Saturday, January 2, 2021

JINSI UMASKINI UNAVYOHARIBU AKILI NA JINSI YA KUEPUKA MTEGO WA UMASKINI.

Umasikini siyo tu ni mzigo na kikwazo kwa mtu kuwa na maisha bora na yenye uhuru, bali pia ni laana ambayo inamfanya anase kwenye maisha ambayo hawezi kujinasua.

Utafiti ambao umewahi kufanywa nchini Marekani na India unaonesha kwamba umasikini huwa unaharibu akili ya mtu.

Utafiti huo ulionesha kwamba wale wanaoishi kwa umasikini, wana upungufu wa alama 13 za kipimo cha akili (IQ) ukilinganisha na wale ambao hawaishi kwenye umasikini.

Kwa lugha rahisi na ya kueleweka vizuri ni kwamba umasikini unawafanya watu kuzidi kuwa wajinga.




Swali unaloweza kujiuliza ni kwa namna gani umasikini unaharibu akili za watu na kuwafanya kuwa wajinga?

Jibu liko wazi, masikini anakuwa ametingwa zaidi na mawazo ya hali ngumu anayokuwa anapitia, hivyo akili yake inakuwa imechoka muda wote. Inapokuja kwenye uhitaji wa kufikiri mambo makubwa na magumu, masikini hawezi kufikiri kwa usahihi, kwa kuwa akili yake tayari imeshachoka.

Chukua mfano wa watu wawili, wana elimu sana na wanafanya kazi ya aina moja. Mtu A ni tajiri na B ni masikini. Mtu A ameamka asubuhi, kapata kifungua kinywa kizuri, kaingia kwenye gari yake binafsi na kwenda kazini. Mtu B ameamka hana hata kifungua kinywa, anaenda kazini kwa kutumia usafiri wa umma ambao ni wa shida na hajui siku hiyo atakula nini, wakati huo huo kuna watu wanamdai na wanamtafuta sana. Watu hao wawili wanapewa jukumu moja la kukamilisha, ambalo linahitaji utulivu wa akili ili kulikamilisha, unafikiri yupi atalikamilisha kwa umakini?

Unajionea mwenyewe hapo, jinsi ambavyo umasikini unakuwa mzigo ambao unaharibu akili ya mtu na kumfanya awe mjinga.

Umasikini unapunguza uwezo wa mtu kufikiri na kufanya maamuzi kwa sababu muda mwingi akili yake inakuwa imetingwa na fikra na hofu mbalimbali.

Mbaya zaidi sasa, na hapa ndipo ilipo laana ya umasikini, ni pale uwezo mdogo wa kufikiri unapomfanya mtu afanye maamuzi mabovu zaidi na yanayomfanya abaki kwenye umasikini.

Tuendelee na mfano wa mtu B, ambaye anafikiria siku yake inaishaje, maana mshahara umeshaisha na mwezi ndiyo kwanza uko katikati. Anasikia kuna mtu anatoa mkopo wa haraka ila una riba kubwa. Kwa sababu anachohofia zaidi ni fedha na hawezi kufikiri kwa usahihi, anajikuta anachukua mkopo huo. Anakuja kulipa mkopo kwa riba kubwa, kitu kinachopunguza kipato chake zaidi.

Maamuzi mengi ambayo mtu anasukumwa kuyafanya akiwa masikini huishia kuwa maamuzi ya kumuumiza zaidi na kumfanya abaki kwenye umasikini.

Unaondokaje kwenye mtego na laana hii ya umasikini?

Umejionea hapo jinsi umasikini unavyoharibu akili na kumnasa mtu kwenye umasikini zaidi.

Kama bado hujafikia uhuru wa kifedha, kama bado unategemea kipato unacholipwa kwa kufanya kazi au biashara ndiyo uendeshe maisha yako, haijalishi kipato hicho ni kikubwa kiasi gani, upo kwenye hii hatari.

