Thursday, February 11, 2021

KUPANDA NA KUSHUKA KATIKA HARAKATI ZA MAISHA , NI JAMBO LA KUJIIMARISHA NA KUKOMAA.

Tunaishi katika wakati wa changamoto ambao watu wengi wametingwa na shughuli mbalimbali, wamezungukwa na kelele nyingi toka katika mitandao ya kijamii, habari na taarifa za kujenga hofu na matukio yasoleta furaha katika maisha. Tena kipindi hiki cha karibu toka mwaka 2019, 2020 na 2021 watu wamezidishiwa hofu, wasiwasi na kupoteza imani kuhusu kesho itakuaje. Matukio ya ugumu wa maisha, changamoto za mahusiano, milipuko ya magonjwa na matukio ya kikatili yameendelea kushamiri.

Maisha yanakumbana na mfuatano wa matukio ya kupanda na kushuka. Kuna nyakati mtu anapitia kufanikiwa au kila anachokifanya kinaleta matokeo mazuri na anapata hamasa ya kwenda mbele ila mambo huja tena yanabadilika na kila kitu mtu ambacho anafanya hakimzalii matunda au matokeo ya siku za nyuma. Nyakati hizi za kupanda na kushuka zina mafunzo makubwa kuhusu maisha yetu katika kuimarika katika mtizamo.

Mtizamo tunaoweka katika yale ambayo tunapitia yana mchango mkubwa wa kutufanya wakati tunaposhuka au kuanguka aidha tubakie hapo hapo tunalia au kulalamika au huenda tukainuka na kuendelea mbele. Mtizamo wa changamoto ukiona kama kikwazo huwezi kukivuka isipokuwa hadi ubadili hiyo changamoto au matatizo kuona ni njia ya kukua, kukomaa na kuvuka.

Si kweli kuwa maisha yataweza kuwa manyoofu wakati wote iwe biashara, mahusiano, uongozi, malezi au taaluma. Kuna nyakati mambo hubadilika yalokuwa rahisi yanakua magumu. Hivyo lazima ujijengee kuwa magumu yanapojitokeza si kuwa ukimbie, ughairishe au uache kuchukua hatua. nyakati hizo zijapo ni za kupima sasa misingi ya kifalsafa ya kistoa kama ujasiri na hekima. Ujasiri si kuwa unafanya kitu kuwa huna hofu au woga ila unaenda kukifanya licha kuwa panaweza tokea hatari, ugumu au vikwazo.

Zoezi la kujijengea taswira hasi “negative visualization” ni muhimu sana katika kujenga mtizamo wa maisha. Tumekuwa tunahimizwa sana katika hamasa mbalimbali kuwa tuwe na mtizamo chanya, tufikirie mambo yatakuwa mazuri ila tunasahau vipi endapo mambo yakienda ovyo au kuvurugika?. Vipi endapo ulichokianzisha kikiaanguka, vipi ulowategemea wakakusaliti, vipi ukiumwa na kupoteza viungo, vipi ikitokea ulipotegemea hakuna upenyo au ulowategemea wakaaga Dunia.

Upande huu wa pili wa mambo yakienda vibaya, wengi wetu huwa tunasahau kuwa nao unaweza kujitokeza. Upande huu ndo falsafa inapokuja kukujenga kuwa jifunze kujiandaa kwa mabaya, mambo yakienda ndivyo sivyo au yakigoma kabisa bado uwe na uwezo wa kusimama, kutotetereka au kutoishia njiani.

Maandalizi ya kujiandaa kupoteza ni sehemu ya kufikiria pia. Hili ni muhimu sababu katika jamii tunaishi na watu ambao nao wana damu kama sisi ila wameanguka katika walivyovianzisha, wamekumbana na magonjwa, wamesalitiwa, wamefiwa, wamepoteza kazi au kufukuzwa kazi, wamekumbana na vifungo na wengine wapo katika utumwa wa uraibu mbalimbali wa pombe, sigara, mapenzi na kadhalika.

Uhalisia wa maisha ni pamoja na kutambua kuwa mateso, magumu na masumbuko yapo kutuimarisha, kutukomaza na kutuandaa tuwe watu wenye ujasiri, haki, kiasi na hekima. Jiandae kukutana na hali za kupanda na kushuka na jiimarishe kuona unapokuwa nyakati za kushuka usiendelee kukaa chini unalia, unalalamika au kukata tamaa bali simama na inuka uendelee na safari.

KOCHA  MWL.  JAPHET    MASATU

WhatsApp +255 716924136  ) + 255 755 400 128  /  + 255 688 361  539

No comments:

Post a Comment