Sunday, January 12, 2020

ACHANA NA ULIMBUKENI WA KUFANYA KILA AINA YA FURSA MPYA UNAYOKUTANA NAYO , UTALIA -----COACH MWL JAPHET MASATU

Kuna wakati kila mtu alikuwa anakimbizana na fursa mpya ya ufugaji wa kware, ikaja ufugaji wa sungura, ikaja pesa za kidijitaji (cryptocurrency), ikaja forex. Hapo bado kuna vingine ambavyo huwa vinakuja na kupoteza, kama biashara za mtandao, kilimo na ufugaji na kadhalika.
Iko hivi rafiki, biashara huwa hazitofautiani sana, bali tamaa za watu ndiyo zinatofautiana. Hakuna biashara ambayo ni nzuri zaidi ya nyingine, bali uzuri wa biashara unategemea ni nani anayeifanya.
Msingi wa kwanza wa kufanikiwa kwenye biashara yoyote ile, ni kuwa tayari kujituma zaidi kwenye biashara hiyo zaidi ya wengine, kuijua kwa undani kuliko wengine. Na hili linakuwa rahisi kama mtu ataipenda biashara ambayo anaifanya, hapo atajituma zaidi na atapenda kuifuatilia kwa karibu na hivyo kuijua zaidi.
Ili kuachana na umalaya wa fursa mpya, zingatia haya yafuatayo;
( 1 ). Anza na kusudi kuu la maisha yako.
Kabla hujaamua ni biashara au kazi gani ufanye, jua lipi kusudi la maisha yako. Unapaswa kujua ni kitu gani uko hapa duniani kukifanya. Na hili utalijua kupitia vitu unavyopenda kufanya au vitu unavyovijali sana. Hata vipaji ulivyonavyo vinaashiria kusudi lako.
Kwa kulijua kusudi la maisha yako, hapo unaweza kuangalia ni biashara au kazi gani inayoendana na kusudi hilo, na hivyo ukiifanya, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa kuliko ukifanya kitu kingine.
( 2 ). Jiwekee maono makubwa.
Baada ya kujua kusudi, unapaswa kujiwekea maono, kwamba miaka kadhaa ijayo unajiona uko wapi. Jiwekee maono makubwa ya maisha yao, kwamba unajiona ukiwa wapi, ili maisha yako yawe na maana, unajiona ukifanya nini kila siku, maisha yako yakiwaje.
Ukishakuwa na maono, ni rahisi kuchagua biashara zipi zinazokufikisha kwenye maono hayo. Hutakimbilia kujaribu kila aina ya biashara, kwa sababu tayari unajua wapi unapotaka kufika.
( 3 ). Weka malengo ya kufikia maono yako.
Maono ni picha ya mbali, kitakachokufikisha kwenye picha hiyo ni malengo na mipango ambayo unakuwa umejiwekea. Hivyo unapaswa kuweka malengo ya kukufikisha kwenye maono uliyonayo.
Malengo yanapaswa kuwa ya muda mfupi, miezi, mwaka, mpaka miaka 2 na ya muda mrefu, miaka mitano, 10, 20 na kuendelea. Unapoweka malengo, unachagua kwa uhakika unatakaje kufika kwenye maono uliyonayo. Hivyo hata biashara utakazochagua, utaanza na malengo uliyojiwekea.
( 4 ). Komaa na malengo yako na mchakato wa kuyafikia.
Ukishakuwa na malengo, sasa hiyo ndiyo ramani yako, usihangaike na kitu kingine chochote. Wewe komaa na malengo uliyojiwekea na mchakato wa kuyafikia. Unapokutana na fursa mpya jiulize je hii ipo kwenye malengo yangu, kama haipo achana nayo na rudi kwenye malengo yako.
Malengo yanakupa wewe nidhamu ya kusimamia kitu kimoja mpaka kitimie, kwa sababu kuna muda uliojiwekea. Unahangaika na fursa mpya kila siku kwa sababu hakuna malengo unayofanyia kazi, hivyo chochote kipya kinachokuja huwezi kukikataa.
( 5 ). Acha tamaa na kutaka mafanikio ya haraka.