Hivyo hatua muhimu kwako kuchukua ni kujijengea uhuru wa kifedha. Na hapa kuna maeneo sita muhimu ya kufanyia kazi ili kuondoka kwenye mtego na laana ya umasikini.

Eneo la kwanza ni kuongeza kipato chako. Kipato chochote unachoingiza sasa hakiwezi kukutosha, gharama za maisha zinachukua sehemu kubwa ya kipato chako. Hivyo pambana kuongeza kipato chako. Kama umeajiriwa anzisha biashara ya pembeni. Kama upo kwenye biashara ongeza huduma na bidhaa zaidi na wafikie wateja wengi zaidi. Kwa kipato chochote unachoingiza sasa, pambana kukikuza zaidi.

Eneo la pili ni kudhibiti matumizi yako. Matumizi huwa yana tabia ya kukua kadiri kipato kinavyokua. Usipoyadhibiti, ongezeko la kipato ulilopambana nalo halitaleta tofauti kwenye maisha yako, badala yake litakuwa limekuchimbia kwenye umasikini zaidi. Dhibiti matumizi yako kwa kuhangaika na yale ya msingi pekee, hasa kama unaanzia kwenye umasikini wa chini kabisa.

Eneo la tatu ni kuwa na akiba ya dharura ya miezi 6 mpaka 12. Kama unaishi maisha ya mkono kwenda kinywani, yaani unafanya kazi, unaingiza kipato na unakitumia chote, basi upo kwenye hatari ya umasikini kuharibu akili yako zaidi. ukipata dharura yoyote ile, iwe ni kazi kusimama au biashara kuyumba, utaanguka vibaya mno. Hakikisha unakuwa na akiba ya kukuwezesha kuendesha maisha yako kwa miezi sita mpaka 12 hata kama hutakuwa na kipato kabisa. Unapokuwa na akiba ya aina hii, unapata utulivu mkubwa ndani yako na kuweza kufanya maamuzi sahihi kwako. Mfano kama umefukuzwa kazi na huna akiba, utalazimika kufanya kazi yoyote hata kama haikulipi, kwa sababu unataka kipato cha kuendesha maisha. Lakini kama umefukuzwa kazi na una akiba ya miezi 12 ya kuendesha maisha, unaweza kusubiri kwa muda mpaka upate kazi nzuri, maana akiba ya kuendesha maisha ipo.

Eneo la nne ni uwekezaji. Huwezi kufanya kazi muda wote na kila muda ambao hufanyi kazi hunufaiki. Unapaswa kuwa na njia ya kuingiza kipato hata kama hufanyi kazi moja kwa moja. Na njia ya kufanya hivyo ni kuwa na uwekezaji ambao unazalisha faida na kukua thamani kadiri muda unavyokwenda. Unapokuwa na uwekezaji unaozalisha faida kubwa ya kukuwezesha kuendesha maisha yako hata kama hufanyi kazi moja kwa moja, unakuwa umefikia uhuru wa kifedha.

Eneo la tano ni kulipa madeni ambayo unayo. Kama umekopa, pambana kulipa madeni yako kwa kutumia ongezeko la kipato ulilofanyia kazi.

Eneo la sita ni kuacha kukopa. Usikope tena, rahisisha maisha yako, punguza yasiyo muhimu na kama kitu huwezi kukimudu jipe muda. Vitu vingi unavyoingia kwenye madeni ili kuwa navyo ni vitu ambavyo siyo muhimu sana kwako. Ukiacha kuiga maisha ya wengine na kuchagua kuishi maisha yako, hutahangaika na mikopo inayokusumbua.

Zingatia maeneo hayo sita ili kuweza kuondokana na mtego na laana ya umasikini.

Ndimi   KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU ,  DAR  ES  SALAAM

 ( WhatsApp + 255 716 924 136 ) /  + 255 755400128 /  + 255 688361539

EMAIL : japhetmasatu@gmail.com

 

1 comment: