye hili;
“Ninatamani kufanya biashara lakini kila ninayetaka kuzungumza naye na kushirikiana naye hasaidii kufika kwenye lengo langu kuhusu biashara na ninajikuta nabaki na maarifa yangu. Pia nimefanya tafiti nyingi kuhusu biashara na kilimo lakini kinachonikwamisha ni kukosa msingi bora wa elimu na kukosa mtu atakaye kusaidia kufikia malengo je nifanyeje. - Ndimi JUMA.
Nakumbuka kwenye moja ya vitabu vya utabibu , kulikuwa na nukuu ya mmoja wa waliofanya makubwa sana kwenye tasnia hiyo ya utabibu aliyeitwa William Osler, nukuu hiyo inasema; He who studies medicine without books sails an uncharted sea, but he who studies medicine without patients does not go to sea at all.
Kwenye nukuu hiyo anamaanisha yule anayejifunza utabibu bila vitabu anaogelea bahari isiyojulikana, lakini yule anayejifunza utabibu bila wagonjwa, hajaenda baharini kabisa.
Kwa maneno mengine ni sawa na mtu anayejifunza kuogelea bila hata ya kuyasogelea maji, au anayejifunza baiskeli bila hata ya kuipanda, unafikiri mtu huyo atanufaika na mafunzo hayo?
Hivyo pia ndivyo tunaweza kusema kuhusu biashara, unaweza kujifunza biashara uwezavyo, unaweza kusoma kila aina ya kitabu cha biashara, unaweza kufanya kila aina ya tafiti, lakini kama hutaingia na kufanya biashara, hujaijua biashara.
Kwenye jambo lolote lile, nadharia ni tofauti kabisa na uhalisia. Hata ukisoma kitabu kilichoandikwa na mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa kabisa, bado aliyopitia yeye siyo utakayopitia yeye. Na hata yeye angekuwa anaanza leo, angerudia kufanya yale aliyofanya hatafika viwango alivyofika.
Je ina maana kujifunza kuhusu biashara hakuna maana? Kufanya utafiti wa biashara hakuna maana? Jibu ni kuna maana mno, lakini utaiona maana hiyo pale utakapoingia uwanjani na kucheza, pale utakapofanya biashara kwa uhalisia.
Unapoingia kwenye biashara ndiyo unajifunza kuna mengi hukuwa unayajua licha ya kujifunza na kufanya tafiti nyingi. Utagundua mawazo uliyokuwa nayo awali hayakuwa sahihi na utahitajika kubadilika kulingana na soko lilivyo.
Na unapokutana na changamoto za kibiashara kiuhalisia, ndiyo sasa unajua wapi urudi kujifunza zaidi, unajua utafiti upi unahitaji kufanya zaidi kwa sababu hapo upo kwenye uhalisia.
Na vipi kama hupati wa kukusaidia? Jibu ni anza na wa kukusaidia watakuja kwako baada ya kuona unafanya.
Unajua kuongea na kupanga ni rahisi, na kila mtu anafanya hivyo. Ila wanaofanya kwa vitendo ni wachache. Hivyo kama unawaambia watu hawakuelewi, ni kwa sababu wameshakusikia unasema sana. Sasa achana na maneno na fanya vitendo. Ukianza biashara na ikaonekana, ni rahisi watu kukuunga mkono, hasa biashara inapokuwa inafanya vizuri.
Hatua za kuchukua;
1. Tambua umeshajifunza na kufanya tafiti vya kutosha, na utaendelea kujifunza kwa safari yako yote ya kibiashara.
2. Amua kuanza biashara sasa, anzia pale ulipo na kwa namna unavyoweza.
3. Anza na mteja hata mmoja, chagua tatizo unaloona linawakabili watu na unajua njia nzuri ya kulitatua, kisha anza kutatua kwa watu wachache.
4. Tumia mbinu za masoko na mauzo ulizojifunza ili kuwafikia wengi zaidi na kuwauzia pia.
5. Kwa kila hatua ya biashara yako unayopiga, jenga mfumo mzuri ambapo mtu anaweza kuona namna unavyofanya biashara na kushawishika kuungana na wewe.
6. Wachague watu sahihi na waoneshe hatua ulizopiga huku ukiwashirikisha mpango wa kukua zaidi na namna gani watanufaika kwa kuungana na wewe, kisha wape mpango wa namna gani wanaweza kuungana na wewe.
7. Pata na usome kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA, hiki siyo cha kusoma mara moja na kuacha, bali ndiyo mwongozo wako kwenye safari nzima ya kibiashara.
Nimeorodhesha hapo hatua moja mpaka saba, lakini nikueleze wazi, mambo hayatakwenda kirahisi hivyo, utakutana na changamoto mbalimbali, utakutana na magumu yatakayokufanya utake kukata tamaa. Utapingwa na kuwekewa vikwazo na watu uliotegemea wakuunge mkono. Lakini usikubali hayo yakurudishe nyuma, amua kwamba unakwenda kufanya biashara na hakuna kitakachokurudisha nyuma.
Imetosha sasa kujifunza, ingia kwenye uhalisia na uendelee kujifunza kupitia kila hatua unayopiga. Biashara ndiyo darasa la maisha, hakuna siku utajiambia umeshajua kila kitu, hivyo anza kufanya na endelea kujifunza, kwa kipindi chote unachokuwa kwenye biashara, utaendelea kujifunza zaidi na zaidi.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
MWL. JAPHET MASATU
WhatsApp = 255 716 924136 ) / + 255 755400128
No comments:
Post a Comment