Tuesday, February 9, 2021

USIKIMBILIE UMAARUFU, UTAKOSA AMANI ,FURAHA NA UHURU.

Leo hii kila utakayeweza kuonana naye basi ndani kuna matamanio ya kutamani ajulikane na watu wengi. Iwe ni biashara, bidhaa, huduma au chochote alichonacho kipate umaarufu au kutambulika kwa watu wengi. Umaarufu limekuwa lengo mojawapo la watu wengi maeneo mbalimbali Duniani likitanguliwa na PESA.

Wapo wanaotamani kuwa maarufu katika wanachokifanya, wapo wanaotamani kuwa maarufu katika eneo dogo walilopo au hata kwa ukubwa. Matamanio haya ya watu wengi kutaka umaarufu mengi yanachangiwa na kutafuta furaha. Wengi wanafikiri watakapokuwa maarufu basi watakuwa na furaha isokoma.

Umaarufu unakuja na gharama zake. Gharama zake ni kunyang’anywa kwa uhuru na furaha. Mtu aliye maarufu atajitahidi kuhakikisha kuendelea kuwafurahisha wengine. Kufanya hivi ni kuuza uhuru na furaha ya maisha ndani ya mtu. Umaarufu wa mtu umefanya wengine wasiwe huru kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine, kula au kuishi kama wengine. Matokeo ya maisha yasiyo halisi huanza kukaribia kwa watu wengi walio maarufu.

Hujawahi ona namna maisha ya watu wengi maarufu yanaishia katika njia isiyo nzuri. Wapo ambao wanaishia kuanguka katika walichokuwa nacho na umaarufu, wanaanguka katika starehe na wengine wanaanguka katika matatizo ya afya ya akili kama sonona. Je ni mtu aache kutafuta umaarufu ?. huenda likawa swali kwa watu wengi wanapoona mbona kuwa maarufu ni mzigo.

Falsafa ya Ustoa inahimiza namna utulivu na uhuru ni mambo makubwa muhimu ya kuyashikilia katika maisha ya kila siku. Licha kuwa wastoa wengi hawapendelei kuweka lengo na nguvu kuwa maarufu ila namna maisha yao na yale wanayoyasimamia yanafanya kazi zao ziende mbali na kujulikana na watu wengi. Umaarufu utokanao na kazi bora unatengeneza njia iliyo na nguvu na kulinda uhuru wa mtu.

Masikitiko makubwa ni pale watu wanapokuwa na njia isiyofaa ya kutafuta kujenga umaarufu. Umaarufu wa kutumia njia za mtu kujishushia utu wake ni umaarufu unaovuma kwa muda kisha anguko lake huwa baya. Wengi ambao wamejenga umaarufu kwa njia ambazo hazikuwa halali au za ujanja ujanja muda huwaangusha hapo baadaye. Umaarufu ni gharama na mtu anapokwepa gharama huanguka mbele ya safari.

Pia utakuwa umewahi ona namna watu wengine wanavyojaribu kutumia njia za mikato kujenga umaarufu na huwa hawafiki mbali wanaanguka. Huenda wengine kuiba hadi kazi za watu, majina ya watu, kuiba majina ya bidhaa na mwisho hawadumu katika walichokifanya wanapotezwa hawasikiki tena. Umaarufu una gharama na mtu anayekwepa hii gharama anaruhusu njia ya kuanguka hapo baadaye.

Si watu wote ambao mara baada ya kuwa maarufu wanabahatika kukutana na maisha ya uhuru na furaha. Wengi wanapoteza haya mambo makubwa mawili; uhuru na furaha. Hawawi tena huru kufanya yale ambayo wao wenyewe wangeweza kufanya ila isipokuwa wanafanya katika kuwafurahisha wale wanaowafuatilia. Pili ni upotevu wa furaha kadri mtu anavyokuwa na kundi kubwa la watu wanaomfuatilia pale anapokosa kujua nini alichokuwa akikihitaji pindi akiwa maarufu. 

KOCHA MWL.JAPHET  MASATU

 WhatsApp +255 716924136 )  /    + 255 755400128

 

No comments:

Post a Comment