Wednesday, May 20, 2020

HAMISHA TABIA ZA AJIRA KWENDA KWENYE KUJIAJIRI UTAFANIKIWA SANA.

Tabia hizo kumi ni kama ifuatavyo;
(1).UNAENDA  KILA SIKU.

Kila siku ambayo ni ya kazi, unaenda kazini. Haijalishi kama unajisikia au hujisikii, umechoka au hujachoka, ni siku ya kazi na unaenda kazini. Na ili kuhakikisha unaenda, sehemu za kazi kuna daftari au mashine ya kuweka sahihi, ili kuthibitisha kwamba kweli umefika kazini.

Unapojiajiri, hakikisha kila siku ya kazi ambayo umejipangia kulingana na kile unachofanya basi unaenda kwenye eneo lako la kazi. Japokuwa una uhuru wa kwenda au kutokwenda, usiutumie kabisa uhuru huo, wewe nenda, iwe unajisikia au hujisikii, iwe umechoka au la. Chukulia kuna bosi anakusubiria pale, na hawezi kukuelewa kama hujaenda.
(2). CHANGAMOTO  ZA  MAISHA  HAZIINGILII  KAZI.
Usiku umegombana na mke wako au mume wako, asubuhi unaamka na kujiandaa kwenda kazini. Hukai nyumbani na kumwambia bosi leo huendi kwa sababu kuna ugomvi nyumbani. Umeamka una mafua makali unajiandaa na kwenda kazini, husemi mafua haya wacha nipone kwanza. Mwajiri wako hawezi kukuelewa.

Peleka tabia hiyo kwenye kujiajiri pia, usikubali sababu ndogo ndogo zinazoendelea kwenye maisha yako kuingilia kazi zako. Endelea na kazi kila siku, kama ambavyo ungeenda kwenye kazi ukiwa umeajiriwa. 
(3). UNAKAA  KAZINI  MUDA  WA  KAZI.
Unaenda kazini kila siku, na ukifika, unakaa mpaka muda wa kazi uishe ndiyo unaondoka. Hata kama siku hiyo huna kazi za kufanya, utakaa hapo kazini mpaka muda wa kutoka ufike. Hata kama siku hiyo hujisikii kufanya kazi, utazurura zurura hapo ofisini mpaka muda wa kutoka ufike. Hutakatisha siku yako ya kazi kwa sababu tu hujisikii, siku ya kazi inaisha muda wa kazi unapoisha.

Hamishia hili kwenye kujiajiri, kwenye muda uliopanga kufanya kazi yako, fanya kazi na usiruhusu kuingiliwa na kitu kingine. Kama umepanga utaandika kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa sita mchana, basi fanya hivyo. Usiahirishe kwa sababu siku hiyo hujisikii kuandika. Kama umepanga utafungua biashara yako saa moja asubuhi na kufunga saa moja jioni fanya hivyo, isitokee siku unafunga saa 10 kwa sababu siku hiyo umechoka zaidi. Jiulize kama ingekuwa kazi ya kuajiriwa je ungeacha, kama hapana, fanya.
( 4 ).UNAFANYA  KAZI  KWA MIAKA  MINGI.
Kazi yoyote unayoifanya, utaifanya kwa miaka mingi. Kama ni mwalimu utafundisha kwa miaka mingi, unaweza kuhama shule mbalimbali, lakini utafundisha. Kama wewe ni daktari utatibu kwa miaka mingi, unaweza kubadili vituo vya kazi, lakini utatibu. Utafanya kazi yako mpaka pale utakapostaafu au kufikia uhuru wa kifedha. Na hufikirii kuifanya kwa muda mchache na isipolipa unaacha, unaifanya kwa miaka mingi.

