Tuesday, June 1, 2021

JISUKUME UANZE LEO , UJITOSE LEO , UMALIZE LEO UTAREKEBISHA MBELE YA SAFARI

Imekuwa ni jambo rahisi kwa watu wengi kughairisha vitu nami nikiwa mmojawapo ya watu ambao nimewahi kupitia hali za kughairisha vitu na baadaye ikawa ni ngumu kufanya tena. Kughairisha kunafariji pale ambapo kitu ulichopaswa kufanya wakati huo unakisogeza mbele au kusema nitafanya baadaye na hilo kushindwa kulifanya. Kughairisha kumeiba ndoto zetu na zimefanya tusiishi kitoshelevu wakati ambao tulikuwa na nafasi ya kufanya.

Unapoghairisha mambo unavuta hali ya kuzembea kuanza kitu ambacho kilikuwa kinawezekana kuanza. Unapofika wakati ujao kile ulichofikiria ungekianza kinaanza kuwa kigumu kukifanya na kadri muda uendavyo unapata ukinzani mkubwa zaidi na hilo linafanya usifanye chochote kile. Wakati unaofaa kuanza kufanya kitu ni wakati huo huo unaosema siwezi sasa nifanye baadaye.

Mara nyingi tunapotaka kuanza kitu basi ndani yetu tunapata sauti ambazo zinatufanya tujishauri kuwa ngoja nitafanya wakati mwingine si sasa. Ile nafasi ya kuamua sasa inapopotea ndivyo wakati unaokuja baadaye inakuwa ngumu kweli kweli kuanzisha kitu. Au wakati mwingine gharama ya jambo ambalo ungelifanya sasa inaweza kuwa mara mbili kwa baadaye. Kumbe kuanzisha kitu sasa kunasaidia kupata matokeo ya haraka zaidi kuliko kujichelewesha.

Kila kitu katika maisha kinahitaji safari na kadri unavyojishauri usianze kufanya kitu ndivyo unavyochelewa katika safari ya kitu hicho. Utakuwa umekutana na watu ambao walikuwa na nafasi ya kuanzisha biashara mapema wakiwa na nguvu ila wanangoja hadi wanapostaafu ndo wanataka kuanzisha biashara ambapo kupata mafanikio kunakuwa kugumu kuliko wale ambao walianza mapema wakaujua mchezo wa biashara na kujua namna ya kuendesha biashara. Unapochelewa kuanza kitu ndivyo unavyochelewa kujifunza mengi zaidi juu ya hicho kitu.

Kuna faida tele za kuanza sasa, wakati ambao wengine wanasema wataanza baadaye wewe jisukume uanze leo, umalize leo na ujitose leo maana muda utakapopita utakuwa upo mbali sana kuliko wengine. Unapojifunza kuchukua hatua leo ndivyo unavyoweza kufanikiwa mapema katika maisha.

Ndimi   Rafiki  Yako

 KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM, TANZANIA

WhatsApp + 255 716 924 136 /  + 255 755 400  128 /   0688 361 539  /  +255 629 748 937

EMAIL :   japhetmasatu@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment