Kutoka
kwenye kitabu "BUILT TO SELL", mwandishi " John Warrillow " anatushirikisha hatua nane za
kufuata katika kutengeneza biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe
bila ya kuwepo kwa mwanzilishi wa biashara hiyo na pia inaweza kuuzwa
muda wowote.
(1). Chagua bidhaa au huduma yenye uwezo wa kukua.
Hatua
ya kwanza kabisa kwenye kutengeneza biashara inayojiendesha yenyewe na
unayoweza kuiuza ni kuchagua bidhaa au huduma ambayo ina uwezo wa kukua.
Bidhaa au huduma yenye uwezo wa kukua ina vigezo vitatu;
Moja, inafundishika. Ni rahisi kumfundisha mtu mwingine jinsi ya kufanya kitu hicho na akaelewa.
Mbili;
ina thamani kwa mteja. Hivyo mteja anakuwa tayari kulipa bei ambayo
umeiweka. Kama kitu kinapatikana kwa wengine, mteja ataenda kwenye bei
rahisi. Lakini kama kinapatikana kwako tu na mteja anakihitaji kweli,
atakuwa tayari kulipa bei uliyopanga.
Tatu;
manunuzi ni ya kujirudia. Mteja anahitaji kuwa anarudia tena na tena
kununua. Isiwe ni kitu ambacho mteja ananunua mara moja kwenye maisha
yake.
Baada
ya kuchagua bidhaa au huduma ambayo inafundishika, ina thamani na
manunuzi yake ni ya kujirudia, unahitaji kukaa chini na kuandika
mchakato mzima wa jinsi unavyofanya biashara yako. Kila kitu
kinachohusika kwenye biashara kinapaswa kuandikwa kwa namna ambayo mtu
mwingine anaweza kufundishwa na akaelewa na kufuata. Huu unakuwa ndiyo
mwongozo mkuu wa ufanyaji wa biashara yako.
Baada
ya kuwa na mwongozo, unapaswa kuipa jina bidhaa au huduma yako. Unaipa
jina kuitofautisha na bidhaa au huduma nyingine, hivyo inakuwa ya
kipekee kwa wateja wako. Kadiri bidhaa au huduma inavyokuwa ya tofauti
na zinazopatikana sokoni, ndivyo inakuwa na thamani kubwa kwa wateja
wako.
Baada
ya kuwa na jina linaloitofautisha bidhaa au huduma yako, andika maelezo
mafupi kuhusu bidhaa au huduma hiyo ambayo yanajumuisha faida zake na
jinsi inavyotatua changamoto za wateja wako, na tumia maelezo hayo
kwenye masoko.
Katika
hatua hii ya kwanza unachagua bidhaa au huduma moja au chache ambao
unaweza kuweka nguvu zako zote na ukawafikia wateja wengi na biashara
kukua pia. Ukifanya hatua hii kwa bidhaa au huduma nyingi utashindwa.
(2). Tengeneza mzunguko chanya wa fedha kwenye biashara.
Mzunguko
wa fedha ndiyo uhai wa biashara yako. Yeyote anayetaka kununua biashara
yako, akishaangalia kama inajiendesha yenyewe, anakwenda kuangalia
mzunguko wa fedha wa biashara hiyo.
Mzunguko
wa fedha kwenye biashara unaweza kuwa chanya au hasi. Mzunguko unakuwa
chanya pale mapato ni makubwa kuliko matumizi na hasi pale matumizi ni
makubwa kuliko mapato.
Ili
kutengeneza mzunguko chanya wa fedha kwenye biashara yako, bidhaa au
huduma unayouza inapaswa kuwafanya wateja walipe kwanza kabla ya
kuipata. Epuka kuendesha biashara ambayo mteja anapata bidhaa au huduma
kwanza halafu analipa baadaye. Hii inaifanya biashara ikae muda mrefu
bila ya fedha na hivyo kuwa na mzunguko hasi wa fedha.
Biashara
inapokuwa na mzunguko chanya, yule anayetaka kuinunua atakulipa zaidi
kwa sababu tayari biashara inazalisha, tofauti na biashara yenye
mzunguko hasi ambayo inahitaji kupokea fedha nyingi ili kujiendesha.
(3 ). Ajiri timu ya mauzo.
Baada
ya kutengeneza bidhaa au huduma ambayo utaiuza kwa wateja kulipa kabla
ya kuipata, unahitaji kujiondoa kwenye kuiuza bidhaa au huduma hiyo. Na
hapa ndipo unapohitaji timu ya mauzo, watu ambao wanaenda kuuza bidhaa
au huduma kwa niaba yako.
Hii
ni hatua muhimu sana ambayo wengi hukwama, unapouza bidhaa au huduma
yako mwenyewe, unawafanya wateja wakutegemee wewe. Lakini unapokuwa na
mfumo wa mauzo, ambao unaendeshwa na watu wa mauzo, wateja hawakutegemei
wewe bali wanategemea mfumo wa biashara.