Peleka tabia hiyo kwenye kujiajiri pia, kile unachochagua kufanya, jiandae kukifanya kwa miaka mingi. Kama ni uandishi, jua utaandika kwa miaka mingi, kama ni biashara pia, jipe muda mrefu wa kufanya. Acha kabisa kujidanganya kwamba utafanya kwa siku chache na kama hailipi utaacha. Jiandae kufanya kwa muda mrefu.
( 5 ). UNA  MAHITAJI  MAKUBWA.
Kinachokufanya uendelee kuifanya kazi yako, hata kama ni ngumu au huipendi ni mahitaji makubwa uliyonayo. Unahitaji fedha ya kuendesha maisha yako, kula, kulala, kuvaa, kuendesha familia, kusomesha watoto na mengine. Una ndugu wanaokutegemea ambapo kazi yako ndiyo inakuwezesha kuwasaidia. Mwajiri akikuambia fanya tu kwa upendo hakuna haja ya malipo huwezi kumwelewa, una mahitaji, unataka fedha, unafanya kazi ili ulipwe.

Chochote unachofanya pale unapojiajiri, hakikisha unalipwa ili uweze kuendesha maisha yako. Na hili ni muhimu sana kwenye kazi za sanaa, ni rahisi kujiambia naandika kwa sababu napenda, siyo kwa sababu nataka kulipwa. Andika ili ulipwe, una mahitaji ya maisha yako, unafikiri utayamudu vipi kama unachofanya hakikulipi?
(6 ). UNAKUBALI MALIPO  YA  KAZI.
Unapoomba kazi, cha kwanza unachouliza ni mshahara. Unapofanya kazi hiyo kwa muda unamtaka mwajiri wako akuongeze mshahara. Unaenda kusoma au kuongeza ujuzi ili upate mshahara zaidi. Unafanya kazi muda wa ziada ili upate malipo zaidi.

Peleka tabia hii kwenye kujiajiri pia, hakikisha unapata malipo na kila wakati kazana kutoa thamani zaidi ili ulipwe zaidi. Weka juhudi kubwa ili kupata malipo makubwa. Na asikusumbue mtu kwamba unataka sana kulipwa, kama hayupo tayari kulipia achana naye. Hufanyi unachofanya kuuza sura, ndiyo kinawasaidia watu, lakini asante haitaleta chakula mezani, hakikisha unalipwa.

( 7 ). KAZI   YAKO  SIYO  WEWE.
Kama wewe ni mwalimu, unajua kabisa ualimu wako unaishia shuleni, hukutani na watoto barabarani na ukaanza kuwafundisha hapo hapo. Kama ni daktari udaktari wako unaishia hospitali, hupandi kwenye daladala na kuanza kuwatibu watu. Kwa kifupi ni kwamba unapokuwa umeajiriwa, unajua kuyatenganisha maisha yako binafsi na maisha ya kazi, huchanganyi hivyo pamoja.

Hapa ndipo wengi waliojiajiri huwa wanafeli, hawajitofautishi wao binafsi na kazi zao. Kila wakati wanachanganya kazi na maisha, na ndiyo maana hawapati muda wa kupumzika. Hivyo kwa kile ambacho umejiajiri kufanya, tenga muda wa kukifanya na tenga muda wa maisha pia. Kushindwa kufanya hivyo, utachoka haraka na kushindwa kuendelea. 
(8). UNAJUA  MBINU  ZA  KUFANYA  KAZI.
Kama wewe ni mwalimu, unajua mbinu za ualimu, njia za kufundisha watu mpaka waelewe na pia unaendelea kujifunza. Kama wewe ni daktari, unajua jinsi ya kudadisi dalili za mgonjwa, vipimo gani ufanye mpaka ujue mgonjwa anaumwa nini na kisha umpe matibabu sahihi. Huamki siku moja na kujiita daktari kisha ukaanza kutibu, unajifunza.

