Thursday, September 2, 2021

KUWA NA VIPAUMBELE KATIKA MAISHA NA VIFANYIE KAZI



Tunaingia katika taabu maishani sababu ya kukosa msingi wa kujipa msimamo dhidi ya mambo fulani fulani katika maisha. Mtu anaporuhusu kila kitu kiwe sehemu ya maisha yake ni kuruhusu kuyaweka maisha hatarini. Mtu anayekosa msimamo ni rahisi kuyumbishwa na hali zozote zile zitakazojitokeza katika safari ya maisha. Na watu wengi wapo katika hatari hii ya kutoyapa maisha msimamo au msingi fulani unaowaongoza kutoyumbishwa na mambo maishani.

Msimamo hauendi pekee katika maisha bali hata uendeshaji wa kazi unahitaji mtu ajiwekee msimamo fulani ili kutoyumba kwa kazi zake. Mfano kama kazi ya utabibu mtu akikosa msimamo fulani alojiwekea wa kazi ni rahisi kuyakubali mambo mengine ambayo ni nje na maadili ya kazi yake.

Msimamo huu wa maisha ni kuchagua mambo ambayo hutakuwa tayari kuyavunja iwe kwa namna yoyote ile mtu atashawishiwa. Msimamo huu ni katika kuweka ugumu wa kutovunja ahadi ambayo mtu amejiwekea mwenyewe dhidi ya misingi fulani maishani. Hili humsaidia mtu kuwa na maisha yasoyumbishwa.

Ni hatua ngumu ambayo si watu wote wanaweza kuiendea katika maisha. Kuwa maisha yao yataongozwa na misimamo fulani fulani ambayo itawafanya waonekane ni watu wenye misimamo mikali dhidi ya wengine, au watu wasojali hisia za watu wengine. Ila hakuna matokeo mazuri maishani yanaweza kujitokeza isipokuwa kwa mtu kuweka mambo yake katika msimamo asokubali kuvunja kwa namna iwayo yoyote ile.

Weka msimamo katika kazi unayofanya, weka msimamo katika namna unavyohusiana na watu na weka msimamo katika mambo yote unayojua bila kuwa na msimamo thabiti basi mambo mengi yanaweza kuharibika. Hili litakusaidia kuwa na maisha yenye uimara na utulivu wakati wote. Kuna faida kubwa katika kujenga msimamo maishani ili lolote linalokuja kwako linakukuta ukiwa imara na hutayumbishwa na kitu chochote kile. 

 

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

WhatsApp + 255 716 924 136 / + 255 755 400128 / + 255 68 361  539

 

No comments:

Post a Comment