Wednesday, January 30, 2019

UKIONA DALILI HII KATIKA MAHUSIANO JUA MAHUSIANO YANAELEKEA KUVUNJIKA.


Mara nyingi tumekuwa tunakaa kwenye mahusiano ambayo baadaye yanaishia kuvunjika bila ya sisi kujua nini kimepelekea mahusiano hayo kuvunjika.
 
Tunaona kama kila kitu kinakwenda vizuri mpaka pale changamoto zinapoanza kuonekana wazi kwenye mahusiano hayo na yanaishia kuvunjika.
 
Ni rahisi kuamini kwamba mahusiano yamevunjika ghafla na sababu haijulikani, lakini ukiwa mwangalifu na kufuatilia kila mahusiano uliyonayo, ni rahisi kuziona dalili za awali kabisa zinazoonesha mahusiano yanayoelekea kuvunjika.
 
Kuna dalili moja na ya awali ambayo inaonesha kwamba mahusiano uliyonayo na mtu yanaelekea kuvunjika. Na sababu inaweza kuwa wewe, mwingine au wote kwa pamoja.
 
Dalili hiyo moja muhimu ni kuhesabu yale ambayo umemfanyia mwingine na yeye hajakufanyia. Ukishaanza kuona kwenye mahusiano, wewe au mwingine anaanza kuhesabu mazuri aliyofanya ambayo mwingine hajayalipiza jua hayo mahusiano hayana tena muda mrefu.
 
Inapofikia kwenye mahusiano unafanya vitu kwa kuhesabu, basi huenda hufanyi kwa moyo mmoja au yule uliyenaye kwenye mahusiano hajali chochote unachofanya. Kwa vyovyote, mahusiano hayo hayataweza kudumu, na kama yataendelea changamoto zitakuwa nyingi.
 
Na hii ni kwa mahusiano yoyote yale, kuanzia mahusiano ya kimapenzi na ndoa, mahusiano ya kindugu na kirafiki na hata mahusiano ya kikazi na kibiashara.
 
Mkiishaanza kuhesabu nani kafanya nini na nani hajafanya nini, hapo mambo yameshaanza kwenda mrama.
 
Mahusiano bora na yenye afya ni yale ambayo kila aliyepo kwenye mahusiano hayo anakazana kufanya kilicho sahihi na bora kwa mwingine kwa sababu ndiyo amechagua kufanya na anajali. Na siyo pale ambapo mtu anafanya kwa sababu mwenzake kafanya au inabidi na yeye aonekane kafanya.
 
Boresha mahusiano yako kwa kufanya kile kilicho sahihi na kutokuhesabu, na kama upande wa pili haujali basi jenga mahusiano mengine bora na wale wanaojali zaidi.
 

No comments:

Post a Comment