“Doctors keep their scalpels and other instruments handy, for emergencies. Keep your philosophy ready too — ready to understand heaven and earth.” Daktari hushika visu na vifaa vingine katika utayari wa mikono kwa ajili ya dharura. Ihifadhi falsafa kwa utayari wa chochote kitakachojitokeza. Kuwa tayari kuitumia kuelewa kuhusu yaliyopo Duniani.
Dharura ni jambo ambalo hukutegemea litokee ila limetokea na pengine utokeaji wake unakutaka uwe tayari kulishughulikia au usimamishe mambo mengine na ulianze nalo. Matumizi ya neno dharura tumekuwa tunalitumia vibaya katika mambo yaso dharura kabisa ila sisi tunayapa uzito kuwa ni ya dharura. Ajali imetokea na watu wameumia vibaya na wanavuja damu kiasi kwamba dakika chache bila kushughulikiwa au kukimbizwa hospitali au huduma ya kwanza wameshayapoteza maisha yao. Je dharura zetu zinakuwa na uharaka wa kiasi hiki cha kumwokoa mtu aliye katika janga la kuyaondoa maisha yake ?
Dharura inapojitokeza inahitaji uharaka na utayari bila kuchelewa. Kadri dharura iliyojitokeza ikikosekana hatua ya kuchukua ndivyo mambo yanavyokuwa mabaya na hatari zaidi. Matukio kama moto katika nyumba, milipuko ya magonjwa, vita yanahitaji hatua za haraka zichukuliwe ili watu wawe salama, watu wapone, watu wasipate madhara makubwa.
Ili dharura iweze kushughulikiwa lazima pawe na zana ziko tayari mikononi. Zana ni muhimu sana ili kuiweza dharura inapojitokeza. Maisha yetu tunahitaji zana ili kuweza kushinda dharura ambazo zitajitokeza wakati wowote ule wa maisha yetu.
Zana yetu kuu kama wanafalsafa ni kuwa na FALSAFA mapema kabla hujakutana na magumu au dharura zozote zile za kimaisha. Kutoishi kifalsafa ni hatari ni sawa na kuishi bila kuwa na zana zozote zile kukabiliana na dharura zitakazojitokeza. Utaona namna watu wasio na falsafa wanavyoumizwa na matukio maishani, wanavyovurugwa na mambo na wengine kupoteza kabisa utulivu.
Falsafa ya Ustoa inakuandaa kukutana na chochote kile tena inakuandaa usishangazwe na lolote lile. Falsafa inakuandaa namna kila kitu ulichonacho kinavyoweza kuharibika, kupotea au kuanguka kabisa. Falsafa hii inakuandaa pia namna unahitaji kuthamini vitu sasa kabla havijatoweka ili vikitoweka usiumizwe navyo, inakuandaa pia kukabiliana na makundi mbalimbali ya watu bila kuumizwa hisia zako, inakuandaa kutoongozwa na hisia katika kukabiliana na mambo. Falsafa hii ni zana ya kukuandaa kukutana na yote yanayoweza kutokea.
Watu wasioishi falsafa hukutana na mambo kwa mshangao maana hakuna maandalizi yoyote ambayo huwa wanayo kuhusu maisha na matukio yanayoweza kutokea. Hivyo wanapokumbana na magumu, misiba, watu wasumbufu, vifungo, umaarufu, uzee au magonjwa wanasumbuliwa zaidi kwa sababu wanakutwa nyakati hizo ambapo hawana zana ya kuwasaidia kuwa wastahimilivu, imara au watulivu katika hayo. Falsafa ni zana ya kuwa nayo wakati wote maana itakusaidia kuvuka changamoto nyingi utakazozipitia maishani.
KOCHA MWL JAPHET MASATU
WhatsApp +255 716 924136 ) + 255 755400128
No comments:
Post a Comment