Saturday, July 10, 2021

KILA MTU ANA KIU YA KUTENDEWA UKARIMU / MEMA---" UKARIMU NI MGUSO WA PEKEE KWA KILA BINADAMU.

Maisha yetu sisi binadamu yanahitaji mguso. Mguso wa kutendewa mambo mazuri hata kama sisi tunawatendea wengine mabaya au tu wabinafsi. Ile kiu ya kutendewa mambo kwa ukarimu huwa kunatugusa sana. Kiu hii au njaa hii imo kwa kila mtu katika moyo wake kutamani kuona anapata kutendewa mema na mazuri. Licha tunaweza kuishi katika nyakati ambazo zimejaa watu wenye chuki, wasio na upendo bado mioyo yetu inatafuta wapi itapata ukarimu, wapi upendo ulipo, wapi furaha ilipo na wapi pa kupata matumaini.

Jamii zetu zina upungufu mkubwa wa watu ambao wana mioyo ya majitoleo. Kila mtu anapambana kuona ni kwa vipi atafaidika kuliko namna atakavyosaidia wengine wafaidike kwanza. Hili linajenga watu wakose ukarimu, wakose kusaidia wengine na wengine hata kuzuia wengine kupata vitu vizuri. Ukarimu imekuwa bidhaa adimu katika maisha tunayoishi maana kila mtu anajifikiria yeye mwenyewe tu na kusahau kuangalia wengine.

Usijekushangaa pale mtu mkarimu anapoonekana ni bidhaa adimu sokoni anapokuwa ni mtu anayewajali wengine, anayewatanguliza wengine, anayejitoa kwa faida ya watu wengine, anayejitosa kuingia gharama kwa ajili ya watu wengine. Si jambo rahisi kupatikana kwa kila mtu kuwa tayari kuingia gharama katika kujisahau yeye kwanza na kuwafikiria wengine kuwa kwa kuwafanyia wengine ukarimu ni yeye mwenyewe kujifanyia ukarimu. Ni vile mtu anavyojitoa kusaidia wengine ni yeye anajisaidia, ni kama vile mtu anavyoona kuwanyima nafasi wengine kufanikiwa ndivyo na yeye anavyojinyima kufanikiwa. Lolote lile tunalowafanyia wengine si kuwa wanaathirika wao tu bali hata sisi tunaathirika iwe moja kwa moja au njia nyingine.

Watu waliojeruhika ni wengi katika mioyo yao, watu walipitia mateso na taabu ni wengi, watu walopita manyanyaso ni wengi. Tendo la ukarimu kwa makundi haya ya watu ni jambo kubwa lisiloweza kupimika. Watu hawa wana kiu na njaa ya kuona hata kidogo wapate kuona matendo mema na ya ukarimu yakifurika katika maisha yao. Tendo jema lina mguso na huacha alama kubwa kwa maisha ya watu.

Tunaishi sasa na ipo siku ambayo tutayaacha maisha haya ya mwili na kufa. Kumbukumbu la maisha yetu itaanzia kwanza katika wema tulotenda kwa wengine au ubaya kwa wengine. Matendo mema huliliwa sana na watu ambao walitenda katika siku za uhai wao. Matendo ya ukarimu hugusa mioyo ya watu na huacha alama njema ya jina la mtu duniani. Tafuta nafasi hata ndogo ya kuonesha matendo ya ukarimu kwa watu wanaokuzunguka. Utaacha mguso usiofutika katika maisha yao na hii ni maana njema ya kuishi kikamilifu na kuishi kwa umoja kwa kuhesabu watu wanaokuzunguka ni sehemu ya viungo vya mwili wako.

UJUMBE : TAFUTA   NAFASI YA  KUTENDA  TENDO   LA  UKARIMU. MUNGU  AKUBARIKI  SANA.

Ndimi  KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

 ( WhatsApp + 255 716 924136 ) / + 255  755 400 128 

 

No comments:

Post a Comment