Rafiki, nina habari ambazo siyo njema sana kwako, hakuna mafanikio rahisi, ya haraka na yasiyohitaji kazi. Huo ni uongo ambao umewanasa wengi wenye tamaa na kuishia kutapeliwa. Jua kabisa kwamba kila biashara inahitaji kazi, muda, ujuzi na uvumilivu mkubwa. Haijalishi watu wanakuambia inalipa kiasi gani, usidanganyike, jua hakuna mafanikio bila ya uwekezaji mkubwa wa kazi, nguvu, muda na maumivu.
Hivyo mtu anapokuja kwako na fursa mpya, akikuambia hii inalipa sana, muulize ni gharama gani unapaswa kulipa kwa upande wa kazi, muda, ujuzi, nguvu na hata maumivu. Kama atakuambia hii ni rahisi, huhitaji hata kufanya kazi, kimbia haraka, unaingizwa kwenye utapeli.
( 6 ).Usisikilize maneno, angalia matokeo.
Mtu anapokuja kwako na kukuambia fursa fulani inalipa sana na unapaswa kuifanya, mwambie akuoneshe jinsi ambavyo yeye inamlipa. Kama ni fedha akuoneshe hizo fedha alizonazo ambazo amepata kwenye fursa hiyo mpya. Kadhalika kama ni mali pia akuoneshe.
Wengi wanaotangaza fursa mpya na wanazosema zinalipa, wao wenyewe zinakuwa hazijawalipa, ila wanakushawishi wewe uingie ili wanufaike kupitia wewe. Mfano mtu anayekuambia kware ni fursa inayolipa, unakuta yeye ndiye anayekuuzia mayai au kware wenyewe, hivyo ananufaika kupitia wewe kuhamasika na fursa.
Chunga sana, unapoambiwa kuna fursa mpya, mara nyingi wewe ndiye unayekuwa fursa yenyewe.
( 7 ). Rudi kwenye msingi mkuu wa biashara ambao ni thamani.
Rafiki, msingi mkuu wa biashara ni huu; mabadilishano ya fedha kwa thamani. Yaani kuna mtu mmoja ana fedha na ana uhitaji, halafu kuna mtu mwingine anaweza kutimiza uhitaji wake na anahitaji fedha, hapo sasa ndipo biashara inapofanyika. Kama hakuna thamani ambayo mtu anaihitaji, hakuna biashara.
Hivyo kwa kila fursa mpya unayokutana nayo, jiulize ni thamani gani ambayo utatoa kwa watu wenye uhitaji na kisha wewe ukapata fedha. Ukianza na biashara ya Forex ambayo imeulizwa hapa, jiulize kwa watu unaowafahamu wewe, forex inaongeza thamani gani kwao kiasi kwamba watakuwa tayari kukulipa wewe fedha. Utapata jibu ni hakuna.
Kadhalika kwenye vitu unavyoambiwa ni fursa kama ufugaji wa kware au sungura, jiulize wewe mwenyewe na wale wanaokuzunguka, ni lini umewahi kutafuta sana nyama ya sungura kwa sababu unaipenda sana? Jibu ni hakuna, lakini anakuja mtu anakuambia hii ni dili, na wewe unakubali!
Kama unaambiwa kitu ni fursa, lakini wewe mwenyewe hujawahi kuwa na uhitaji nacho, na hata wale wanaokuzunguka hawana uhitaji nacho, jua wewe ndiye fursa rafiki yangu, na kaa mbali.
Rudi kwenye msingi mkuu wa biashara, angalia kile ambacho tayari kina uhitaji. Badala ya kukimbizana na kware au sungura, fanya ufugaji wa kuku, kuku amekuwa kitoweo kwa kila mtu tangu enzi na enzi, huhitaji kumfundisha mtu faida za kula kuku au mayai ndiyo akuelewe na kununua. Ukiwa na kuku au mayai mazuri, kwa bei ambayo watu wanaweza kuimudu, una biashara.
Rafiki, watu wengi wanayumbishwa na fursa mpya kwa sababu hawana msimamo kwenye maisha yao, hawajui wanataka nini na hawajajipanga ni kwa namna gani watakipata, ndiyo maana kila kipya kinachokuja wanaona ndiyo tumaini lao. Ondoka kwenye hali hiyo sasa na jua nini hasa unataka kwenye maisha yako, jinsi gani utakipata na kisha kuwa na msimamo katika kuchukua hatua. Kila la kheri.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako
Mwl    Japhet   Masatu

No comments:

Post a Comment