Thursday, September 2, 2021

KUPOTEZA " TUMAINI " NI KITU KIBAYA SANA KATIKA MAISHA

Maisha yanaweza kukupitisha katika nyakati ngumu ambazo mbele yako huoni kama utatoka au kuna nafuu yoyote. Nyakati hizi ndizo zinazofanya wengine wasiamini kama lipo tumaini au njia ya kuvuka. Ni lugha ngumu mtu kukuelewa pale anapopitia magumu na unamwambia kuwa hayo magumu utashinda tu huku akiangalia hakuna dalili zozote za suluhisho. Kibinadamu si hali rahisi kushawishiwa kuwa mambo yatakaa sawa na yatapita. Hili ndilo ambalo watu wengine huamua kukatisha maisha yao kwa kuona hawaoni msaada unaoweza kuwatoa walipo.

Hali ya kukosa tumaini inaweza kumkuta mtu yeyote yule katika zama tuishizo. Mambo yanapobadilika ghafla na matarajio mbalimbali kupotea ni hali inayosababisha mtu ashuke hamasa ya kufanya vitu, changamoto zinapokuwa hazikomi, hali ngumu za kiuchumi, migogoro katika kazi au mahusiano, nyakati ngumu za masoko na biashara vinapokuja kwa pamoja kwa mtu mmoja si jambo jepesi la kuvumilika. Ni wengi utakuta wanapata hali ya kukosa hamasa, wanashuka ari ya kufanya kazi na mzigo unapowazidia basi tumaini la nafuu ya hali wapitiazo hufifia au hata kuzima kabisa. Inahitaji ustahimilivu, faraja na nguvu ya kutia moyo na watu wengine kipindi cha hali ngumu.

Mtu anapoanza kupoteza matumaini ni dalili za hatari ambapo asiposaidiwa ni rahisi kufanya maamuzi mabaya ya kimaisha. Hali ya kukosa tumaini huanza pale ambapo mtu huanza kukata tamaa kwa yale anayoyapitia. Huenda ni katika kila jaribio mtu anaona kushindwa na kuanguka. Kukata tamaa kunamsababisha mtu afadhaike na kupata hali ya kupata hatia, kuona hamasa haipo tena na kujawa na hali ya kukata tamaa kabisa ya kimaisha. Hali hizi huwatokea watu wengi wanaopitia hali za sonona katika maisha ambapo kutokana na hali mbalimbali walizoshindwa kuzikabili basi wakajikuta wanazidiwa na kupoteza tumaini.

Magumu katika maisha hayakosekani na si kuwa watu hawapitii magumu. Ikiwa kila mmoja atahadithia simulizi ya yale aloyapitia utakuja kuona unayoyapitia huenda ni madogo. Kinachotia moyo ni kuwa wapo ambao maisha yao ukiyatazama unaona la kwako unalopitia ni dogo na wakati mwingine maisha yao yanaweza kukutia moyo kuwa hupaswi kumbe kukata tamaa. Kila wasaa unapoona tumaini linafifia jipe wasaa wa kuona watu wengine wenye magumu zaidi wasivyokata tamaa wala mioyo yao kuinama.

Unaweza kupoteza kila kitu maishani na ukarejea tena katika kuyaishi maisha endapo hutapoteza “tumaini”. Watu wengi ambao wamepitia magumu, taabu na shida na wakainuka tena hawakupoteza tumaini. Waliweka tumaini kuwa licha magumu yote ambayo yamejitokeza bado wanaona ipo njia, hali zitabadilika na mbele kuna njia ya kutoka. Maisha huwa mapya pale ambapo kila unapopitia magumu hupotezi tumaini kwa kile unachokifanya, tumaini la kuishi na tumaini la kuona kila kitu kitakuwa sawa kadri muda unavyoenda.

Kuna nyakati ambazo nilipitia ngumu sana, niliona siwezi kuinuka tena, niliona ndo mwisho wa kile nilichokuwa nakitegemea ila ninashukuru kuwa nilibakiwa na hali ya kuwa na tumaini kuwa hali nayoipitia itapita. Hili limekuwa likinisaidia hata sasa kuwa kwa kila hali ambayo itatokea iwe ngumu, yenye misusuko mingi nachotakiwa kukitunza ni kuwa na tumaini kuwa mambo yataenda tu. Tumaini ni ukombozi mkubwa katika maisha tuishiyo duniani.

NA  KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES    SALAAM

WhatsApp + 255 716924136 /   + 255 755 400128

 

No comments:

Post a Comment