Mara
nyingi tumekuwa tunakaa kwenye mahusiano ambayo baadaye yanaishia
kuvunjika bila ya sisi kujua nini kimepelekea mahusiano hayo kuvunjika.
Tunaona
kama kila kitu kinakwenda vizuri mpaka pale changamoto zinapoanza
kuonekana wazi kwenye mahusiano hayo na yanaishia kuvunjika.
Ni
rahisi kuamini kwamba mahusiano yamevunjika ghafla na sababu
haijulikani, lakini ukiwa mwangalifu na kufuatilia kila mahusiano
uliyonayo, ni rahisi kuziona dalili za awali kabisa zinazoonesha
mahusiano yanayoelekea kuvunjika.
Kuna dalili moja na ya awali ambayo inaonesha kwamba mahusiano uliyonayo na mtu yanaelekea kuvunjika. Na sababu inaweza kuwa wewe, mwingine au wote kwa pamoja.
Dalili hiyo moja muhimu ni kuhesabu yale ambayo umemfanyia mwingine na yeye hajakufanyia. Ukishaanza
kuona kwenye mahusiano, wewe au mwingine anaanza kuhesabu mazuri
aliyofanya ambayo mwingine hajayalipiza jua hayo mahusiano hayana tena
muda mrefu.
Inapofikia
kwenye mahusiano unafanya vitu kwa kuhesabu, basi huenda hufanyi kwa
moyo mmoja au yule uliyenaye kwenye mahusiano hajali chochote
unachofanya. Kwa vyovyote, mahusiano hayo hayataweza kudumu, na kama yataendelea changamoto zitakuwa nyingi.
Na
hii ni kwa mahusiano yoyote yale, kuanzia mahusiano ya kimapenzi na
ndoa, mahusiano ya kindugu na kirafiki na hata mahusiano ya kikazi na
kibiashara.
Mkiishaanza kuhesabu nani kafanya nini na nani hajafanya nini, hapo mambo yameshaanza kwenda mrama.
Mahusiano
bora na yenye afya ni yale ambayo kila aliyepo kwenye mahusiano hayo
anakazana kufanya kilicho sahihi na bora kwa mwingine kwa sababu ndiyo
amechagua kufanya na anajali. Na siyo pale ambapo mtu anafanya kwa sababu mwenzake kafanya au inabidi na yeye aonekane kafanya.
Boresha
mahusiano yako kwa kufanya kile kilicho sahihi na kutokuhesabu, na kama
upande wa pili haujali basi jenga mahusiano mengine bora na wale
wanaojali zaidi.