Friday, January 17, 2020

HATUA O4 ZA KUPATA UHURU WA MUDA , FEDHA NA ENEO ILI KUWA NA MAISHA YA MAFANIKIO

Kupata uhuru kamili kwenye maisha ni mtego ambao wengi wamekuwa wananasa.
Chukua mfano huu, mtu aliyeajiriwa anafanya kazi kwa juhudi, ili atoe thamani zaidi na hilo lipelekee yeye kulipwa zaidi. Kwa juhudi anazoweka, mwajiri wake anaona anastahili kulipwa zaidi, hivyo anampandisha cheo na kumwongezea mshahara. Lakini cheo anachopandishwa kinakuja na majukumu zaidi, hivyo licha ya kipato kuongezeka, mtu huyo anazidi kukosa muda na hivyo anakosa uhuru na maisha yake.
Kadhalika kwenye biashara, mtu anaanza biashara ndogo, ambayo inampa muda mwingi wa kufanya mambo yake, biashara inakua, wateja wanaongezeka na faida inaongezeka pia, lakini hilo linamtaka atumie muda zaidi kwenye biashara. Wingi wa wateja unakuja na changamoto nyingi za wateja hao ambazo zinampa kazi zaidi. Hivyo licha ya biashara kukua na kipato kuongezeka, uhuru unazidi kupungua kwa sababu muda wa kufanya mambo mengine kwenye maisha yake unakuwa haupo.
Tusipokuwa makini, tutakuwa tunakimbiza uhuru kama kipepeo ambacho kinakimbilia maua mazuri, kila wakati utaona nikipiga hatua hii nitakuwa huru na unaishia kukosa uhuru zaidi.
Ili kuweza kupata uhuru kamili wa maisha yetu, ambao unajumuisha uhuru wa muda, uhuru wa fedha na uhuru a eneo, kuna hatua nne za kuchukua.
Hatua hizi nne tumeshirikishwa na Tim Ferriss kwenye kitabu chake cha THE 4-HOUR WORK WEEK.
Hapa nakwenda kukushirikisha hatua hizo nne kwa ufupi,
Karibu kwenye hatua nne za kuchukua ili kupata uhuru kamili wa maisha yako.
HATUA YA KWANZA NI D  (DEFINITION)
Hapa unabadili sheria na kanuni zote za mchezo wa kazi au biashara na kujiwekea utaratibu wako mpya ambao utautumia kuendesha maisha ya tofauti kwako kwenye eneo la kazi.
Baadhi ya mambo ya kubadili ni kutokusubiri mpaka uzeeke ndiyo upate mapumziko kupitia kustaafu, badala yake tengeneza mapumziko mafupi kwenye maisha yako ya sasa.
Pia jua maana halisi ya mafanikio kwako, unajipimaje kwamba umefanikiwa, na siyo kujilinganisha na wengine au kuiga yale ambayo wengine wanafanya.
Kwa kifupi, jua hasa kile unachokitaka na jinsi ambavyo utakipata kwa namna ambayo ni bora kwako.
HATUA YA PILI NI E  (ELIMINATION)
Hapa unakwenda kufuta mambo yote yasiyo muhimu na ambayo yanachukua muda wakoi mwingi, hivyo kubaki na machache muhimu ambayo yanachukua muda wako mchache. Hapa ndipo unapokwenda kupunguza sana muda wako wa kazi na kupata uhuru wa kwanza ambao ni MUDA.
Kuna sheria mbili ambazo Tim ametushirikisha kwenye hatua hii;
Sheria ya kwanza ni ya Pareto (80/20) ambayo inasema asilimia 80 ya matokeo inatokana na asilimia 20 ya juhudi, hivyo kuna mambo machache yanayoleta matokeo makubwa na tunapaswa kufanya hayo tu.
Sheria ya pili ni ya Parkinson, ambayo inasema jukumu huwa linameza muda ambao limepangiwa, hivyo tunapaswa kujiwekea muda mdogo wa kukamilisha majukumu yetu ili tuache kupoteza muda.
Kwenye uchambuzi wa kitabu hili utajifunza vizuri jinsi ya kutumia sheria hizi kwa pamoja ili ziwe na manufaa kwako.
HATUA YA TATU NI A (AUTOMATION)
Hapa unatengeneza mpango wa kulipwa hata kama wewe haupo, unajenga misingi ya kuiwezesha biashara au kazi yako kujiendesha yenyewe hata kama wewe haupo na wewe kupokea fedha. Kupitia hatua hii, unapata uhuru wa pili ambao ni FEDHA.
Kikwazo cha kwanza kwenye uhuru wako ni wewe mwenyewe. Umeshajiweka sana kwenye kile unachofanya kiasi kwamba hakiwezi kwenda bila ya wewe kuwepo na ndiyo maana kila hatua unayopiga unazidi kupoteza uhuru wako.
Unapaswa kuweka mfumo unaoiwezesha kazi au biashara yako kujiendesha yenyewe hata kama wewe haupo.
HATUA YA NNE NI L (LIBERATION)
Hapa unapata uhuru kamili wa maisha yako, kwa kuweza kuwa eneo lolote duniani huku kazi au biashara yako ikiendelea kujiendesha yenyewe na fedha zikiingia. Hapa unapata uhuru wa tatu ambao ni wa ENEO.
Baada ya kuamua mafanikio yana maana gani kwako, kuachana na yasiyo muhimu na kutengeneza mfumo wa biashara yako kwenda hata kama haupo, sasa unakuwa huru na maisha yako, na unaweza kuchagua kuwa eneo lolote kwa wakati wowote unaotaka wewe. Na huu ndiyo uhuru kamili ambao wengi hawapati nafasi ya kuufikia kwenye maisha yao. Lakini wewe unaweza kuufikia kama utafanyia kazi maarifa haya uliyoyapata.
Kwa pamoja, hatua hizi nne zinatupa neno DEAL, ambapo ni kutengeneza mpango mpya, kufuta yasiyo muhimu, kuiwezesha kazi kwenda bila wewe kuwepo na kuwa huru kusafiri kwenda popote.
Katika utekelezaji wa hatua hizi nne, Tim anashauri waliojiajiri kutumia mtiririko huo wa DEAL, lakini walioajiriwa kutumia mtiririko wa DELA, yaani kwa waajiriwa, kabla hajaweza kutengeneza njia ya kazi yake kwenda bila ya yeye kuwepo, anapaswa kutengeneza kwanza uhuru wa kutokuwepo kwenye kazi.

No comments:

Post a Comment