Peleka tabia hii kwenye kile unachojiajiri kufanya, mwanzoni jua kabisa ni muda wa kujifunza, kuzijua njia bora za kufanya kitu hicho na kila wakati kazana kujua mbinu bora zaidi. Unafanya vizuri pale unapokuwa na ujuzi wa kufanya. Hivyo jifunze ujuzi wa kile ulichojiajiri kufanya.
(9 ). UNA UCHESHI  AU  UTANI  KWENYE  KAZI.
Kwa kila kazi, kuna utani fulani upo, ambao huwa haukuumizi. Utani huo unaweza kuonekana kama ni kejeli, lakini haukusumbui. Mfano baina ya madaktari, huwa wanataniana sana, mfano daktari wa upasuaji atamuita daktari wa magonjwa ya ndani ni mtu wa kubahatisha, maana anatibu kitu ambacho hakioni. Daktari wa magonjwa ya ndani atamuita daktari wa upasuaji kama mtu wa buchani, kazi yake ni kukata vitu. Huu ni utani ambao upo na madaktari hao hawapigani kwa sababu ya utani huo.

Tuhusu utani au ucheshi kwenye kile ambacho umejiajiri kufanya. Kuna watu watachukulia hiyo kama sehemu ya kukudhihaki au kukukejeli, lakini wewe utachukulia ni kama utani tu na utaendelea kufanya. Mfano unaweza kuwa mwandishi na watu wakakuambia unachoandika ni nadharia tu, hakiwezekani kwa vitendo. Usichukulie kwa umakini sana hilo, ona kama ni utani na endelea kuandika.
(10 ). UNAPOKEA  SIFA  NA  LAWAMA  KWA  KAZI  UNAYOFANYA.
Ukiwa kwenye ajira, unaweza kufanya kazi yako vizuri na ukasifiwa sana, wakati mwingine unakosolewa na kulaumiwa kupitia kazi yako. Unajua hiyo ni sehemu ya kazi, hivyo huendi nyumbani na kukosa usingizi kwa sababu bosi wako amekuambia ripoti uliyoadika siyo sahihi. Unajua kesho utaenda kufanya marekebisho kama alivyokuambia, ni sehemu ya kazi.

Peleka tabia hii kwenye kujiajiri pia. Kwa kila unachofanya, jua kuna wakati itasifiwa na kuna wakati utapingwa, kukosolewa au kulaumiwa. Kuwa tayari kupokea hayo na kuchukua hatua sahihi. Usiache kuandika kwa sababu mtu amekuambia makala yako au kitabu chako ni cha hovyo, jua kipi hakipo sahihi na boresha zaidi kwenye uandishi ujao.

2 comments:

  1. Watu wengi waliopo kwenye ajira huwa wanatamani sana kuondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri wenyewe. Inaweza kuwa ni kupitia biashara au vipaji vya kisanii walivyonavyo kama uandishi, uchoraji, unenaji na kadhalika.

    Lakini wengi wa wanaotoka kwenye ajira na kwenda kuajiri, huwa wanashindwa kufanikiwa. Hii ni kwa sababu mazingira ya kujiajiri, ambapo mtu unajisimamia mwenyewe ni tofauti kabisa na mazingira ya kuajiriwa ambapo mtu unasimamiwa na wengine.

    Kwa asili, sisi binadamu ni wavivu, huwa hatupendi kufanya kazi ngumu, hivyo inapokuwa chini ya uamuzi wetu wenyewe, huwa tunaahirisha kazi yoyote ambayo ni ngumu. Ndiyo maana hata kwenye ajira, majukumu mengi hufanywa pale mwisho wa kuyafanya unapokuwa umefika.

    Ukipewa wiki moja ya kuandika ripoti, siku tatu za kwanza hutaigusa kabisa, siku ya nne na ya tano utapanga jinsi ya kuiandaa. Siku ya sita utaanza kuifanya lakini hutapiga hatua sana. Lakini inapofika siku ya saba, siku ambayo lazima ripoti ikamilike, hapo utafanya kazi kwa mfululizo bila kuruhusu usumbufu wowote, ikibidi utaongeza muda wa kufanya kazi.

    Ripoti uliyokuwa na siku saba za kuifanya, umeifanya ndani ya siku moja. Je huo siyo muujiza? HAMISHIA TABIA HIZO UNAZOZIFANYA KATIKA AJIRA YAKO KWENDA KWENYE KUJIAJIRI----WENGI HUANGUKA HAPA ! BADILIKA SASA NA FANYA KAZI KWA BIDII

    ReplyDelete