Saturday, January 30, 2021

INATOSHA KUWA UNACHOKIFANYA NI KIZURI HUHITAJI PONGEZI ZA WATU

 Mitandao ya kijamii imeteka watu wengi na kuwaumiza wengi pale ambapo watu wanashirikisha maisha yao au matukio fulani ili watu wengine wawapongeze au kuwafurahia “likes” au “Comments”. Ikitokea mtu kashirikisha kitu iwe picha yake na hakuna mtu yeyote anayesema umependeza au unaonekana vizuri basi watu wengi wanaumia kuwa inaonekana watu hawajapenda nilichofanya. Watu wengi wanakazana lakini wanaumia kuwa wanachokifanya watu hawatoi mrejesho.

Zama tuishizo zimekosa subira pia katika kuweka mambo ya siri kuwa siri na ya umma kuwa ya umma. Ila watu wengi utaona maisha ya siri au mambo ya faragha wanasukumwa kushirikisha wengine kwa nia mbalimbali na moja ni kupongezwa na watu wengine. Matarajio makubwa ambayo mtu anaweka kuwa akishirikisha atapongezwa na asipopongezwa huumia ndani yake. Huu ni mtego na utumwa ambao unawaendesha watu wengi wasio na udhibiti wa maisha yao.

Mstoa Marcus Aurelius nanukuu “A man when he has done a good act, does not call out for others to come and see, but he goes on to another act, as a vine goes on to produce again the grapes in season.” Hii ikiwa na maana “Mtu ambaye kafanya tendo jema, hapaswi ita watu wengine waje na kuona, ila huendelea na tendo lingine jema. Hufanya vile mzabibu utoavyo zabibu kila vipindi vyake”. Matendo mema hujitangaza yenyewe na hutoa mchango mkubwa kwa maisha bila msukumo wa pongezi au hongera toka nje.

Huhitaji pongezi ndo uendelee kufanya kitu chochote kilicho bora katika maisha yako. Ondoa haya matarajio na huu utumwa ambao utakuzuia kufanya mambo mazuri katika maisha. Ikiwa unachokifanya ni kizuri basi furaha ya ndani kukifanya inatosha na huhitaji kulazimisha watu watoe pongezi kwa ulichokifanya. Wengi huu mtego hunasa hasa pale ambapo wanafanya vitu vizuri na wanasukumwa kuwashirikisha wengine kwa lengo la kusikia “hongera” au “keep it up”. Ukikosa mrejesho huo utaumiza hisia zako na kama wanafalsafa hatuhitaji kuumia kihisia kwa vitu vilivyo katika udhibiti wetu.

Endelea kutenda yaliyo mazuri bila msukumo wa nje kufanya hilo. Nguvu kubwa ambayo unaweka katika kufanya yaliyo na mchango chanya yanatengeneza utoshelevu mkubwa ndani ya mtu atendaye. Hili linatosha na mengine yatakayotokea ni ya ziada si lazima yatokee. Si lazima watu wakupongeze kwa kazi nzuri unayofanya, si lazima kupongezwa kwa hatua nzuri ulofikia. Usikubali kuwa mtumwa wa kuhitaji wengine watambue unachokifanya. Kazi yako ni kutenda kilicho kizuri na hili latosha katika safari ya maisha mengine ni ya ziada tu.

Jifunze kufanya kitu kilicho kizuri au kupiga hatua nzuri katika maisha na usiumizwe na hali zozote zitakazojitokeza za watu kutojali ulichokifanya, kutokupongeza au kupata utambulisho au utambuzi wa mchango wako “recognition”. Hesabia kuwa sehemu ya pongezi si jambo la lazima kupata. Inatosha kufanya kazi nzuri na ndani yako kupata utoshelevu na furaha. Shinda jambo hili ili uwe na utulivu mkubwa ndani yako. Zoezi hili linaweza kuwa gumu kuanza ila ukishazoea hutakwamishwa na chochote kile wala kuumizwa na matarajio “expectations” unayoweka maishani.

Jitahidi kusoma kitabu cha mwandishi William Irvine cha “A Guide to Good Life” kikiwa kinampa msingi mwanafalsafa yeyote mchanga ambaye atapenda kujifunza falsafa ya Ustoa. Kisome na kiishi hakika utakuwa imara katika maisha yako.

KOCHA    MWL.  JAPHET   MASATU

WhatsApp  +255 716 924 136

No comments:

Post a Comment