Saturday, July 10, 2021

AFYA NI MTAJI NAMBA MOJA UNAOPASWA KUUJENGA NA KUULINDA ILI KUFANIKIWA.

Rafiki yangu mpendwa, mdau wangu
Mtaji umekuwa sababu ambayo wengi wanaitumia kama kikwazo kwao kufanikiwa.
Na wengi wanapozungumzia mtaji, huwa wanaangalia mtaji wa aina moja tu, fedha.

Kuna mitaji mingine muhimu ambayo mtu anakuwa nayo na anaweza kuitumia kufanya makubwa kwenye maisha yake, lakini haitambui wala kuitumia.
Anang’ang’ana na mtaji mmoja tu, ambao hata akiupata bado changamoto kwake haziishi.

Leo nakwenda kukushirikisha aina nyingine ya mtaji ambao unapaswa kujijengea na kuulinda ili uweze kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Kabla sijakuambia mtaji huo ni upi, kwanza nikupe taarifa muhimu kuhusu mafanikio, ambazo wengi wamekuwa hawakupi.

MOJA; mafanikio yanataka uweze kufanya maamuzi bora na haraka kuliko wengine. Maamuzi yanawatofautisha sana wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

MBILI; mafanikio yanataka uweze kufanya kazi kwa juhudi kubwa na kwa muda mrefu kuliko wengine. Haijalishi unafanya nini, juhudi zinahitajika sana.

TATU; mafanikio yanakutaka uwe na uvumilivu mkubwa licha ya kupitia magumu na kukatishwa tamaa. Wanaofanikiwa siyo kwamba njia yao inakuwa rahisi, ila wanakuwa wagumu kuliko magumu wanayokutana nayo.

Vitu hivyo vitatu ni muhimu kuliko kingine chochote kwako kufanikiwa. Kufanya maamuzi sahihi, kuweka juhudi kuwa na kuwa mvumilivu.
Vyote hivi vitatu ni zao la AFYA.
Na hiyo AFYA ndiyo mtaji muhimu mno kwako kuweza kufanikiwa.
Bila ya afya bora, hakuna makubwa unayoweza kufanya kwenye maisha yako.




Wengi hudhani afya ni kutokuwa na magonjwa, lakini hilo siyo kweli.
Shirika la afya duniani linaeleza afya kama kuwa vizuri kimwili, kiakili, kiroho, kijamii na kiuchumi.
Kwa maana hiyo ya afya, unaweza kuwa huna ugonjwa wowote, lakini bado afya yako ikawa siyo nzuri.

Unaweza kujionea hapa ni kwa nini afya ndiyo mtaji muhimu kwako kufikia mafanikio makubwa, kwa sababu imegusa kila eneo la maisha.

Ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kujenga afya yako kwenye maeneo haya matano.

( 1 ).  MWILI.
Mwili wako ndiyo hekalu la maisha yako, ndiyo gari la kukufikisha kwenye mafanikio yako makubwa.
Bila mwili imara, hutaweza kuweka juhudi za kutosha ili uweze kufanikiwa.
Maana mafanikio yanakutaka uweke juhudi kubwa na kwa muda mrefu.
Jenga afya yako ya mwili kwa kuwa na ulaji mzuri, kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika.
Linda afya yako ya mwili kwa kuepuka magonjwa na tabia hatarishi.
Mwili unapokuwa imara, unaweza kuendesha mapambano ya mafanikio.

( 2 ). AKILI.
Akili yako ndiyo inayofanya maamuzi, mafanikio yanahitaji sana maamuzi sahihi kwenye maisha. Hivyo ni muhimu kuijenga afya ya akili ili uweze kufanya maamuzi bora kwenye maisha yako.
Jenga afya yako ya akili kwa kuilisha maarifa sahihi na kufanya mazoezi ya kufikiri kwa kina katika hali mbalimbali. Pia kuwa na muda wa kutafakari mambo yako.
Linda afya yako ya akili kwa kuepuka habari hasi, vilevi mbalimbali na mitandao ya kijamii. Vyote hivyo vinadhoofisha akili yako na kuifanya isiweze kufanya maamuzi bora.
Bila ya maamuzi bora, mafanikio yatakuwa magumu kwako.