Kazi
yako kama mjasiriamali ni kuuza kampuni yako, siyo kuuza bidhaa au
huduma za kampuni hiyo. Ajiri na tengeneza timu bora ya mauzo na ipe
mwongozo wa kuuza bidhaa au huduma yako na wewe utapata muda mwingi wa
kuikuza zaidi kampuni yako.
Unapoajiri
watu wa mauzo, ajiri ambao wana uzoefu wa kuuza bidhaa na epuka sana
watu ambao wana uzoefu wa kuuza huduma. Hii ni kwa sababu wauzaji wa
bidhaa huwa wanamuuzia mteja kile kilichopo, wakati wauzaji wa huduma
wanabadilika kulingana na mahitaji ya mteja. Kwa sasa biashara yako
inauza bidhaa, hata kama ni huduma, unapaswa kuiuza kama bidhaa, hivyo
watu waliozoea kuuza bidhaa watakusaidia kuuza vizuri bila ya kutaka
kubadili chochote.
Pia
unapoajiri watu wa mauzo, ajiri angalau wawili. Hii inaleta hali fulani
ya ushindani baina yao na inawasukuma kujituma zaidi. Mfano kama mmoja
ameuza kwa wateja 10 kwa wiki, na mwingine akauza kwa wateja 7, yule wa
wateja saba atakazana naye afike wateja 10. Kadhalika wa wateja kumi
atakazana zaidi ili asipitwe. Watu wa mauzo huwa wanapenda kujipima kwa
namba, unapokuwa na wawili na kuendelea, wanakuwa na ushindani ambao
unawasukuma zaidi.
(4 ). Acha kuuza vitu vingine vyote.
Tumeona
chanzo cha biashara nyingi kutokuuzika ni zinaendeshwa kwa vurugu, kila
kitu kinauzwa na mteja akisema anataka kitu cha tofauti anapatiwa. Sasa
hutaweza kuikuza wala kuiuza biashara kama inaendeshwa kwa vurugu kiasi
hicho.
Hivyo
baada ya kuchagua bidhaa au huduma moja kuu unayouza kwenye biashara
yako, acha kuuza vitu vingine vyote. Inawezekana kuna vitu vingine
ulikuwa unauza ambavyo vinakuingizia faida. Lakini kama vipo nje ya ile
bidhaa au huduma uliyoiainisha kama msingi mkuu wa biashara yako, basi
unapaswa kuacha kuuza vitu hivyo vingine.
Unahitaji
kuweka nguvu zako zote kwenye kuikuza biashara yako kupitia bidhaa au
huduma yenye fursa ya ukuaji zaidi. Unapojihusisha na kuuza vitu
vingine, unawapa wateja wako wakati mgumu kukuelewa na kukutegemea.
Wateja
wana tabia ya kujaribu wafanyabiashara, watakujaribu kwenye kutaka bei
ya chini zaidi, watakujaribu kwenye kutaka kitu cha tofauti na unachotoa
na watakujaribu kwa kutaka uboreshe zaidi kile unachotoa kiendane na
wao. Epuka sana mitego na majaribu haya ya wateja, simamia kile
ulichopanga na wateja wanapojifunza kwamba unasimamia nini,
wanakuheshimu kwa hilo na kuwa tayari kununua kile unachouza.
Muhimu
ni uzingatie hatua ya kwanza ya kuwa na bidhaa au huduma yenye thamani
kwa wateja na ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote.
(5). Kuwa na mpango bora wa motisha kwa mameneja wako.
Kadiri
biashara yako inavyokwenda, inazidi kukua. Timu ya mauzo inaleta wateja
na biashara inakuwa kwenye mzunguko chanya wa fedha. Kwa kuwa wewe
huhusiki moja kwa moja kwenye mauzo na wala kuandaa bidhaa au huduma,
unahitaji kutengeneza viongozi kwenye biashara yako.
Hata
mtu anayetaka kununua biashara yako, anaanza kuangalia uongozi uliopo
kwenye biashara hiyo. Hivyo utahitaji kuwapandisha cheo wafanyakazi wako
na kuwafanya kuwa mameneja, kisha kuajiri wafanyakazi wengine
watakaofanya kazi chini ya usimamizi wao.
Ili mameneja hawa wajitume kweli unahitaji kuwa na mpango bora wa motisha kwao.
Zipo
njia mbalimbali za kutoa motisha kwa mameneja wako, ipo njia ya
kuwalipa bonasi mwisho wa mwaka kutokana na ongezeko la faida, hii
inawasukuma kujituma zaidi ili kutengeneza faida kubwa.
Lakini
pia baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wanawapa mameneja wao sehemu ya
umiliki wa biashara hiyo, kwa kuwapa hisa. Kama lengo lako ni kuuza
biashara yako, usitumie njia hii, kwa sababu ukishawapa umiliki,
mchakato wa kuiuza biashara hiyo unakuwa mgumu zaidi.
Tumia
mfumo wa kulipa bonasi kutokana na ongezeko la faida. Na pale biashara
inapouzwa, basi wape zawadi ya bonasi kutokana na mauzo hayo.
