Tuesday, June 7, 2016

MWALIMU NYERERE HAKUWA MDINI -- GERALD NYERERE

Kushoto: John Rupia, Julius Nyerere na Zuberi Mtemvu
Nyuma ni vijana wa Bantu Group walinzi wa Nyerere wakati wa kupigania
uhuru wa Tanganyika 1954 - 1961
Picha kwa hisani ya Abdulrahman Msham 
Utangulizi

Kijana msomi Chambi Chachage kaniletea hayo niliyoweka hapo chini akiniuliza kama ninayajua. Mimi nikamwandikia Gerald Nyerere moja kwa moja mwandishi Gerald Nyerere kumuomba ruksa niweke maandiko yake kuhusu Baba wa Taifa na msimamo wake katika dini hapa. 

Gerald Nyerere ameniruhusu akisema kuwa ni vizuri wengi wakayajua haya.
Mohamed Said

Kaka Chambi,


Asante kwa kuniuliza.

Hapa naomba nieleze kwa ufupi zaidi na kaka Madaraka anaweza kuongezea na kurekebisha pale nilipokosea.

Mwalimu Nyerere hakuwa mdini na ameongoza taifa letu pasipo kuingiza udini. Kabla ya harakati za Uhuru, Mwalimu bado alikuwa na mchanganyiko huu wa dini. Babu yetu, mtemi/chifu Nyerere Burito wa himaya ya Uzanaki/Butiama japo hakuwa na dini alikula yamini (affirmation) na chifu wa himaya jirani ya Ikizu, mtemi/chifu Makongoro ambaye alikuwa ni Mwislamu. Kwa hiyo ukoo wa Nyerere na ukoo wa Makongoro ni ndugu hadi leo hii.

Babu yangu, mzee Ali Nyabange kutoka utemi/uchifu wa Nyabange karibu na Musoma mjini alikuwa ni Mwislamu na amefariki mwaka 2000 akiwa ni Mwislamu. Mama yangu mzazi, Joha Janeth Nyabange alikuwa ni Mwislamu na alifunga ndoa ya kimila na Baba yangu Mzee Josephat Kiboko bila kuacha Uislamu wake mpaka alipobatizwa mwaka 1988 tukiwa Morogoro kabla ya kufariki mwaka 1994. Mama yangu alikuwa ni Mwaislamu na baadaye alibatizwa na kuwa Mkristo.

Bibi yetu, Christina Mgaya wa Nyangombe ndiye aliyependekeza mama yangu Joha Nyabange aolewe baada ya kumtembelea babu yangu Mzee Ali Nyabange na kumchagua mama yangu kutoka katika binti watatu wa Mzee Ali Nyabange mjini Musoma. Harusi ilifanyikia Musoma na baadaye Butiama na Mwalimu Nyerere kutoa baraka zote na mwenyewe kugharamia ndoa hiyo.

Babu yetu, Mzee Nyerere Burito hakukubali kabisa dini kuingia kwenye himaya yake ya Uzanaki. Na Mwalimu aliheshimu hivyo. Mpaka miaka ya 1980 Butiama hakukuwa na kanisa wala msikiti. Mwalimu Nyerere alipokuwa Butiama ilibidi awe anaenda kusali  kijiji jirani cha Magorombe maeneo ya Buswege ambapo kulikuwa na Kanisa Katoliki, Parokia ya Zanaki (Zanaki Parish). Kanisa Katoliki Butiama (Butiama Parish) limeanza na kutoa huduma za kichungaji mwaka 1993.

Mwalimu Nyerere wakati akijiandaa na safari ya kwenda kumtembelea Rais wa Libya, Muammar Ghadafi hiyo miaka ya 1990 aliwaita viongozi wa Msikiti pale Butiama kuwauliza nini wangependa awasaidie, na mmoja wa viongozi wale akiwemo Iddi, mpishi wa muda mrefu wa Mwalimu Nyerere aliomba wajengewe Msikiti. Hivyo Msikiti wa Butiama ulijengwa na kufunguliwa rasmi tarehe 13 Oktoba 2000 kwa msaada wa Muammar Ghadafi.

Mwalimu Nyerere aliwapenda watu wa dini zote Tanzania, Afrika na duniani kote bila kubagua, Mwalimu HAKUWA MDINI.


GN
 
CHANZO   CHA HABARI :  MOHAMED  SAID    WEBSITE , JUNE  07, 2016

No comments:

Post a Comment