( 3 ). ROHO.
Roho yako ndiyo kichocheo cha wewe kuendelea na safari ya mafanikio hata pale unapokutana na magumu yanayokatisha tamaa. Kama haupo imara kiroho, hutaiweza safari ya mafanikio kwa sababu ina magumu na inakatisha sana tamaa.
Jijengee afya ya kiroho kwa kusali, kufanya tahajudi na kuwa na imani imara.
Linda afya yako ya kiroho kwa kuepuka waliokata tamaa na wasiokuwa na imani, maana mambo hayo huambukizwa kwa urahisi.

( 4 ). UCHUMI.
Uchumi ni eneo muhimu kinalokupa utulivu wa kuyaendesha maisha yako. Kama hujui kesho utapata wapi fedha ya kula, akili yako haiwezi kutulia kwenye mafanikio makubwa unayotaka kufikia.
Hivyo unapaswa kujenga afya yako ya kiuchumi ili uwe na uhakika wa kuyaendesha maisha yako wakati unaendelea kupambana na mafanikio.
Kujenga afya yako ya kiuchumi hakikisha una akiba ya kuweza kuyaendesha maisha yako kwa angalau miezi sita hata kama utapoteza kipato unachoingiza sasa.
Kulinda afya yako ya kiuchumi epuka matumizi kuzidi mapato yako. Kwa kila kipato unachoingiza, tenga sehemu ya kipato hicho ambayo utaweka kama akiba.

( 5 ). JAMII.
Jamii ni wale wanaokuzunguka, ambao unawahitaji sana kwenye safari yako ya mafanikio. Huwezi kufanikiwa peke yako, chochote unachotaka kinatoka kwa watu wengine.
Jenga afya yako ya kijamii kwa kuboresha mahusiano yako na wengine, kuwajali na kuweka maslahi yao mbele. Jua utapata unachotaka kwa kuwapa wengine kile wanachotaka.
Linda afya yako ya kijamii kwa kuepuka kuwasema wengine vibaya, majungu na kuwadhulumu wengine. Hata kama unaona unaweza kufanya kwa siri, jua kuna siku mambo yote yatakuwa hadharani.

Jenga afya yako kwenye maeneo hayo matano na utakuwa moto wa kuotea mbali kwenye safari yako ya mafanikio. Kwani utakuwa na mwili wenye nguvu ya kupambana, akili yenye uwezo wa kufanya maamuzi bora, roho yenye hamasa ya mafanikio, uchumi unaokuweka huru na jamii inayokupa kile unachotaka.




KARIBU  UJIUNGE   " DARASA  ONLINE " na ujifunze jinsi ulivyo na nguvu kubwa ndani yako za kukuwezesha kufanya makubwa mno.


Unaweza kuwa unajichukulia poa na kuona huwezi kufika kwenye mafanikio makubwa, lakini kwa kujifunza   zaidi   kwa  undani  utaona wazi nguvu zako zilipo na jinsi ya kuzitumia kufanya makubwa  na  kufanikiwa. HAKUNA  UCHAWI.


Rafiki, umejifunza hapa jinsi AFYA ilivyo mtaji muhimu kwako kufanikiwa, chukua hatua sahihi sasa ili kujenga afya imara itakayokuwezesha kufika kwenye mafanikio makubwa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU, DAR ES  SALAAM , TANZANIA

Tuwasiliane  nami  sasa ili  nikuunge  katika   "DARASA   ONLINE "  kwa   kutumia  EMAIL   YAKO   YA  GMAIL "


( WhatsApp  + 255 716 92 4136  ) /   + 255 755 400128

No comments:

Post a Comment