(6).Tafuta dalali sahihi kwako.
Baada
ya biashara yako kuwa inajiendesha yenyewe, kwa kuwa na timu bora ya
uongozi na mzunguko chanya wa fedha, sasa unaanza kuangalia uwezekano wa
kuiuza.
Hapa
ndipo unapohitaji kutafuta dalali au wakala ambaye atakuunganisha na
wanunuaji wa biashara. Zipo kampuni ambazo hizi ndiyo kazi zake,
kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji au wanunuaji wa biashara.
Unahitaji
kuchagua kampuni ambayo utafanya nayo kazi, ambayo itakuwa upande wako.
Hivyo ongea na watu mbalimbali mpaka upate ambaye unaona anaweza
kukuwakilisha vizuri kwa wanunuzi wa biashara hiyo.
Kampuni
hizi za udalali huwa zinalipwa kwa asilimia ya mauzo bada ya mauzo
kufanyika, lakini zinakusaidia sana kukutana na wanunuzi na kuweza kuuza
biashara yako.
(7). Iambie timu yako ya uongozi kuhusu mpango wa kuuza biashara.
Timu
ya uongozi wa biashara yako ni watu ambao wana imani kubwa sana na
wewe. Ni watu ambao wanajitoa sana ili biashara yako ikue zaidi. Hivyo
unahitaji kuwa makini sana pale unapotaka kuuza biashara yako.
Kwanza
unahitaji kufanya mchakato huo kwa siri mwanzoni wakati unatafuta
mteja. Ukishapata mteja sasa, unahitaji kuiambia timu yako kuhusu mpango
wako wa kuuza.
Inaweza
kuwa wakati mgumu sana kwako kuiambia timu ambayo inakuamini kwamba
unapanga kuuza biashara hiyo, wapo ambao watakuchukulia wewe ni msaliti
na huwajali wao bali unajali fedha tu.
Hivyo
unapopanga kuwaambia, waoneshe kwamba biashara inapouzwa, hata wao pia
wananufaika. Mfano biashara ikinunuliwa na kampuni ambayo ni kubwa
zaidi, wao wanapata nafasi ya kukua zaidi. Wanakuwa kwenye mazingira
bora zaidi ya kufanya kazi na pia wanaweza kupata nafasi za juu zaidi.
Pia
waahidi kupata bonasi pale ambapo biashara itauzwa. Kwa njia hii
watakubaliana na wewe na watakuwa tayari kusaidia ili mchakato wa mauzo
ukamilike vizuri.
Ni
muhimu uiambie timu yako kwa sababu anayenunua atahitaji kukutana na
timu yako ya uongozi na pia kuna ukaguzi wa kina utakaofanyika kwenye
biashara yako, ambao utahusisha kila aliyepo kwenye timu ya uongozi.
Hatua ya nane; geuza ofa kuwa makubaliano ya kisheria.
Wale
wanaoonesha nia ya kununua biashara yako huwa wanatoa ofa ya kiasi
wanachopanga kulipa ili kununua biashara hiyo. Lakini ofa siyo
makubaliano, wakati wowote wanaweza kubadilika.
Na
katika makubaliano ya kibiashara, watu huwa wanakuwa na mbinu
mbalimbali za kupata kitu kwa bei ya chini. Mfano kwenye kuuza biashara,
mtu atatoa ofa yake, kisha atafanya uchunguzi kwenye biashara na
baadaye atakuja na matokeo ya uchunguzi na kukuambia kuna mambo ambayo
ameyaona na hataweza kulipa ofa ya kwanza na hivyo kupunguza.
Ili
kuepuka kujikuta kwenye hali hiyo, kwanza chagua ni kiasi gani upo
tayari kupokea kwa kuuza biashara yako. Hivyo wanapokuja na ofa ya juu
ya kiasi hicho kubali. Lakini pia wape muda wa ukomo, la sivyo zoezi
litachukua muda mrefu zaidi.
Wanapofanya
uchunguzi na kuja na majibu yao, ambapo watapunguza ofa yao, angalia
kama bado inaendana na mpango wako wa awali. Kama ndiyo basi kubaliana
nao na kamilisheni dili. Kama ofa yao iko chini ya mpango wako wa awali
kataa na tafuta mnunuzi mwingine.
Zoezi
la kutengeneza biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe linategemea
zaidi mfumo unaoweka kwenye biashara hiyo, unapokuwa na mfumo bora
ndivyo kazi inakuwa rahisi kwako.
Zoezi
la kuuza biashara yako huwa ni gumu na linalokuweka kwenye wakati mgumu
mno. Hivyo kama unachagua kuuza biashara, lazima ujue una kipindi
kigumu mbele yako, kuanzia kupata mnunuzi mpaka kufikia makubaliano.
Iwe
unapanga kuuza biashara yako au la, bado utanufaika sana kama biashara
yako inaweza kujiendesha yenyewe bila ya kukutegemea wewe moja kwa moja.
Hivyo fuata hatua hizi nane na utaweza kutengeneza bishara bora sana
kwako.