Saturday, January 30, 2021

JIFUNZE KUHUSU ASILI NA ULIMWENGU KUJIHUSU WEWE.

Mwaka 2020 nilikuwa nikijipa zoezi kubwa la kubadilisha kila juma lilolokuwa likipita kwa kulipa jina na kukisoma kitu hicho kwa kina na kukiishi. Nilifanya majuma mengi yaloenda kwa majina kama “Utulivu”, Muziki, Upendo, Machozi, Utoaji na Asili. Somo la asili nilikuwa nikishirikisha tafakari nyingi kuhusu asili kwa siku saba kupitia mtandaoni tu kwa njia ya kuta za mtandao “Status wall”. Somo hili lilipendwa na wengi na wengi waliona namna wanapata nguvu mpya kuona kumbe asili ni mwalimu na mtunza siri za nguvu kubwa za Maumbile mbalimbali ulimwenguni.  

Nikatia uzito zaidi wa somo hili la asili nilipoona na Marcus Aurelius Mstoa naye kaandika katika kitabu chake cha “The Meditations”. Namnukuu “The more you learn about nature and the universe, the more you learn about yourself. For without knowing where you are, you can’t know who you are, or the role you have to play”. Maneno haya yakiwa na tafsiri ya “Kadri unavyojifunza zaidi kuhusu asili na ulimwengu, ndivyo unavyojifunza mengi kujihusu wewe. Kama ilivyo usipojua utokako, ni Kazi wewe kujijua wewe ni nani au una kazi gani kubwa hapa “duniani” ya kufanya. Maneno haya ndio yanayoenda kubeba msingi wa barua yetu ya leo.

Asili ni mwalimu wa falsafa ya utoaji usiokoma. Ona jua linavyofanya kazi pasipo kuchoka kwa watu wote, ona namna usiku na mchana usivyokoma, ona namna asili ina mimea na wanyama ambao kwa mategemeano kuna chakula na hewa safi inayosaidia viumbe hai kuendelea kuishi. Ona namna asili licha kuwepo kwa vifo vya viumbe bado inaleta uzao mpya usiokoma vizazi hadi vizazi. Utoaji huu unafanya asili iendelee kustawi na kukua kusikokoma.

Asili ni mhifadhi wa hazina ya hekima kupitia vilivyomo kuanzia mimea, wanyama, watu, milima, bahari, mito na mabonde. Masomo makubwa ya maisha hutayakosa ukijifunza moja kwa moja kutoka katika asili. Watu hutalii maeneo mbalimbali duniani ili wajifunze maisha na kujifahamu zaidi. Hazina ya hekima iliomo katika asili haipimiki na haielezeki. Mimea hutufunza juu ya utoaji, juu ya ustahimilivu, juu ya utetezi wa uhai na juu ya upendo usiokoma. Mafunzo yamehifadhiwa na asili kwa viumbe wote wenye udadisi kuyafaidi na kujifunza.

Asili ina Nguvu zisizokoma zinazofanya kustajaabisha namna mambo hufanyika. Kila eneo la asili linaloonekana na lisiloonekana limefanywa katika nishati. Nishati au nguvu zimebeba maana ya maisha na nguvu hii haiharibiwi na chochote isipokuwa hubadilika umbile lake. Kila kitu unachokiona ni nishati kwa udogo wake. Karatasi unayoiona nayo ni nishati tulivu ambayo inaweza kubadilika kuwa nishati mwanga, sauti au joto. Choma karatasi ambalo awali uliona ni tulivu lisilo na madhara uone namna karatasi hilo linawaka, linaang’aza na kutoa sauti. Watu wote wanaojua wao ni sehemu ya hii Nguvu ya Asili hufanya mambo makubwa yasowezwa kupimwa.

Asili ina utajiri na utele kwa viumbe wake wote na haiwezi kukaukiwa kwa kuwa inatoa isivyo kawaida. Hutaona asili inaishiwa isipokuwa watu wanaokaa wanaweza tu kuharibu maumbile kwa hasara tunayoitengeneza wenyewe. Walio na utulivu na kupenda kuithamini asili basi ina wingi wa utajiri wa mambo yasowezwa kumalizwa na mtu awaye yeyote kwa mara moja. Kila kitu unachokiona kipo kwa ukubwa usioweza kubebeka. Unaweza kusema umeona mtu ni mkarimu au mwenye upendo ila hujakutana na mtu mwenye upendo kuzidi huyo.

Unajifunzaje kujihusu wewe kupitia asili?, tumeona asili ina nguvu na kuwa kila kilichomo ni nishati au nguvu ilofichwa katika maumbile tu. Watu wote bila kujali chochote kwa maana ya jinsi, umri au utaifa kuna nguvu ndani yetu. Kila kitu chenye umbile kina nguvu iliyofichika ndani yake. Nguvu ndio kiini cha maisha na matokeo makubwa yoyote tunayoyaona. Iwe ni ubunifu, kuamka kiroho, ugunduzi na utoaji ni muunganiko wa nguvu zilizopo ndani yetu zilizo mamoja na asili na mazingira yanayotunguka. Kadri unavyojifunza asili iwe kwa kutazama kwa utulivu na kupata kuzijua siri na ajabu zake, au kufanya tahajudi ndivyo unavyojikuta u sehemu moja na asili na huu ndio mwanzo wa kujua kusudi kubwa la uwepo wa mtu kuwa hapa Duniani.

Kusudi la mtu lipo katika nguvu ambayo inafanya njia kwa ajili ya watu wengine “Mtengeneza Njia”. Si watu wote hupata nafasi ya kuamka “uwezo wa kuona mbali” na kujitambua kuwa wana nguvu na wana uwezo fulani wa kufanya makubwa. Watu wanaopata nafasi ya kujitambua husaidia na wengine wajitambue na wajifahamu zaidi walivyo. Hili ni zao kubwa la kila anayejibiidisha kujifunza kutokana na asili na ulimwengu.

Tenga muda katika maisha yako kuwa na utulivu wa kutembelea maeneo tulivu kama mbuga, mashamba, misitu, sehemu za milima na pata saa za kutafakari na kutuliza akili uone namna asili iko karibu na wewe na inao utajiri mkubwa, upendo, makazi na nguvu kubwa ya kusaidia watu kuelekea kujitambua na kuamka kihisia, kimwili, kiakili hadi kiroho.

KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU

WhatsApp +255 716  924 136

No comments:

Post a Comment