Saturday, February 13, 2021

UHAI TULIONAO , TUMEAZIMA , UKIWEZA ISHI KAMA HUTAISHI TENA.

Maisha yetu ipo siku ambapo yatafika ukomo kama ambavyo yameisha ukomo kwa watu ambao tulikuwa tunawajua ila sasa hawapo nasi. Habari za kifo ni watu wengi huwa hawapendi kuzisikia licha ni habari za uhalisia na kweli kuwa kila aliyepata zawadi ya kuwa hai basi ana sifa mojawapo ya kweli siku lazima atapoteza maisha. Kupoteza ni kitu kinachotupa wasi wasi na woga watu wote duniani. Maswali mengi huwa tunajiuliza nini kitatokea pindi pumzi zetu zitakapokata. Maswali haya yameendelea kuwepo enzi na enzi hata waliokuwepo zama hizo walijiuliza ila sasa hawapo nasi.  

Tunapozaliwa huwa hatuna mashaka yoyote kuhusu maisha yetu sababu huwa tunakuwa bado ni wachanga kujua maisha yalivyo. Ukuaji unapoanza kutokea na tunapokuwa watu wazima au wazee ndipo mambo yahusuyo kifo huwa yanatufikirisha sana na wakati mwingine yanatuogopesha zaidi pale tunapoona watu wanaotuzunguka wanaondoka mmoja hadi mwingine kwa mfuatano. Huwa tunahofu huenda zamu yetu ya kifo kubisha hodi imefika. Hili ni jambo la kweli na ambalo hatupaswi kulikimbia au kuhofu bali kuwa tayari kujiandaa kukikabili kifo tunapoendelea kuishi.

Last time meditation” ina maana ya tahajudi ya muda wa mwisho. Tahajudi hii inahusisha kujipa tafakari kuwa kila kitu unachokifanya sasa huenda ndo ikawa mara yako ya mwisho kufanya na usirudie tena. Au kwa lugha nyepesi kuwa ni tafakari ya kufungua ufahamu kuwa hujui kuwa kila ambacho unakigusa sasa huenda ikawa mara yako ya mwisho kabla ya kifo hakijabisha hodi. Umuhimu wa tahajudi hii ni kukuandaa kuwa unapofanya chochote kile basi fanya kama hutapata tena nafasi ya kufanya hilo tena. Wengi huwa tunaishi kimazoea tukijua nafasi tunazopata za kuwa na watu wanaotuzunguka zitadumu kumbe maskini ndo nafasi za mwisho kuwaona na tunapokuja kusikia habari baadaye basi watu hao walikwisha kufa.

Uhai ambao tunao sasa ni nafasi ya kuazimishwa tu maana kuna wakati ambao pasipo kujua tunaweza kupoteza hii nafasi tusiipate tena. Kughairisha vitu au mambo tunakupa nafasi kubwa pasipo kujua kuwa uhai wetu unaweza kuisha wakati wowote na tusiwe tumeacha alama yoyote ya maisha yetu. Ila ni tofauti sana na pale unapojua kuwa ndani ya miezi sita ijayo hutakuwepo duniani lazima utaweka juhudi na pengine kubadili kabisa vipaumbele vya kufanya ukijua kuwa huna muda wa kutosha kufanya kila kitu.

Najua ni ngumu kuwa kila siku uwe unafikiria kuwa leo ndo siku yangu ya mwisho ya maisha hivyo nikazane kufanya vitu kwa utoshelevu. Inaweza kuwa ukajisikia vibaya kuwa na tafakari za kujiandaa kwa kifo chako ila tafakari hizi zitakusaidia kuthamini muda unaopata wa maisha, utathamini watu wanaokuzunguka wakiwa hai, utathamini kila kitu ambacho unacho sasa maana unajua kuwa hakuna kitu kitaweza kudumu milele ipo siku huharibika, huanguka au kufa kabisa. Jifunze tafakari hii ambayo itakupa kuthamini maisha yako na muda ulionao wa maisha. 

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU

+255 716 924136   /   + 255 755 400128    /   + 255 688 362 539


 

No comments:

Post a Comment